DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, kidini na kikabila washiriki kikamilifu kutoa maoni ili kuhakikisha Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo inakuwa jumuishi na shirikishi.
Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata/Shehia, Mitaa/Vijiji na vitongoji wahamasishe na kuwaelimisha wananchi wanaoishi katika maeneo yao ili washiriki kikamilifu katika kutoa maoni ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa, Februari 16, 2024 wakati akiahirisha Mkutano wa 14 wa Bunge la 12 Bungeni, Dodoma. Amesema ajenda ya Maendeleo ya Taifa imefafanuliwa na inaongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kufikia ukomo mwezi Juni, 2026.
Waziri Mkuu amesema kufuatia hali hiyo, Serikali imeanzisha mchakato wa kuandaa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ambayo inatarajiwa kutoa mwongozo wa mwelekeo wa maendeleo wa nchi kwa kipindi cha miaka zaidi ya 25 ijayo, hivyo wananchi hawana budi kujitokeza na kutoa maoni yao.
“Vilevile, vyombo vya habari vitenge muda na kuweka kipaumbele katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika zoezi la kutoa maoni. Andaeni vipindi na makala maalum ili kila mwananchi aweze kupata taarifa. Redio za jamii nazo zihusike kikamilifu kuelimisha umma.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa sekta binafsi asasi za kiraia, makundi maalum kama vile vijana, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na mashirikisho mengine yashirikiane na Tume ya Mipango katika uratibu wa ukusanyaji wa maoni ya wanachama na wadau wao. ”Hii itasaidia kuhakikisha kuwa maoni ya makundi husika yanapokelewa na kujumuishwa katika maandalizi ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo.”
Waziri Mkuu amesema kazi zinazofuata katika maandalizi ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kupitia kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wananchi kushiriki katika maandalizi ya Dira mpya na kukamilisha na kusambaza taarifa ya ukusanyaji maoni.
”Uchambuzi wa taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025 kwa ajili ya maandalizi ya maandiko mahsusi ya kisera kwa ajili ya kuzingatiwa katika Dira mpya pamoja na kuainisha, kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali ambazo zitatoa taarifa katika uandishi wa Dira mpya na uchambuzi na majadiliano ya kina ya kitaalamu na wabobezi kwenye maeneo yatakayoongoza uandishi wa Dira."
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameielekeza Ofisi ya Rais - TAMISEMI ishirikiane na wadau mbalimbali katika maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wasimamizi wa maboresho ya daftari la Mpigakura wahamasishe umma na kutoa elimu ya Mpigakura kwa makundi yote katika jamii.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la maelekezo hayo ni kuwafikia wananchi wote na kuwawezesha kuelewa sheria, kanuni, taratibu za mchakato mzima wa uchaguzi, wajibu wao na umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi.
Waziri Mkuu amesema kwa kuwa suala la elimu ni muhimu katika kuongeza idadi ya wananchi watakaojiandikisha katika Daftari la Mpigakura na hatimaye kuwa na sifa ya kupiga kura wakati wa uchaguzi, nitumie fursa hii kutoa rai kwa Watanzania wote kushiriki katika hatua hii muhimu. Watanzania wenzangu jitokezeni kwa wingi katika vituo vitakavyowekwa, jiandikisheni ili msipoteze haki yenu ya kupiga kura.