Mheshimiwa Mpina afafanua kuhusu hoja huduma za kuongeza makalio

UFAFANUZI WA MBUNGE WA JIMBO LA KISESA MHE. LUHAGA JOELSON MPINA, KUHUSU HOJA YA HOSPITALI ZA SERIKALI KUANZA KUTOA HUDUMA ZA KUONGEZA MAKALIO NA MATITI ALIPOZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 14 FEBRUARI 2024 VIWANJA VYA BUNGE DODOMA

Ndugu Waandishi wa Habari, asanteni kwa nafasi hii mliyonipa ili niweze kutolea ufafanuzi baadhi ya mambo yaliyotokea hapa bungeni, ni kweli wakati nachangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika hoja ya kuongeza makalio na matiti sikuweza kuwasilisha maelezo yangu yote kutokana na changamoto ya muda na hivyo kwa maswali mliyoniuliza na nafasi mliyonipa naomba kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-

Ndugu Waandishi wa Habari, mtakumbuka kuwa Umma wa watanzania ulitangaziwa na Mkuu wa Idara ya Upasuaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili- Mloganzila, Dkt. Erick Muhumba kupitia tangazo lake la tarehe 10 Oktoba 2023 kuwa kuanzia tarehe 27-28 Oktoba 2023 huduma za kuongeza makalio na matiti zitaanza kutolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili- Mloganzila na ikaelezwa zaidi kuwa huduma hiyo itatolewa kwa ushirikiano wa madaktari wa ndani na wa kutoka India na Afrika Kusini.

Ndugu Waandishi wa Habari, Nnmefuatilia hotuba mbalimbali za viongozi wakuu wa nchi, taarifa na Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya na taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika mwaka wa fedha 2023/2024 na miaka mingine ya nyuma, huduma hii ya kuongeza makalio na matiti haijaelezwa mahali popote. Pia nimefuatilia kujua kama huduma hii inaruhusiwa au la.

Ili huduma yoyote ya afya itolewe nchini mambo yafuatayo huzingatiwa kama ifuatavyo:-

(i) Huduma ya afya inayotolewa ni lazima iwe imejumuishwa katika sera, nimejiridhisha kuwa suala la kuongeza makalio na matiti halimo kwenye Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ambayo ndiyo sera inayotoa mwongozo wa utoaji huduma zote za afya nchini, huduma za uongezaji wa makalio na matiti ni huduma za anasa na hufanyika kwa watu ambao hawana changamoto yoyote ya kiafya ni upasuaji wa kimapambo (Cosmetic Surgery) ambayo hufanyika kwa lengo la kupendeza au kubadili mwonekano (shepu).

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Ali Mwalimu katika majibu yake alisema huduma ya kuongeza makalio inatolewa hapa nchini kwa kuzingatia sera za Shirika la Afya Duniani (WHO), huku akijua kuwa hakuna sera ya WHO inayotumika hapa nchini bila kuridhiwa na kutungiwa sera na sheria za ndani. Hivyo Waziri alipaswa kutaja aya ya Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inayoruhusu suala hilo badala ya kujificha kwenye sera za WHO.

(ii) Huduma inayotolewa ni lazima iwe na mwongozo, Kanuni, na Sheria (Legal Framework) ili kubainisha haki na mambo yanaruhusiwa na yasiyoruhusiwa, nimepitia na kujiridhisha kuwa suala kuongeza makalio na matiti halina mwongozo wala kanuni za kusimamia utekelezaji wake ni hatari kwa suala kama hili kuanza kutolewa bila mwongozo wala kanuni zinazobainisha haki za wateja na Daktari anayetoa huduma hiyo analindwa vipi kisheria dhidi ya madhara yatakayotokea.

(iii) Huduma inayotolewa ni lazima uwe umefanyika utafiti na tathmini ya kina kujiridhisha juu ya ufanisi na madhara yatakayotokea, nimejiridhisha hakuna utafiti wala tathmini iliyofanywa hapa nchini kuthibitisha usalama wa afya na madhara yanayoweza kutokea kutokana na upasuaji wa kuongeza makalio na matiti.

Aidha Waziri na Naibu Waziri wa Afya walipaswa kuwa wameliarifu Bunge kuhusu tahadhari ya madhara yanayoweza kutokea kutokana na huduma hii.

Baadhi ya nchi zinazotoa huduma za kuongeza makalio imekuwa ikiripotiwa kuwepo kwa madhara kwa watu waliopatiwa huduma hizo kama kupata magonjwa ya saratani, kuathiri afya ya uzazi na kusababisha ugumba, kuhudhuria kliniki mara kwa mara, kuathiri viungo vingine kwenye mwili na kusababisha magonjwa ya moyo, muonekano au shepu kuwa sio wa kudumu, makalio kubomoka wakati wowote na ngozi ya mwili kubadilika rangi. Hivyo kama taifa ni muhimu kujiridhisha na athari hizi kabla ya kuanza kutoa huduma hii hapa nchini.

