NA FRESHA KINASA
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) mkoani Mara imetakiwa kusimamia tatizo la nauli kupandishwa bila utaratibu linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa magari yanayofanya safari zake kutoka Manispaa ya Musoma kwenda Busekera wilayani humo pamoja na kuonesha nyimbo zisizokuwa na maudhui yenye maadili katika magari yao.
Hayo yamesemwa Februari 16,2024 na baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma katika kikao Cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo uliopo Kata ya Suguti.
Katika kikao hicho madiwani hao wamesema, tatizo la abiria kutozwa nauli ambazo hazina uhalisia ni kubwa sana lakini hakuna hatua zozote zinachukuliwa na LATRA katika kudhibiti ongezeko hilo. Huku baadhi ya magari yakionesha video zenye nyimbo zisizokuwa na maudhui na staha kwa tamaduni za kitanzania bila kuchukuliwa hatua.
"Mimi toka Musoma Mjini- kuja Kwikonero nimelipa Shilingi 4000, lakini kumbe nauli niliyotozwa sio halali bali ni kubwa ikilinganishwa na LATRA ambavyo wamepanga nauli zao. Katika hili hakuna usimamizi kabisa Wananchi wetu wanalia sana," Gerrard Kasonyi Diwani Ifulifu.
Munubi Mussa ni Diwani wa Kata ya Bukumi amesema baadhi ya magari yamekuwa yakionesha video za nyimbo ambazo hazina maadili. Jambo ambalo linachangia mmomonyoko wa maadili na hivyo kuna haja ya kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Mwenyeki wa Halmashauri wa Halmashauri hiyo Charles Magoma amesema kuwa Wananchi wanateseka sana na kitendo Cha kuzidishiwa nauli hali inayopelekea malalamiko mengi yasiyokuwa na ufumbuzi licha ya LATRA kuwa na majukumu ya kudhibiti Usafiri Ardhini.
Kwa upande wake Daud Sagara Afisa Leseni kutoka LATRA Mkoa wa Mara amesema kuwa tatizo la kuzidisha nauli lipo lakini Mamlaka inaendelea kudhibiti tatizo hilo na pia ameomba Wananchi wanaozidishiwa nauli wawasilishe tiketi zao LATRA ili kusudi itawaita wenye magari kuweza kurudisha fedha iliyozidishwa sambamba na kuchukua hatua Kali dhidi yao.
Amesema, mamlaka hiyo katika kuonesha kwamba inawajibika imefanya kaguzi kwa Mkoa wa Mara kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2023 kwa vyombo mbalimbali vya usafiri na kuchukua hatua kwa vyombo vilivyokiuka.
Amebainisha nauli ya barabara ya lami ni Shilingi 48.47, na vumbi ni Shilingi 53.32 kwa abiria kwa kilometa. Basi daraja la kawaida, na Shilingi 67.84 kwa abiria kwa kilometa basi daraja la Kati.
"Tumefanya kaguzi 53 kwa Mkoa wa Mara, ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma jumla ya kaguzi ni 13. Idadi ya vyombo vya usafiri vilivyochukuliwa hatua kwa Mkoa ni 703, na katika Wilaya ya Musoma idadi ya vyombo vilivyochukuliwa hatua ni 54 kwa hiyo tushirikiane kuwafichua wanaozidisha nauli Mamlaka itachukua hatua,"amesema Daud na kuongeza.
"Lakini pia Idadi ya Makosa yaliyobainika katika kipindi cha Oktoba hadi Dicemba 2023 kwa kaguzi zilizofanyika Wilaya ya Musoma. Mabasi kuzidisha abiria idadi ya magari yaliyokamatwa ni 8, na asilimia inayochangia katika Makosa yote ni asilimia 14.8, mabasi kuzidisha idadi ya abiria 9, na asilimia inayochangia katika Makosa 16.7, mabasi kutokutoa tiketi kwa abiria ni magari 3, na asilimia iliyochangia katika makosa yote ni 5.6,"
Aidha,ameongeza kuwa upande wa magari au mizigo kutokuwa na leseni ya usafirishaji ni 25, na asilimia inayochangia katika Makosa yote ni 46.3, dereva na kondakta kutokuvaa sare ni magari 9, na asilimia inayochangia katika Makosa ni 16.7.
Ameongeza kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba hadi Dicemba 2023 Ofisi ya LATRA Mkoa wa Mara ilitoa jumla ya leseni za usafirishaji 1,170 ikiwa sawa na ongezeko la asilimia 68 ukilinganisha na idadi ya leseni 698 zilizotolewa kwa kipindi cha miezi kama hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023