NA GODFREY NNKO
RAIS wa Chama cha Madaktari nchini (MAT), Dkt. Deusdedit J.Ndilanha amesema chama hicho kipo tayari kuanza kwa utekelezaji wa kitita kipya cha mafao na kitaamsha ari kwa wauguzi kuwahudumia zaidi wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) nchini.
"Kwanza tunaunga mkono mapendekezo ya kamati, na sisi Chama cha Madaktari tunaamini kamati ilikuwa ni huru, imeenda kwenye uhalisia na kwa msingi huo yale yote ambayo wameyapendekeza sisi tunayaunga mkono.
"Nitoe pongezi, kwa kweli kwa maboresho ambayo wameyafanya na ni baada ya mazungumzo ambayo tuliyafanya, ninafikiri wananchi watakuwa wanakumbuka kwamba mwaka jana mwishoni, mfuko ulitoa kitita na ukasema kwamba unarejea, una mpango wa kufanya maboresho na yataanza kutumika mwaka huu (2024).
"Na sisi kama Chama cha Madaktari tulikuwa na maeneo ambayo tulifikiri kwamba yalitakiwa yaboreshwe kidogo, kwa hiyo tulipata hiyo nafasi baada ya Mheshimiwa Waziri kuunda kamati huru, ambayo sisi kama Chama cha Madaktari tulipata nafasi tukaenda tukapeleka hoja zetu na tarehe 19, kamati iliwasilisha mapendekezo kwa Mheshimiwa Waziri.
"Na kwa kweli kwa asilimia kubwa yale ambayo madakatari walikuwa wanayasemea, wanayapigia kelele kamati iliyachukua na sasa yanaenda kufanyiwa kazi.
"Kwa hiyo, kwa kweli sisi kama chama tunapongeza na kwa bahati nzuri kamati ilisema kwamba, milango iko wazi kwa wizara na mfuko kwamba kama kuna maeneo tunafikiri bado tunaweza tukawa tuna maoni, maboresho basi tuyapeleke official na sisi kama Chama cha Madaktari tuko tayari, tutafanya hivyo.
"Ni katika kukiboresha hiki kitita ambacho kitaanza kutumika soon na tunaunga mkono ni kwa sababu kinaenda kujibu sehemu ya malalamiko ya madaktari hasa madaktari ambao wanafanya kazi kwenye hospitali za mikoa, kushuka chini.
"Wale ambao,walikuwa na kiwango cha elimu ambacho kinalingana na madaktari ambao wapo kwenye hospitali za kanda na hospitali za Taifa.
"Tulikuwa tunaona madaktari wengi baada ya kusoma, wamebobea walikuwa wanajaribu kuhama kutoka kwenye hospitali za mikoa za wilaya kewenda kwenye hospitali za juu ni kwa sababu ya incentive kidogo ambapo wenzetu wa hospitali za kanda na taifa walikuwa wanapata.
"Sasa,kwa maboresho haya maana yake madakari hawa tuna-intend kwamba watabaki huko, na hii itaendana na maboresho ambayo kwa kweli yamefanyika kwenye miundombinu ya kutolea huduma ambayo Serikali ya Awamu ya Sita na Serikali zote zilizopita zimeyafanya.
"Kwa hiyo, madaktari hawa watapata hamasa, sasa kubaki huko kuendelea kuwahudumia wananchi. Mfuko wetu ni muhimu sana kwa nchi,huwezi kuzungumzia maboresho makubwa kwenye sekta ya afya bila kutaja NHIF.
"Na ni katika msingi huo, sisi wote sio tu Chama cha Madaktari na wananchi kwa ujumla tuna wajibu wa kuulinda huu mfuko (NHIF) usife kwa namna yoyote ile, kwa hiyo kama kutakuwa na changamoto zozote za hapa pale njia nzuri ni majadiliano.
"Na kufikia mwafaka ili wote twende kwa pamoja, ni mfuko wa kuigwa kwa Afrika, na tunafahamu kuna nchi ambazo zilijaribu mfuko ukafeli, lakini sisi hatutaki kuingia kwenye historia kwamba tulikuwa na mfuko ukafa.
"Kwa hiyo tuna wajibu wa kuulinda mfuko wetu kwa sababu ni mkombozi sana kwa wananchi wengi na tunafahamu kuna maeneo ambayo bado yanaweza kuwa na changamoto za hapa na pale na ni niliyasema haya mbele ya Mheshimiwa Waziri kuwa unapoingia kwenye makubaliano kuna kutoa na kuchukua.
"Kwa hiyo kuna mambo ambayo Serikali imekubali, kuna mambo ambayo na sisi wadau tulikubali, halafu yapo ambayo yana changamoto, basi milango bado iko wazi mara zote tunaweza kukubaliana tukaboresha zaidi ili mwananchi anufaike.