(iv) Huduma itakayotolewa ni lazima sababu za kutolewa zibainishwe bayana na ziwe kwa maslahi ya umma, nimefuatilia na kupitia maelezo ya Waziri hakuna sababu za msingi za kuanzishwa huduma hii. Maelezo kwamba Wizara imezingatia kuwepo kwa uhitaji, chanzo cha mapato na usumbufu wa wananchi wanaolazimika kusafiri hadi Uturuki, China na India kusaka huduma hiyo hayana mantiki yoyote kwani cha kwanza katika utoaji wa huduma ya afya ni kuwahakikishia wananchi usalama wa afya zao.


Hatuwezi kuweka rehani maisha ya watanzania kwa sababu ya mapato na hatuwezi kuruhusu kila hitaji la huduma ya kiafya hata yenye madhara ifanyike nchini.

(v) Huduma inayotolewa ni lazima ieleze bayana inalenga kundi gani kwenye jamii, Tangazo la kuongeza makalio limewaalika watu wote kwenda Mloganzila kupatiwa huduma hiyo, Hii ina maana kuwa huduma hii itatolewa kwa watu wa rika zote wakiwemo watoto na wanafunzi.


Jambo hili linaweza kuwatoa vijana wetu kwenye mstari wa kielimu kama taifa ni vyema kutumia nguvu zetu zote kuwaandaa vijana kukabiliana na maisha na ujenzi wa taifa lao kwa kuwapatia elimu bora, ujuzi na maarifa, badala ya kuwabebesha mzigo wa makalio na matiti.

Hapa walengwa wa huduma hii ni akina nani hasa? Jinsia gani? Na rika gani? Kwanini hatuelezwi linazungumzwa kijumla jumla kuna nini kinachofichwa? kwa hivi sasa gharama za upasuaji wa kuongeza makalio na matiti ni kubwa hivyo watu wengi wanaweza kushindwa kumudu gharama hizo, Je akitokea mfadhili wa kugharamia huduma hii na kuanza kutolewa bure kwa wananchi wote nchini kwa watu wa rika zote, tutakuwa tunatengeneza taifa la aina gani?

(vi) Huduma inayotolewa isitengeneze matabaka kwenye jamii ya wenye nacho na wasio kuwa nacho, Kwa kuwa gharama za kuongeza makalio zilizotangazwa na Serikali ni Tsh. Milioni 12 hadi Tsh. Milioni 18 ni kubwa na hivyo ni watu wachache watakaokuwa na uwezo wa kumudu gharama hizo na hivyo kuchochea matabaka baina ya walionacho na wasio nacho ndani ya nchi.

(vii) Malipo yanayotozwa ni lazima yawe kwa mujibu wa sheria, gharama zilizotangazwa za kuongeza makalio na matiti ya Tsh. Milioni 12 hadi Tsh. Milioni 18 hayapo kisheria kwa kuwa hakuna GN yoyote iliyoidhinisha tozo hizi. Pia hakuna uwazi katika mgawanyo wa mapato kwa madaktari wa kutoka India na Afrika Kusini.

(viii) Huduma inayotolewa lazima izingatie mila, desturi na tamaduni, suala la kuongeza makalio na matiti sio mila na desturi za kitanzania na lina mapokeo hasi kwenye jamii ambapo pia nimejiridhisha kupitia maoni mbalimbali ya wananchi kwenye mitandao ya Kijamii.

Ndugu Waandishi wa Habari, kwa uchambuzi niliofanya kwenye vipengele nane (8) hapo juu ni dhahiri kwamba suala la kuongeza makalio na matiti limeanzishwa kiholela na bila kuzingatia sheria za nchi na kuna mambo mengi yasiyo ya kawaida yaliyojificha.

Ndugu Waandishi wa Habari, Kama suala la uongezaji wa makalio na matiti halijaruhusiwa katika Sera ya Afya na hakuna sheria, kanuni wala miongozo inayosimamia suala hili, Huduma hii ya kuongeza makalio na matiti hapa nchini inafanyika kwa idhini ya nani?

Ndugu Waandishi wa Habari, Nashauri tena huduma ya kuongeza makalio na matiti ipigwe marufuku nchini hadi hapo tutakapokuwa na muafaka wa kitaifa na pale tutakapokuwa tumejiridhisha kuhusu madhara yanayoweza kutokea kwa watu wanaopewa huduma hiyo na athari ambazo jamii inaweza kupata. Kama Viongozi na wawakilishi wa wananchi tunalo jukumu la kuhakikisha wananchi wetu wana afya bora na sio kuwapelekea mzigo wa maradhi.

