Hotuba ya Waziri Mkuu wakati akihairisha Mkutano wa 14 wa Bunge la 12 leo


HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB.) WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA 14 WA BUNGE LA 12 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 16 FEBRUARI, 2024 BUNGENI JIJINI DODOMA

UTANGULIZI

Shukrani na Pongezi

Mheshimiwa Spika, wakati tukielekea kuhitimisha shughuli zote za Mkutano wa 14 wa Bunge la 12 hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutukirimia afya njema kwa kipindi chote cha majuma matatu ya kutekeleza majukumu ya shughuli za Bunge kwa mujibu wa ratiba.

Vilevile, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie heri na fanaka katika mwaka 2024 na kutuwezesha kutekeleza majukumu yote ya kitaifa kama yalivyopangwa.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake makubwa ambayo yameendelea kuchagiza kasi ya maendeleo ya Taifa letu.

Sote tumeshuhudia jitihada na dhamira yake njema ya kuleta mageuzi katika uchumi, utoaji wa huduma za jamii na kuimarisha ustawi wa kila mwananchi wa Tanzania.

Niwasisitize Watanzania wenzangu tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, katika utekelezaji wa maono aliyonayo kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, vilevile, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Phillip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukushukuru na kukupongeza sana wewe binafsi kwa kuendelea kuliongoza vema Bunge lako tukufu.

Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakubaliana nami kuwa Mheshimiwa Spika ameendelea kuonesha ukomavu, ustahimilivu na weledi wa hali ya juu katika kusimamia shughuli za Bunge pamoja mijadala yote kama ilivyopangwa katika Mkutano huu wa 14 tutakaouhitimisha hivi punde.

Hongera sana Mheshimiwa Spika kwa kutekeleza majukumu yako kwa viwango vya hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.), Naibu Spika kwa umahiri ambao ameendelea kuuonesha katika kutekeleza majukumu ya kukusadia wewe Mheshimiwa Spika kuliongoza Bunge lako tukufu.


Kipekee, niwapongeze pia, Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge ambao ni Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb.) na Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb.) kwa kazi nzuri wanayoifanya, ama kwa hakika wamekuwa nguzo kubwa na muhimu katika kutekeleza shughuli za mkutano huu wa Bunge.

Salamu za Pole Kufuatia Matukio Mbalimbali

Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mkutano huu wa 14 wa Bunge lako tukufu, mnamo tarehe 10 Februari, 2024 tuliondokewa na mpendwa wetu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, mwanasiasa mahiri aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nami niungane na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa salamu za pole kwa familia, kipekee kwa Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Fredrick Lowassa, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, wana CCM na Watanzania wote kwa ujumla.

Hayati Edward Lowassa atakumbukwa kwa uthubutu wake, uwezo, mvuto na ushawishi mkubwa wa kisiasa ndani na nje ya nchi yetu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa marehemu pumziko la amani. Amina.

Mheshimiwa Spika, niruhusu sasa nizungumze machache kuhusu utumishi wa mpendwa wetu Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Edward Lowassa akiwa Mbunge wa Jimbo la Monduli, alilitumikia Bunge la 10 katika nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika nusu ya kwanza ya uhai wa Bunge la 10 na katika nusu ya pili, akawa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Lowassa ilifanikiwa kutatua changamoto za baadhi ya ofisi za balozi zetu kuchelewa kupata mawasiliano hususan pale Balozi anapohitimisha muda wake.

Aidha, iliweza kuhakikisha kunakuwepo na mawasiliano ya haraka pamoja na kutatua suala la “Diplomatic Bags kutoa majibu kwa haraka.

Vilevile, Kamati hiyo ilianzisha utaratibu wa kutembelea ofisi za Balozi zetu katika nchi mbalimbali, jambo ambalo lilisaidia kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.

Mchango wa Hayati Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa katika nafasi yake ya Uwaziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wa Tisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Fredrick Tluway Sumaye.

