DAR ES SALAAM-Joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika eneo la Magharibi mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Afrika Mashariki) ikilinganishwa na upande wa Mashariki mwa Bahari ya Hindi.
Hayo yamebainishwa leo Februari 22, 2024 jijini Dar es Salaam na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TM) kupitia taarifa ya utabiri wa Masika 2024.
Vilevile, kwa mujibu wa TMA joto la bahari la chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la Kusini mwa Kisiwa cha Madagaska.
"Hali hii kwa pamoja inatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua nchini kwa kuimarisha kasi na nguvu ya msukumo wa unyevu nyevu kutoka baharini kuelekea katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki."
Kwa mujibu wa TMA,katika eneo la Mashariki mwa Bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola), joto la bahari la chini kidogo ya wastani linatarajiwa.
"Hali hii inatarajiwa kuimarisha msukumo wa unyevu nyevu kutoka misitu ya Kongo kuelekea nchini hususani katika maeneo yanayozunguka ziwa Viktoria, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.
"Hata hivyo, hali ya El-Niño inayoendelea katika Bahari ya Pasifiki inatarajiwa kupungua nguvu hususan tunapoelekea mwishoni mwa msimu wa mvua wa MAM, 2024,"imebainisha taarifa hiyo ya TMA.