"Kwa hiyo sisi tunaunga mkono, na kwa kweli madaktari wako tayari na wamefurahi wako tayari kuwahudumia wanachama wa NHIF,"amefafanua kwa kina Rais wa Chama cha Madaktari nchini (MAT), Dkt. Deusdedit J.Ndilanha.
NHIF
Dkt.Ndilanha ameyabanisha hayo ikiwa ni saa chache zimepita baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Bernad Konga kubainisha kuwa, Machi Mosi, mwaka huu utekelezaji wa kitita hicho unaanza rasmi.
Ameyabainisha hayo Februari 28,2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Kitita cha Mafao ni orodha ya huduma za matibabu ambazo zinatolewa kwa wanufaika wa NHIF na bei zake ambazo hutumika wakati wa malipo kwa madai ya watoa huduma za matibabu.
“Maboresho ya mwisho ya Kitita cha Mafao cha NHIF kinachotumika sasa yalifanyika Juni, 2016 takribani miaka nane iliyopita na hivyo kuwepo kwa umuhimu wa kufanya marejeo yake kutokana na sababu mbalimbali."
Konga amesema,NHIF ilianzishwa kwa Sheria Sura 395 kwa lengo la kusimamia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa makundi yanayosajiliwa na moja ya jukumu lake ni kufanya mapitio ya Kitita cha Mafao.
Ni kwa lengo la kuhakikisha kinaendana na mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika katika Sekta ya Afya nchini na kwa mujibu wa tathimini ya uhai na uendelevu wa mfuko kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 39A cha sheria hiyo.
Amesema, maboresho ya kitita yanalenga kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama ikiwa ni pamoja na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo awali.
Pia, kufanya maboresho ya huduma na gharama zake kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na hali halisi ya bei katika soko.
"Ikiwemo kuwianisha Kitita cha Mafao na miongozo ya tiba iliyoboreshwa ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa mfuko.
"Na kuwianisha Kitita cha Mafao na miongozo ya tiba iliyoboreshwa ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa mfuko."
Nyingine ni kujumuisha maoni na mapendekezo mbalimbali ya wadau na kutekeleza ushauri wa Taarifa ya Mapendekezo ya Tathmini ya Uhai na Uendelevu wa Mfuko kwa kipindi kinachoishia Juni 30, 2021 na kuimarisha udhibiti katika mianya ya udanganyifu.
Amesema,mfuko ulianza zoezi la kufanya marejeo ya kitita kuanzia mwaka 2018.Hata hivyo, Konga amefafanua kuwa, utekelezaji wa kitita kipya haukufanyika kutokana na uhitaji wa kuhusisha wadau zaidi ili kuwa na uelewa na maoni zaidi kuboresha kitita hicho.
"Maboresho ya Kitita cha Mafao yamehusisha kufanya tathmini ya uhai na uendelevu wa mfuko na kutekeleza mapendekezo yake ambapo tathmini ya mwisho ilifanyika Juni, 2021.
"Kifungu Na 15.2 cha mkataba baina ya mfuko na watoa huduma kinautaka mfuko kutoa notisi ya miezi mitatu ya kusudio la kufanya maboresho katika kitita chake kabla ya kuanza kutumika."
Katika kutekeleza takwa hilo la mkataba,Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHIF amesema Agosti 1, 2022 mfuko kupitia barua yenye Kumb. Na. EA.35/269/01-A/32 ulitoa notisi ya miezi mitatu ya kusudio la kufanya maboresho ya Kitita cha Mafao.
Amesema,tangu tarehe ya kutolewa kwa notisi hiyo, mfuko uliendelea kushirikisha wadau, kukusanya na kupokea maoni, ushauri na mapendekezo kutoka kwa wadau wake kwa lengo la kuboresha kitita chake cha mafao.
Konga amefafanua, kwa nyakati tofauti mfuko ulifanikiwa kukutana na watoa huduma za matibabu wa umma na binafsi na madhehebu ya dini vikiwemo vyama mbalimbali vya taaluma za afya.
Vile vile kushirikisha taasisi chini ya Wizara ya Afya ikiwemo Bohari ya Madawa (MSD) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa lengo la kuwianisha Kitita cha Mafao na kinadi cha MSD pamoja na orodha ya dawa zilizosajiliwa na TMDA.
Pia,walifanya tafiti ya gharama halisi za matibabu katika soko na kujumuisha maelezo ya Serikali yenye leno la kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Maeneo yaliyofanyiwa mapitio na maboresho katika Kitita cha Mafao ni pamoja na ada ya usajili na kupata ushauri wa dakatari.
Mengine ni huduma za dawa, huduma za vipimo, huduma za upasuaji na gaharama za kliniki za kawaida na kibingwa.