Mheshimiwa Spika, Taifa litaendelea kumkumbuka Hayati Edward Ngoyai Lowassa kwa rekodi kubwa ya usimamizi wa shughuli za Serikali ikiwemo masuala yafuatayo:

Kusimamia ujenzi wa shule za sekondari katika kila Kata ambao uliwezesha watoto wengi waliofaulu elimu ya msingi kujiunga na elimu ya sekondari.

Kusimamia uamuzi wa kubadili Vyuo vya Ualimu vya Mkwawa na Changombe ili viwe vyuo vikuu vya ualimu.

Kuhimiza ujenzi wa zahanati katika kila kijiji na ujenzi wa vituo vya afya katika kila Kata.

Kuruhusu biashara ya pikipiki kubeba abiria jambo ambao lilisaidia vijana kupata ajira.

Kusimamia kikamilifu kuanzishwa kwa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES).

Kuhamasisha jamii ya wafugaji kupenda elimu kwa kuanzisha shule nyingi za sekondari katika maeneo yao.

Kutilia mkazo suala la elimu na kupiga vita mimba kwa wanafunzi.

Kusimamia uanzishwaji wa SACCOS hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, licha ya hayo, kati ya mwaka 1990 na 2005, Mheshimiwa Edward Lowassa amewahi kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Mahakama, Masuala ya Bunge na Uratibu wa Maafa; Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Mazingira na Kuondoa Umaskini; na Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo. Nafasi ambazo alizitumikia kwa weledi na ameacha alama kubwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, wakati taifa letu likiendelea na maombolezo, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuondokewa na Waheshimiwa Wabunge ambao waliwahi kushika nafasi mbalimbali za uwaziri.

Mnamo tarehe 12 Februari, 2024 tulipokea taarifa ya kuondokewa na Mheshimiwa Balozi Diodorus Kamala aliyefariki Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Kamala aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Waziri wa Afrika Mashariki na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Uholanzi.

Vilevile, tarehe 13 Februari, 2024 tulipokea taarifa ya kuondokewa na Dkt. Ibrahim Msabaha, aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha, Waziri wa Madini na Nishati lakini pia Waziri wa Afrika Mashariki.

Ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, wanaCCM na Watanzania wote kwa kuondokewa na wapendwa wetu.

Mheshimiwa Spika, hakika michango yao katika utumishi wa umma, utendaji Serikalini pamoja na kuwawakilisha Watanzania itaendelea kukumbukwa daima. Ninamuomba Mwenyezi Mungu awape marehemu pumziko la amani. Amina!

Mheshimiwa Spika, vilevile, nitumie nafasi hii kutoa salamu za pole kwa waathirika wote maafa yaliyotokea Hanang kufuatia maporomoko ya udongo katika Mlima Hanang yaliyogharimu maisha ya Watanzania wenzetu pamoja na kusababisha uharibifu wa mali na majeruhi.

Ninawasihi sana Watanzania wote tuendelee kuonesha uvumilivu, mshikamano na umoja wakati maafa yanapojitokeza ili kwa pamoja tuwe sehemu ya kurejesha hali kwa waathirika wote.

Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi karibuni nchi yetu pia ilikumbwa na mafuriko yaliyosababisha athari mbalimbali ikiwemo vifo, uharibifu wa mali na miundombinu.

Ninatoa pole kwa Watanzania wote waliopoteza wapendwa wao na wengine kujeruhiwa kutokana na mafuriko, lakini pia ninatoa pole kwa waathirika wa matukio mengine yakiwemo majanga ya moto na ajali za vyombo vya usafiri.

Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie majeruhi afya njema na awape marehemu pumziko la amani. Amina!

SHUGHULI ZA BUNGE

Maswali na Majibu

Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa 14 wa Bunge la 12, jumla ya maswali 224 ya msingi na mengine 871 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.

Pia, jumla ya maswali 12 yalielekezwa kwa Waziri Mkuu na kujibiwa kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa umahiri waliouonesha katika kufuatilia na kuisimamia Serikali, kwani maswali hayo yanasaidia kuikumbusha Serikali na kuifanya itoe ufafanuzi na kuchukua hatua katika masuala mbalimbali.

Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge

Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano huu, Bunge lako tukufu kwa sehemu kubwa lilikuwa na kazi ya kupokea na kujadili taarifa 16 za Kamati za Kudumu za Bunge. Taarifa hizo ni kama zifuatazo:

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kamati ya Bajeti;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kamati ya Hesabu za Serikali;

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kamati ya Hesabu ya Serikali za Mitaa; na

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Spika, katika taarifa hizi muhimu zilizowasilishwa na Kamati zetu, tumeshuhudia mijadala mizuri ambayo ilijielekeza kwenye kupanga maendeleo ya pamoja ya Taifa letu.

Aidha, Serikali imepokea maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika mkutano huu na inaahidi itayafanyia kazi.

Miswada ya Sheria

Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Bunge lako tukufu limepokea miswada minne ya Sheria na imepitishwa kwa hatua zote kama ifuatavyo:

Moja: Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2023;

Mbili: Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2023;

Tatu: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa ya mwaka 2023.

Nne: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na.5) ya mwaka 2023.

Taarifa za Serikali

Mheshimiwa Spika, tarehe 1 Februari, 2024 nilitumia Kanuni ya Kudumu ya Bunge toleo la Februari, 2023, Kanuni ya 44 kanuni ndogo ya 4 ambayo inatoa fursa kwa Waziri Mkuu kupitia kipindi cha maswali ya papo kwa papo kutoa taarifa kwenye jambo lenye maslahi kwa Taifa.

Hivyo, nilitumia fursa hiyo kutoa taarifa kuhusiana na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023 na Mitaala ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu.

MAENEO YA MSISITIZO

Maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo

Mheshimiwa Spika, ajenda ya maendeleo ya Taifa letu imefafanuliwa na inaongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kufikia ukomo mwezi Juni, 2026.

Hivyo, Serikali imeanzisha mchakato wa kuandaa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ambayo inatarajiwa kutoa mwongozo wa mwelekeo wa maendeleo wa nchi kwa kipindi cha miaka zaidi ya 25 ijayo.

Mheshimiwa Spika, kazi zinazofuata katika maandalizi ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ni pamoja na:

Elimu kwa umma kupitia kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wananchi kushiriki katika maandalizi ya Dira mpya;

Kukamilisha na kusambaza taarifa ya ukusanyaji maoni;

Uchambuzi wa taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025 kwa ajili ya maandalizi ya maandiko mahsusi ya kisera kwa ajili ya kuzingatiwa katika Dira mpya pamoja na kuainisha;

Kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali ambazo zitatoa taarifa katika uandishi wa Dira mpya;

Uchambuzi na majadiliano ya kina ya kitaalamu na wabobezi kwenye maeneo yatakayoongoza uandishi wa Dira;

Kujifunza uzoefu wa nchi mbalimbali zilizofanikiwa kufanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo katika maeneo ya sekta mbalimbali;

Uandishi wa Dira mpya na Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu; na Uidhinishaji wa Dira na Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, kidini na kikabila kushiriki kikamilifu kutoa maoni ili kuhakikisha uwepo wa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ambayo ni jumuishi na shirikishi.

Aidha, viongozi wote wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata/Shehia, Mitaa/Vijiji na vitongoji wahamasishe na kuelimisha wananchi wanaoishi katika maeneo yao ili washiriki kikamilifu katika kutoa maoni ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, vilevile, vyombo vya habari vitenge muda na kuweka kipaumbele katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika zoezi la kutoa maoni.

Andaeni vipindi na makala maalum ili kila mwananchi aweze kupata taarifa. Redio za jamii nazo zihusike kikamilifu kuelimisha umma.

Mheshimiwa Spika, kadhalika, sekta binafsi; asasi za kiraia, makundi maalum kama vile vijana, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na mashirikisho mengine yashirikiane na Tume ya Mipango katika uratibu wa ukusanyaji wa maoni ya wanachama na wadau wao.