Ndugu Waandishi wa Habari, Pia niliomba kuongeza azimio kwenye Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwamba Bunge liazimie kwamba huduma za kuongeza makalio na matiti zipigwe marufuku nchini na ufanyike uchunguzi wa kina kubaini kilicho nyuma ya pazia na kujua tumefikaje hapo na kwamba wote waliohusika kuruhusu Hospitali za umma kutoa huduma ya kuongeza makalio na matiti wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa Sheria za nchi.


MAELEZO YALIYOTOLEWA NA WAZIRI, NAIBU WAZIRI NA MWENYEKITI WA KAMATI KUHUSU HOJA YA KUONGEZA MAKALIO NA MATITI BUNGENI

Ndugu Waandishi wa Habari, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Ali Mwalimu wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI tarehe 12 Februari 2024 hapa bungeni alisema eti tunaongozwa na tafsiri au na miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), afya ni ukamilifu wa binadamu kimwili, kiakili na Kijamii na kutokuwepo kwa magonjwa lakini sera ya hii pia inatutaka tutoe huduma kwa kuzingatia mahitaji ya kila mtu na kwamba mapato makubwa yanayopatikana kwenye biashara ya kuongeza makalio yanatumika kutibia wagonjwa wa msamaha, kina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Alisema Waziri Mhe. Ummy.

Hapa Waziri amejielekeza vibaya kwani Tasfiri ya neno Afya inayotolewa na WHO haiondoi msimamo wa kila nchi wa namna inavyotasfiri ukamilifu wa binadamu kimwili, kiakili na Kijamii na kuwepo matibabu. Tanzania ina msimamo wake wa utoaji wa huduma za afya kupitia Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambapo kupitia sera hiyo inabainisha huduma za afya zinazoruhusiwa kutolewa nchini.

Ndugu Waandishi wa Habari, Waziri wa Afya alipaswa kueleza ni aya gani katika sera ya afya ya mwaka 2007 au Sheria, Kanuni na Mwongozo inayoruhusu kuongeza makalio na matiti au kufanya upasuaji wa kimapambo katika nchi yetu, lakini badala yake Waziri anasingizia sera za WHO ambazo wala hazihusiki.

Msimamo wa Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu aliouonyesha Bungeni kushabikia suala la kuongeza makalio na matiti unaleta tafsiri kuwa chini ya uongozi wake kama Waziri wa Afya huduma yoyote ya kiafya inaweza kutolewa nchini ilimradi kuna watu wanahitaji na kwamba ni chanzo cha mapato ya Serikali bila kujali kama huduma hiyo ina madhara gani kiafya na kwa mustakabali mwema wa taifa letu.

Kwa Muktadha huo, hata kufanya upasuaji wa kubadili jinsia (Transgender), Kufanya upasuaji wa kutoa mimba, kufanya upasuaji wa kubadili sura kwake Waziri Ummy ni sawa kisa kuna wahitaji, chanzo cha mapato na huduma hizo zimeruhusiwa na WHO. Nchi yetu ina miiko siyo kila aina ya huduma za kiafya zinatolewa.

Waziri wa Afya ni mtumishi wa umma anapaswa kutambua kuwa hawezi kuwa na msimamo wake binafsi zaidi ya msimamo wa nchi ambao umefafanuliwa katika Sera, Sheria, Kanuni na miongozo.

Hata hivyo maelezo ya Waziri wa Afya kwamba kuna watanzania wengi wanahitaji huduma ya kuongeza makalio na kwamba wamekuwa wakihangaika kwenda nchi za Uturuki, India na China hayana ukweli wowote kwa sababu hakuna utafiti uliofanywa wala ushahidi wa kitakwimu (Statistical Evidence) kuthibitisha maelezo yake. Pia Waziri Ummy hakuweka wazi ni kiasi gani cha fedha Serikali imekusanya tangu ilipoanza kutoa huduma za kuongeza makalio na matiti Oktoba 2023.

Hivi kweli Waziri wa Afya anasema watanzania wanategemea fedha kutokana na mapato yatokayo na huduma ya kuongeza makalio na matiti kwa ajili ya kugharamia huduma za afya nchini? hii ni kashfa kubwa sana. Ni Kauli ambayo haikutegemewa kutolewa na kiongozi aliyepewa dhamana kubwa ya kulinda afya za watanzania.

Ndugu Waandishi wa Habari, Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dk. Godwin Mollel naye alipoomba kutoa taarifa wakati nikichangia taarifa ya Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI tarehe 12 Februari 2024 hapa Bungeni, taarifa ya Naibu Waziri Dk. Mollel kimantiki ilikuwa sawa na mchango wa Waziri huku akitoa taarifa kwa dharau kubwa eti anamfundisha mchangiaji (Mpina).


