MOROGORO-Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt.Anthony Diallo amelitaka Baraza la Wafanyakazi la mamlaka hiyo kujadili namna bora ya kutoa elimu ya mbolea kwa umma ili kuondoa fikra potofu kuwa mbolea inaharibu udongo.


Amesema, makadirio ya kiasi cha mbolea kinachohitajika kwa mwaka yatabadilika kutokana na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea itakayotolewa kwa wananchi ambao baada ya mafunzo wataona umuhimu wa kutumia mbolea na kuongeza tija kwenye kilimo chao.
Ametoa wito huo leo Februari 13, 2024 wakati akifungua kikao cha nne cha baraza la wafanyakazi kinachofanyika katika ukumbi wa Gairo ndani ya Hoteli ya Morena mjini Morogoro.
Aidha, amewataka wajumbe wa baraza hilo kujadili vyema makadirio ya bajeti ya mwaka 2024/2025 ili kuhakikisha inaendana na malengo ya mamlaka.
Pamoja na hayo, alieleza kuwa Bodi yake itahakikisha Mamlaka inatekeleza majukumu yake kulingana na malengo iliyojiwekea huku ikifuatilia taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka kila robo ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu yake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza, Bi. Happiness Mbelle ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti alimshukuru Mwenyekiti wa Bodi kwa kutenga muda na kufika kufungua kikao hicho.
Alieleza kuwa, mamlaka imepokea maelekezo, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa maslahi ya Mamlaka na Taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo (katikati) akiwa katika picha na viongozi wa Tughe tawi la TFRA, Mwakilishi kutoka TUGHE Makao Makuu, TUGHE Mkoa wa Dar Es Salaam na ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira. Kushoto kwa Mwenyekiti ni Kaimu Mkurugenzi wa TFRA na Mwenyekiti wa kikao cha Baraza, Bi. Victoria Elangwa.

Mwisho amewataka wajumbe kutekeleza lengo la kuja kushiriki kikao hicho na kutoa mapendekezo mazuri kwa bajeti inayoendelea kutekelezwa juu ya namna bora ya kuhakikisha kazi zilizopangwa zinatekelezeka.