Hii itasaidia kuhakikisha kuwa maoni ya makundi husika yanapokelewa na kujumuishwa katika maandalizi ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo.

Tahadhari Kuhusu Hali ya Chakula Kufuatia Mvua Kubwa

Mheshimiwa Spika, kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha uharibifu wa mazao, nitoe wito kwa wakulima wajielekeze katika kilimo cha mazao yanayoendana na hali ya hewa pamoja na kufuata maelekezo ya maafisa ugani walioko katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maafisa ugani wafuatilie kwa karibu taarifa za mara kwa mara za mwenendo wa hali ya hewa nchini.

Hii itawawezesha kuwa na wigo mpana wa kuwashauri wakulima mazao yanayofaa kulimwa katika maeneo yao pindi yanapotokea mabadiliko ya hali ya hewa.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia, kuwasisitiza wananchi kuhifadhi chakula cha kutosha na kuepuka matumizi ya chakula na yasiyokuwa ya lazima kutokana na uharibifu mkubwa wa mazao yaliyopo mashambani uliosababishwa mafuriko.

Uboreshaji wa Miundombinu Iliyoharibiwa na Mvua

Mheshimiwa Spika, naielekeza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kuendelea kujipanga na kuwa na utayari wa kukabiliana na changamoto za kukatika kwa mawasiliano ya barabara kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.

Mheshimiwa Spika, aidha, ziendelee kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kadri zinavyoendelea kutangazwa na Mamlaka ya Hali ya hewa.

Vilevile, Jeshi la Polisi liendelee kusimamia usalama wa barabara zetu na kuongoza vyombo vya moto ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kwenye barabara zinazoharibiwa na mvua.

Madereva nao wachukue tahadhari ya kutosha na kuwa na subira wanapoona maji yamefunika barabara na madaraja ili wasije kutumbukia kwenye maeneo yaliyomomonyoka.

Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuielekeza Ofisi ya Rais - TAMISEMI ishirikiane na wadau mbalimbali katika maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Wasimamizi wa maboresho ya daftari la mpigakura wahamasishe umma na kutoa elimu ya mpigakura kwa makundi yote katika jamii.

Lengo likiwa kuwafikia wananchi wote na kuwawezesha kuelewa sheria, kanuni, taratibu za mchakato mzima wa uchaguzi, wajibu wao na umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala la elimu ni muhimu katika kuongeza idadi ya wananchi watakaojiandikisha katika Daftari la Mpigakura na hatimaye kuwa na sifa ya kupiga wakati uchaguzi, nitumie fursa hii kutoa rai kwa Watanzania wote kushiriki katika hatua hii muhimu.

Watanzania wenzangu jitokezeni kwa wingi katika vituo vitakavyowekwa, jiandikisheni ili msipoteze haki yenu ya kupiga kura.

SEKTA YA MICHEZO

Mheshimiwa Spika, sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakubaliana nami kuwa nchi yetu imeendelea kupata mafanikio makubwa sana katika sekta ya utamaduni, sanaa na michezo.

Tumekuwa tukishuhudia mshiriki mmoja mmoja, vilabu ama timu zetu za Taifa zikifanya vizuri na kukonga nyoyo za washabiki na Watanzania kwa ujumla.

Hongereni sana wachezaji wote kwa kuwakilisha vema.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mpira wa miguu tumeshuhudia vilabu vyetu vikizidi kung’ara katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha, timu zetu za Taifa nazo zimeendelea kufanya vema. Kama mtakumbuka, kwa mara ya kwanza timu zetu zote za Taifa za mpira wa miguu za wanaume na wanawake (Taifa Stars) na Twiga Stars zilifanikiwa kufuzu Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) na WAFCON 2024.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Taifa Stars ilishindwa kusonga mbele kwenye hatua ya mtoano, ilionesha kiwango cha hali ya juu hususan kwenye michezo miwili ya kundi F lililohusisha timu za Morocco, DR Congo, Zambia na Tanzania.

