Makamu wa Rais atoa maelekezo kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, OR-TAMISEMI

TANGA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo ni msimamizi wa taasisi na mashirika ya umma nchini na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI msimamizi wa halmashauri, kuona namna taasisi, mashirika na baadhi ya halmashauri zinavyoweza kutumia dirisha la Hatifungani kuharakisha utekelezaji wa miradi.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo wakati wa Uzinduzi wa Uuzaji wa Hatifungani kwaajili ya Fedha za Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Maji, Tanga uliyofanyika katika Ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga.

Amesema Hatifungani iliyozinduaiwa mkoani Tanga inapaswa kuwa chachu na motisha kwa Halmashauri na taasisi nyingine zikiwemo Halmashauri kutumia njia hiyo kupata fedha za miradi ya maendeleo na kutoa nafasi kwa Serikali kujikita kwenye maeneo mengine ya kipaumbele ambako hakuna uwezeshaji wa aina hiyo.

Makamu wa Rais ameitaka Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga, kusimamia vizuri matumizi ya fedha zitakazopatikana kupitia Hatifungani iliyozinduliwa na mapato mengine yatakayokusanywa baada ya kukamilisha mradi huo.

Amesema nidhamu ya fedha na usimamizi thabiti ndiyo utakaowawezesha kurejesha kwa wakati fedha za wawekezaji wa Hatifungani hiyo na Serikali haitavumilia uzembe wa aina yoyote utakaoonekana kukwamisha jitihada hizo.

Aidha, Makamu wa Rais amesema ni vyema kujipanga mapema ikiwezekana kwa kufungua mfuko maalum wa kukusanya kidogokidogo fedha za marejesho ili kuondoa changamoto wakati wa malipo kwa kuwa urejeshaji wa fedha hizo ni kwa mkupuo baada ya kuiva kwa Hatifungani.

Pia ameiagiza Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Wizara ya Maji kuweka utaratitu na mfumo wa tahadhari (early warning system) ili kufuatilia na kubaini mapema vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika utaratibu huo.

Makamu wa Rais ametoa pongezi kwa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga kwa kuwa na uthubutu na kufungua njia mbadala ya kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.

Amesema,Hatifungani hiyo itasaidia kuongeza kiasi cha maji yanayozalishwa kutoka lita milioni 42 hadi milioni 60, kuongeza upatikanaji wa maji katika jiji la Tanga kutoka asilimia 96 hadi takriban asilimia 100 ifikapo Juni 2025.

Kuongeza mtandao wa maji katika miji ya Muheza na Pangani kutoka asilimia 70 hadi zaidi ya asilimia 95 ifikapo Juni 2025. Ameongeza kwamba mradi huo utanufaisha zaidi ya wananchi 458,365 waliopo katika jiji la Tanga na miji ya Pangani na Muheza pamoja na kupata maji ya kutosha kwa ajili ya wananchi wapatao 74,124 wa wilaya ya Mkinga.

Kwa Upande wake Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso amesema Wizara itafanya kazi kwa uadilifu na ubunifu mkubwa kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana kwa kutumia njia hiyo mpya ya hatifungani kwa maendeleo ya sekta ya maji nchini.

Waziri Aweso ametoa wito kwa wadau wa sekta ya maji kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maji katika kufanikisha suala hilo la matumizi ya hatifungani katika miradi ya maji.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Chande amesema mkakati huo wa matumizi ya hatifungani umelenga kuwezesha serikali kugharamia miradi mingi zaidi hususani yenye uwezo wa kuzalisha mapato.

Amesema soko la mitaji na dhamana lipo tayari kwaajili ya kupokea hatifungani zingine kutoka taasisi za serikali kwaajili ya maendeleo ya nchi. Wizara ya Fedha itahakikisha mkakati wa kugharamia miradi ya maendeleo kupitia njia mbadala unatekelezwa kama ilivyopangwa.

Jumla ya shilingi bilioni 53.12 zinatarajiwa kuwekezwa katika Hatifungani ya Kijani ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu ya maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news