Katika taarifa yake Dk. Mollel alijaribu kupotosha kuhusu aina na tofauti kati ya upasuaji wa kurudisha mwonekano wa awali (Plastic Surgery) na upasuaji wa kimapambo (Cosmetic Surgery) mambo ambayo hayakuwa sehemu ya mchango wangu.

Ndugu Waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo akihitimisha hoja yake bungeni alilikataa pendekezo langu la Azimio la kupiga marufuku upasuaji wa kuongeza makalio na matiti nchini na kuchukua hatua kwa walioruhusu suala hili kinyemela, kwa maelezo kuwa suala hilo linaruhusiwa kimataifa ingawa pia hakufafanua kama suala hilo linaruhusiwa ndani ya nchi kupitia Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo ya utoaji wa huduma za afya nchini.


Lakini pia kwa bahati mbaya sana Mwenyekiti wa Kamati hakueleza madhara wanayoweza kupata jamii na watu wanaoongeza makalio na matiti.

Maelezo ya Mwenyekiti kuwa kuongeza makalio na matiti ni moja ya huduma za ubingwa na ubingwa bobezi zinazotolewa nchini, hapo alijielekeza vibaya kwani ubingwa huo una mipaka na siyo kila huduma za ubingwa na ubingwa bobezi zinazotolewa maeneo mengine duniani zinaweza kutolewa nchini mwetu.


Utoaji wa huduma za afya nchini unatolewa chini ya mwongozo wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ambapo suala la kuongeza makalio na matiti halijaruhusiwa.

Hata hivyo maelezo ya Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Nyongo kwamba Kamati itakwenda kulitizama upya suala hili inatia matumaini na ni imani yangu kuwa watafanya kwa dharura ili kuondoa sintofahamu iliyopo.


HITIMISHO

Ndugu Waandishi wa Habari, nimesema suala la kuongeza makalio na matiti haliruhusiwi kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, sera hiyo katika aya ya 5.5 inazungumzia utoaji wa huduma za utengemao ambapo upasuaji wa kimapambo sio sehemu ya sera hiyo.


Lakini pia suala hili halina Sheria, Kanuni wala Miongozo ya kulisimamia nchini. wale wanaosema suala hili linaruhusiwa watoke hadharani na watoe uthibitisho walionao.

Sera za afya za Shirika la Afya Duniani (WHO) hutoa mwongozo wa jumla wa usimamizi wa afya kimataifa ambapo utekelezaji wake hutofautiana nchi na nchi kulingana na mila, desturi na tamaduni za nchi husika. Nchi hulazimika kuandaa Sera, Sheria, Kanuni na miongozo iliyokubaliwa na nchi husika (Domestication). Mfano hata suala la haki za binadamu kila nchi ina namna inavyotafsiri.

Upasuaji unaoendelea wa kuongeza makalio na matiti hapa nchini ni kinyume cha Sera na Sheria za nchi na ni hatari kuruhusu jambo hili kufanyika bila tafiti na tathmini za kina kuhusu athari zinazoweza kuwapata watu wanaopatiwa huduma hizo.


Hakuna sababu za msingi za kuruhusu suala hili na badala yake kama nchi tujikite kutafuta ufumbuzi wa magonjwa yanayowasumbua watanzania ambayo yanawapa mateso makubwa, umasikini na kusababisha vifo. mfano kuna sintofahamu kubwa ya nini chanzo cha ongezeko la magonjwa ya Kansa, tezi dume, magonjwa ya figo, magonjwa ya Moyo na Kisukari hapa nchini.

Aidha katika kuhitimisha maelezo yangu naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza Madaktari, Wauguzi na watalaamu wengine wa Sekta ya Afya kote nchini walioko katika taasisi za umma na binafsi kwa namna wanavyojitoa kupambana na maradhi yanayowakabili watanzania na kuokoa maisha yao.

Pia niipongeze Serikali kwa uwekezaji mkubwa inaoendelea kufanya katika miundombinu, vifaa na wataalamu hali inayowezesha kuendelea kuimarika kwa utoaji wa huduma za afya nchini.

Ndugu Waandishi wa Habari, Mwisho ila sio kwa umuhimu naomba kipekee nimpongeze sana Profesa David Homeli Mwakyusa (Daktari Bingwa wa ubingwa bobezi) aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wakati Sera ya Afya inatungwa mwaka 2007 yeye na wenzake walituandalia sera nzuri sana ambayo imesaidia kwa kiwango kikubwa kutoa mwongozo wa utoaji wa huduma bora za afya nchini.

Mungu aendelee kumpa maisha marefu mzee wetu Prof. Mwakyusa, Taifa litaendelea kuenzi mchango wake katika kuinua sekta ya afya nchini.

Asanteni kwa kunisikiliza,
Luhaga Joelson Mpina (Mb) Mbunge wa Jimbo la Kisesa

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news