Ninawapongeza sana wachezaji wote, walimu wao na kila mmoja aliyeshiriki kwa namna moja au nyingine katika hatua zote za mafanikio ya timu zetu za Taifa.

Ninaamini timu zetu zitaendelea kujifua na kufanya vema, kuwapa burudani Watanzania na kuliheshimisha soka la nchi yetu kimataifa.

Niliombe shirikisho la soka nchini kuendeleza mshikamano baina yake na wadau wa michezo, wachezaji na mabenchi ya ufundi ya timu zetu.

Mheshimiwa Spika, mafanikio ya timu zetu za Taifa yanahitaji uwekezaji mkubwa upande wa rasilimali fedha.

Kama mtakumbuka, mnamo tarehe 10 Januari, 2024 nilimwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika zoezi la harambee kwa ajili ya kukusanya fedha za kuzigharamia timu zetu za Taifa zinazotarajia kushiriki mashindano ya kimataifa.

Nitumie fursa hii kuwashukuru sana wadau wote wa michezo, taasisi za Serikali, wakuu wa mashirika na makampuni waliojitokeza kuchangia fedha na kutuwezesha kukusanya sh. bilioni 4.7.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kuwasihi sana Watanzania wote kuendelea kuchangia timu zetu za Taifa.

Zoezi la Harambee bado linaendelea Watanzania wote tuchangie kupitia namba zitakazotangazwa.

Wizara ya michezo bado inaendelea kuratibu zoezi la uchangiaji. Kama wahenga walivyosema Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu, tuunganishe nguvu za pamoja ili tuweze kufanikiwa na kuliheshimisha Taifa letu kupitia sekta ya michezo.

Tumewachagua wasanii maarufu wa kuhamasisha zoezi hili ambao ni Baba Levo, Mwijaku na Joti.

SHUKRANI NA KUTOA HOJA

Mheshimiwa Spika, nikiwa naelekea kuhitimisha hotuba yangu, naomba sasa niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuchangia katika mijadala iliyoendeshwa katika kipindi hiki cha Bunge.

Mmetoa ushauri na maoni ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kufanya maboresho katika utendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kadhalika ninawashukuru Katibu wa Bunge pamoja na watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa huduma zote walizotupatia katika kuhakikisha Mkutano huu unaendeshwa kwa mafanikio makubwa na kwa kuzingatia ratiba iliyopangwa.

Kipekee, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuwahakikishia wabunge na watendaji wengine usalama na amani wakati wote wa mkutano huu.

Mheshimiwa Spika, vilevile, niwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri pamoja na watendaji wote wa Serikali kwa kazi nzuri ya kuratibu shughuli zote zinazofanywa na sekta zetu kwa kutolea ufafanuzi hoja za Waheshimiwa Wabunge lakini pia kufanyia kazi masuala muhimu ambayo yamekuwa yakijitokeza wakati mijadala mbalimbali ikiendeshwa.

Aidha, ninawashukuru wanahabari ambao wakati wote wamekuwa wakihakikisha Watanzania wanapata habari kuhusu mwenendo wa utekelezaji wa shughuli zote za Bunge letu Tukufu kuanzia siku liliopoanza hata leo tunapoekea kuhitimisha.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru madereva wetu ambao wamefanya kazi kwa uadilifu mkubwa katika kipindi chote cha Mkutano huu.

Pia, ninawashukuru sana watu wote waliotoa huduma kwa namna moja au nyingine wakati Bunge hili likiendelea hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia, kuwatakia waumini wa Kikristo, mfungo mwema wa Kwaresma na sherehe njema ya sikukuu ya Pasaka.

Aidha, niwatakie Watanzania wote sherehe zenye amani na utulivu wakati wote wa mapumziko ya sikukuu ya Pasaka.

Kadhalika, ninawatakia waumini wa Kiislamu maandalizi mema ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Nitoe rai kwa wafanyabiashara wote kutopandisha bei za vyakula kiholela.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa ninapenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 02 Aprili, 2024 saa tatu kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu hapa Jijini Dodoma.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news