MCHANGO WA MBUNGE WA JIMBO LA KISESA, MHE. LUHAGA JOELSON MPINA AKICHANGIA KUHUSU TAARIFA ZA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA MASUALA YA UKIMWI NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA, KILIMO NA MIFUGO TAREHE 12 FEBRUARI 2024 BUNGENI DODOMA
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naongea leo ikiwa Taifa letu limepata msiba mkubwa wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Edward Ngoyai Lowassa bado nakumbuka uwezo wake katika uongozi na uwezo wake katika kusimamia shughuli za Serikali.
Taifa halitamsahau kiongozi huyu mashuhuri aliyesimamia ujenzi wa shule za sekondari kila kata katika Kauli mbiu yake ya Maamuzi Magumu na kwamba kipaumbele cha kwanza ni elimu, kipaumbele cha pili elimu na kipaumbele cha tatu ni elimu.
Pia Hayati Lowassa alisimamia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), aliwakatalia watu wa Misri kuwa wanufaika pekee wa maji ya Ziwa Victoria na kufanya maamuzi magumu ya kuanzisha Mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria enzi za utawala wa Awamu ya Tatu akiwa Waziri wa Maji na Mifugo.
Lakini pia hotuba zake za kiuanamapinduzi na zenye kusisimua alizokuwa akizitoa hasa nyakati za kuahirisha mikutano ya Bunge. Hakika tutamkumbuka daima na Mungu aiweke mahala pema roho ya Marehemu Hayati Mhe. Edward Ngoyai Lowassa, Amina.
Leo ni siku muhimu ambayo tunajadili sekta muhimu kwa mustakabali wa ustawi wa nchi yetu, aidha niwapongeze wawekezaji, wafanyabiashara na wajasiriamali kwa namna wanavyotoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu.
Baadhi ya sekta zinafanya kazi vizuri na wako waheshimiwa mawaziri na watendaji wengine wa Serikali wanastahili pongezi na kuungwa mkono, lakini pia zipo baadhi ya sekta ambazo zinakabiliwa na changamoto kubwa na zinastahili nguvu ya pamoja kutatua changamoto hizo.
Niliwahi kusema hapa bungeni watendaji na Viongozi wazembe, wala rushwa, mafisadi na wafanya dhuluma wasimuingize Mheshimiwa Rais na Chama cha Mapinduzi katika udhaifu wa utendaji wa kazi zao.
Wengine wakibanwa wanasingizia Chama cha Mapinduzi kinachafuliwa au Mheshimiwa Rais amechafuliwa. Udhaifu wao wa kiutendaji hauwezi kubebwa na CCM wala Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anaendelea kulitumikia taifa letu kwa uzalendo mkubwa na amekuwa akiwasisitiza viongozi na watendaji wa umma kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria na amekuwa akichukizwa sana na baadhi ya Viongozi na watendaji wa Serikali wanaojaribu kutakasa uovu wao kwa kutumia jina lake.
Baadhi yao wanafanya hivyo kwa lengo la kulinda vyeo vyao na kufanikisha maslahi binafsi kwa gharama za wananchi masikini.
Nataka niwambie wale wote ambao wamekuwa wakifanya kampeni hizo wafahamu kuwa CCM sio kichaka cha kuficha wahalifu, wazembe, wezi, wala rushwa, mafisadi na wafanya dhuluma, Chama hiki cha Mapinduzi kimejipambanua katika kusimamia misingi ya haki na usawa na kimekataa kugeuzwa kuwa pango la walanguzi tangu kuundwa kwake. Nanukuu ukurasa wa “vi” kipengele cha (3) cha Katiba ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 toleo la 2022. Nanukuu
“…Chama tutakachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini na kupambana na jaribio lolote lile la mtu kumuonea mtu au shirika au chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au kuzorotesha maendeleo ya taifa….” Mwisho wa kunukuu.
