NA BONIFACE JACOB
HUENDA jina siyo geni masikioni kwako, ama umelisikia au kupita eneo maarufu Jijini Dar es Salaam, Wilaya ya Ubungo (zamani Kinondoni) na umekukutana na Jina hili mashuhuri.
Kwa bahati mbaya makosa ya kihistoria na jiografia yanataka kufanya Jina zuri la 'Riverside' kujulikana kwa sifa mbaya ya makao makuu madogo ya Dada poa.
Ukweli ni kwamba, eneo wanalosimama Madada poa na kutambulika kama 'Riverside' siyo eneo halisi la Riverside kimipaka, kihistoria au Kijiografia.
Pale wanaposimama madada poa ni Kata ya Ubungo ambayo nimekuwa,mtaa wa Ubungo Kisiwani,na hakuna uhusiano kabisa na Jina la Riverside.
Upande ule wa Kata ya Ubungo, mtaa wa Ubungo Kisiwani maeneo ya Zambezi bar na Chonya Inn (Bar) kuja hadi kituo cha mafuta cha Gudal ndipo wanaposimama madada poa mida ya Jioni.
Kituo cha Daladala cha eneo lile kinaitwa ZAMBEZI kwa Daladala zinazokwenda Buguruni, Tazara na Temeke mikoroshini.
Ukitoka Ubungo, kinakuka kituo cha zambezi,Kinafuata Bakwata (Micassa Bar) kinafuata Kwa teacher (Mabibo Hostel) Kinafuata External,Kinafuata Nyota gereji (Gereji),kinafuata Relini (Mwananchi) na kuendelea.
RIVERSIDE
Ni eneo 'Bar' maarufu iliyopo Wilaya ya Ubungo lakini ndani ya Kata ya Makuburi, mtaa wa Kibangu, upande wa kushoto wa barabara ya Mandela kama unatoka Buguruni/Tazara.
Baadae mwanzoni mwa miaka ya 1990 kikaanzishwa kituo cha daladala kikaitwa "Riverside" baada ya mradi wa barabara mbili ya Mandela na Kampuni ya KONOIKE,na Kikaja Kujengwa kutuo rasmi baada ya mradi wa 2005 upanuzi wa barabara ya Mandela na Kampuni ya Specon & Matauro.
Ni jina lililokua na kuenea miaka ya 1970 hadi 1980 lilianzishwa na muasisi wake Mzee Mrema (ambaye hadi sasa yupo).
Mzee Mrema, alianzisha Bar yake akaipa Jina la Riverside miaka ya 1970s -kwa sababu tangu utoto wetu miaka 1980s jina la 'Riverside bar' lilishakuwa kubwa sana.
Mzee mrema ndiyo muasisi wa Congo bar iliyopo Kariakoo. Pia ameshawahi kuwa na Kampuni ya mabasi ya kwenda mkoani ya 'CHAGA DAY' miaka ile ya 1980 ambayo ilikufa miaka ya 1990.
Mzee Mrema kuanzia miaka hiyo ya 1970 hadi sasa Riverside Bar ipo na inaendelea na shughuli zake za kuuza Kinywaji na vyakula hasa nyama choma.
Upekee wa nyama choma ya Mbuzi pamoja na uwepo wa Mbege miaka ya 70,80,90 na hata 2000 ulifanya Jina la Riverside Bar kuwa kubwa sana.
Watu kutoka sehemu mbalimbali ndani ya Jiji la Dar es Salaam walifika kupata nyama choma na mbege wengi wao wakiwa ni wachaga.
Riverside ilizidi kuwa maarufu baada ya kuongezwa mahitaji ya duka la jumla la bia na soda, miaka ya 1980 hadi miaka 1990. Biashara ambayo ilikufa baada ya Majambazi kuvamia mara kwa mara duka la mauzo la Bia.
Siku hizi pana nyongeza ya ukumbi wa shughuli mbalimbali unaoitwa "Riverside hall".Hiyo ndiyo historia ya Jina la RIVERSIDE.
Mwandishi wa makala haya, Boniface Jacob ni mwanasiasa na Meya Mstaafu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.