DODOMA-Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IJP Camillius Wambura amemuhamisha kituo cha kazi Naibu Kamishna wa Polisi, DCP Stella Mutabihirwa kwenda makao makuu ya upelelezi wa makosa ya jinai kuwa mkuu wa kitengo cha makosa dhidi ya binadamu.
Nafasi yake kulingana na taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,SACP David Misime imechukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,SACP Amon Kakwale ambaye alikuwa mkuu wa kikosi cha kuzuia dawa za kulevya.
Pia,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi,SACP Martin Otieno amehamishwa kwenda makao makuu ya Polisi Dodoma kuwa mkuu wa uchambuzi wa makosa ya uhalifu.
Nafasi yake aliyokuwa akiitumikia awali imechukuliwa na SACP Agustini Senga ambaye alikuwa Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar.
Aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Pwani,SACP Issa Suleiman amehamishwa kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara akichukua nafasi ya SACP Nicodemus Katembo ambaye amehamishwa kwenda kuwa Afisa Mnadhimu Kamisheni ya Polisi Jamii makao makuu ya Polisi Dodoma.