Pia katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 (2020-2025) ukurasa wa 163 ibara ya 113 kuhusu Mapambano dhidi ya Rushwa na Ufisadi. Nanukuu
“Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ni suala muhimu kwa kuwa athari zake ni kubwa katika harakati za kufikia maendeleo ya jamii na kiuchumi. Endapo suala la rushwa litaendelea kutokuchukuliwa hatua stahiki, juhudi za kujenga uchumi imara ambao utachangia kupunguza kiwango cha umasikini wa wananchi hazitaweza kuzaa matunda…” Mwisho wa kunukuu
Ibara ya 116 nanukuu “Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa kutambua kuwa rushwa ni adui wa haki na kwamba hakitavumilia vitendo vya rushwa na ufisadi kwa namna yoyote ile. Ili kufikia malengo hayo, Chama cha Mapinduzi kitaielekeza Serikali kuchukua hatua zifuatazo:-
(b) Kudhibiti matumizi mabaya ya ofisi na upotevu wa fedha za umma na kukabili vitendo vya rushwa katika maeneo mbalimbali” mwisho wa kunukuu.
Kwa msingi huo wa Katiba na Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na ahadi za mwanachama wa CCM, wahalifu hawana nafasi wala hifadhi ndani ya CCM na hivyo watafute vichaka vingine vya kujifichia lakini siyo chama pendwa CCM na hapa nataka niseme kwa kujiamini kuwa michango ninayoitoa hapa bungeni ina baraka zote za Chama changu kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani na Katiba ya Chama cha Mapinduzi.
Lakini pia tumeshuhudia Maabara ya kupima ufanisi wa utendaji wa Serikali inayoendeshwa nchi nzima na Chama cha Mapinduzi kupitia Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndg. Paul Christian Makonda ambapo kwa sehemu kubwa malalamiko yanayotolewa na wananchi ni yale yaliyolalamikiwa na waheshimiwa wabunge hapa bungeni na mawaziri kushindwa kuchukua hatua. Huu ni ushahidi kuwa Chama cha Mapinduzi hakilei wezi wala mafisadi.
Waheshimiwa wabunge tusikubali kurudishwa nyuma na tusikubali kuchonganishwa sisi kwa sisi badala yake tuunganishe nguvu tuwakabili vilivyo wazembe, wezi, wala rushwa, mafisadi na wanaofanya dhuluma kwa wananchi wetu ili kuwezesha kujenga misingi imara ya haki na usawa na
kuhakikisha kwamba raslimali za nchi zinawanufaisha watu wote, kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa taifa letu.
2. SEKTA YA AFYA
(i) Uchangiaji wa gharama za matitabu na huduma za afya
Sera ya Afya ya mwaka 2007 inasisitiza juu ya uchangiaji wa gharama ya huduma za afya ili kupanua wigo, kuimarisha na kuendeleza vyanzo vya mapato vya kuendeshea huduma za afya kwa nia ya kuboresha huduma na kupunguza utegemezi na kuimarisha ushiriki wa huduma hizi kwa wananchi.
Pamoja na nia hiyo njema Lakini yapo maeneo yanayolalamikiwa na wananchi kutokana na gharama kubwa na uwezo mdogo kumudu gharama hizo. Na hapa nitaeleza maeneo matatu kama ifuatavyo:-
(a) Matibabu ya Figo
Gharama za kusafisha figo (Dialysis) ni wastani wa Tsh 540,000 kwa wiki kwa mgonjwa anayesafisha figo mara 3 na hivyo gharama ya kusafisha figo kwa mwezi Tsh. 2,160,000 na mwaka ni Tsh 25,920,000.
Gharama hizi ni kubwa na si rahisi wananchi kuzimudu. Yapo matukio mengi jimboni kwangu Kisesa na maeneo mengine nchini yanayotia simanzi na huzuni kubwa kwa watu waliopoteza maisha kwa kukosa uwezo wa kugharamia matibabu ya figo zao.
(b) Gharama za kuhifadhi mwili wa Marehemu
Gharama za huduma hii zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi hasa inapotokea ndugu wa marehemu kukosa uwezo wa kumudu gharama hizo hivyo hupelekea kushindwa kuchukua miili ya wapendwa wao kwa wakati na mara nyingine kutelekeza miili ya marehemu na hivyo kushindwa kupata fursa ya kuzika ndugu zao.