Kwa upande wa huduma za usajili na kupata ushauri wa daktari, Konga amesema, lengo ni kuwezesha madaktari kufanya kazi katika ngazi zote kutokana na kuwepo kwa usawa wa ada ya kumuona daktari kwa ngazi zote kwa madaktari wa kada zinazoendana.
"Hii itawezesha wanachama kupata huduma za kibingwa katika ngazi mbalimbali za vituo kwa kuzingatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika Sekta ya Afya nchini."
Kwa upande wa huduma za dawa amesema, jumla ya dawa 736 zimefanyiwa mapitio kwa kuzingatia bei za soko na gharama za uendeshaji na wastani wa faida.
Amesema,hii itaondoa changamoto ya wanachama kukosa baadhi ya huduma za dawa kutokana na changamoto za bei.
Wakati huo huo,Konga amesema zimeongeka dawa zaidi ya 247 ambazo zinatokana na dawa mpya zilizoko katika Mwongozo wa Orodha ya Dawa Muhimu za Taifa (MEMLIT).
Mkurugenzi Mkuu huyo anasema,hii inaongeza wigo wa upatikanaji wa dawa kwa wanachama.
"Kuzingatia mabadiliko katika ngazi za matumizi ya dawa kama zilivyoainishwa katika MEMLIT. Maboresho haya yataongeza upatikanai wa huduma za dawa katika vituo vya ngazi ya msingi mfano dawa za matibabu ya shinikizo la damu na kisukari."
Aidha, kwa upande wa huduma za upasuaji na vipimo amesema, gharama za vipimo 311 na huduma za upasuaji zimefanyiwa mapitio kwa kuzingatia bei za soko katika ununuzi wa vifaa na vitendanishi, gharama za uendeshaji na wastani wa faida.
"Pia hii itaondoa changamoto ya kukosekana kwa huduma za vipimo na upasuaji kutokana na changamoto ya bei.Na kuongeza wigo wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi za upasuaji na vipimo katika hospitali za rufaa ngazi za kanda na Taifa."
Amesema, maboresho haya yataongeza upatikanaji wa huduma za matibabu ya saratani na upasuaji wa mifupa.
Nyingine ni upasuaji wa moyo katika hospitali si za Taifa tu bali hata hospitali za kanda, hivyo kusogeza huduma karibu na maeneo ya wananchi.
"Katika kuimarisha upatikanaji wa huduma, mfuko umeendelea kuimarisha utambuzi wa wanufaika katika vituo vya kutolea huduma kwa kutumia alama za vidole na sura.
"Pia, kuweka jukwaa mahususi litakalowezesha watoa huduma kubadilishana taarifa za mgonjwa miongoni mwa vituo."
Vile vile kuweka utaratibu utakoawezesha wanufaika kuzingatia utaratibu wa rufaa na kuendelea kudhibiti udanganyifu na kuchukua hatua stahiki kwa wadau watakaodhibitika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu.
Ameongeza kuwa, mfuko unaendelea kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa wadau wake hasa wanachama na watoa huduma katika kufanikisha utekelezaji wa kitita hiki kipya.
“Na tunaamini maboresho haya yatakwenda kuwa chachu ya kufikia azma ya Serikali ya Afya Bora kwa Wote.
“Aidha, mfuko unathamini kazi kubwa inayofanywa na mtoa huduma mmoja mmoja kwa kuzingatia mkataba baina yao na mfuko.
“Hivyo, mawasiliano yataendelea kuimarishwa ikiwemo huduma kwa wateja ili kuwawezesha kufikia malengo yao.
“Endapo kutakuwa na suala lolote baina ya mtoa huduma na mfuko, basi kwa kuzingatia mahusiano haya ufumbuzi utapatikana.”
Mbali na hayo, Konga amesema kuwa, mfuko unaendelea kupkea maoni kutoka kwa wadau. “Na tutaendelea kuwajulisha pindi maboresho yoyote yanapotokea ili kuwa na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Mfuko unatoa rai kwa mwanachama na mtoa huduma yeyote atakayepata changamoto wakati wa kupata huduma kuwasiliana na mfuko kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa kupiga simu namba 199 bure au kwa kuwasilana na ofisi ya NHIF iliyo karibu.”
Mkurugenzi Mkuu huyo amewataka wananchi kufahamu kuwa, maboresho yaliyofanyika ni baina ya NHIF na watoa huduma wanaoshirikiana nao.
Aidha, gharama za maboresho hayo hazimgusi mwanachama bali ni kati ya NHIF na watoa huduma ili kuboresha zaidi huduma karibu na wananchi nchini.
Tags
Afya
Chama cha Madaktari nchini (MAT)
Habari
Kitita cha Mafao NHIF
Kitita Kipya NHIF
NHIF
NHIF Tanzania