DAR ES SALAAM-JKT Queens imepokwa alama tano na kutozwa faini ya shilingi milioni 3.
Uamuzi huo umefikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) baada ya kugomea mchezo dhidi ya Simba Queens mnamo Januari 9, 2024.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) ulipaswa kuchezwa katika Uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam, badala yake JKT walikaidi na kutaka mchezo upigwe katika Uwanja wao wa Major General Isamuyo ulioko Mbweni jijini humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya WPL chini ya TFF, pia imeizawaidia Simba Queens alama 3 na mabao 3 kwa mujibu kanuni ya 18:45 toleo la 2023.
“Pia Kamati imemfungia Katibu Mkuu wa JKT Queens, Duncan Maliyabwana kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi kumi na miwili (12) kwa kuzingatia Kanuni ya 32:1.5 ya Ligi Kuu ya Wanawake Toleo la 2023.
“Kamati imejiridhisha pasipo shaka kuwa Klabu ya JKT Queens ilipata taarifa za mchezo husika kuchezwa Azam Complex, Chamazi kabla ya siku ya mchezo na siku ya mchezo Januari 8, 2024 katika kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM), Mwenyekiti wa
Kikao alikumbusha juu ya muda na uwanja utakaoutumika kwa mchezo huo,” imebainisha sehemu ya taarifa hiyo.
Vile vile, Kamati hiyo pia imejiridhisha kuwa klabu ya Alliance Girls ilifanya udanganyifu na kumtumia mchezaji Nelly Kache katika mchezo namba 3 dhidi ya Geita Queens huku ikijua fika hana uhalali wa kucheza.
“Kamati imekubaliana kuwa Alliance Girls ilifanya makosa na hivyo imepoteza mchezo huo, na Geita Queens imepewa ushindi wa alama 3 na mabao 3 kwa mujibu wa Kanuni ya 48:23 ya Ligi Kuu ya Wanawake Toleo la 2023. Pia Alliance Girls imepigwa faini ya sh. laki tano,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa upande mwingine, Meneja wa timu ya Alliance Girls, Thereza Chacha ametozwa faini ya sh.500,000 kwa kutoa taarifa ama nyaraka zisizo sahihi juu ya mchezaji Nelly Kache (leseni) ili kucheza katika mchezo huo.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:13 Ligi Kuu ya Wanawake kuhusu Udhibiti wa Viongozi.
Mchezaji Nelly Kache ametozwa faini ya sh. laki tano (500,000/-) kwa mujibu wa Kanuni ya 42:11 kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.