(c) Gharama za matibabu wanazodaiwa ndugu wa Marehemu
Gharama za matibabu wanazodaiwa ndugu wa marehemu baada ya mpendwa wao kufariki, Ndugu wengi wa marehemu wamekuwa wakishindwa kulipa gharama hizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uwezo mdogo, marehemu ndiye alikuwa tegemeo la familia na kuwepo kwa majonzi na simanzi kubwa ya kupotelewa na ndugu yao. Pamoja na Waraka namba moja wa mwaka 2021 eneo hili bado linalalamikiwa na wananchi.
Kama taifa ni lazima tuangalie upya uchangiaji wa huduma za afya za usafishaji figo, gharama za matitabu ya marehemu na gharama za kuhifadhi mwili wa marehemu ili kuondoa mateso, fedheha, majonzi na simanzi kubwa kwa wananchi na wengine ambao wamekuwa wakipoteza maisha bila matibabu.
Pia ifahamike kuwa hawa ndugu zetu wamefariki wakiwa wanalipigania taifa lao katika shughuli mbalimbali za Kijamii, kimaendeleo na kiuchumi.
Hapa tujiulize endapo huduma hizi zitatolewa bure Serikali itapoteza mapato kiasi gani? Ni Bunge hili hili limekuwa likitoa ruzuku na misamaha ya kodi katika maeneo mbalimbali mfano katika siku za karibuni tumepitisha Sheria ya kusamehe kodi wawekezaji mahiri ambapo karibu wawekezaji wengi wakubwa kutoka nje wamekuwa hawalipi kodi.
Pia tulifikia uamuzi wa kuondoa faini kwa wafanyabiashara wanaotenda makosa ya miamala ya Transfer Pricing. Pia tumeweza kutoa elimu bure kuanzia shule ya awali hadi kidato cha 6.
Jambo hili muhimu linalotuhusu sisi sote hatuwezi kushindwa kulitolea msamaha na hivyo ninaomba kuongezea Azimio la kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuwa Bunge liazimie kuwa huduma za kusafisha figo, gharama za matibabu za marehemu na gharama za kuhifadhi mwili wa marehemu zitolewa bure nchini.
(ii) Hospitali za Serikali kuanza kuongeza makalio na matiti
Umma wa watanzania ulitangaziwa na Mkuu wa Idara ya Upasuaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, Dk. Erick Muhumba kupitia Tangazo la Tarehe 10 Oktoba 2023 kuwa kuanzia Tarehe 27-28 Oktoba 2023 huduma za kuongeza makalio na matiti zitaanza kutolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili- Mloganzila.
Nimefuatilia Hotuba mbalimbali za Viongozi wakuu wa nchi, taarifa na Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya na taarifa ya Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika mwaka wa fedha 2023/2024 na miaka mingine ya nyuma, huduma hii ya kuongeza makalio na matiti haijaelezwa mahali popote. Pia nimepitia Sera ya Afya, Sheria, Kanuni na miongozo ili kuona kama jambo hili linaruhusiwa au laa na kubaini yafuatayo:-
(a) Suala la kuongeza makalio na matiti halimo kwenye Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ambayo ndiyo sera inayotoa mwongozo wa utoaji huduma zote za afya nchini, huduma za uongezaji wa makalio na matiti ni huduma za anasa na hufanyika kwa watu ambao hawana changamoto yoyote ya kiafya ni upasuaji wa kimapambo (Cosmetic Surgery) hufanyika kwa lengo la kupendeza au kubadili mwonekano (shepu).
Sera ya Afya ya mwaka 2007 aya ya 5.5 imesisisitiza utoaji wa huduma ya utengemao katika nyanja za kijamii na kitabibu kwa kupewa mazoezi ya viungo, ushauri nasaha au kuwekewa viungo bandia pale mhusika anapopoteza kiungo kama mkono au mguu (Plastic Surgery), huduma ya upasuaji mwingine kama kuungua moto, vichwa vikubwa, midomo sungura. Nk. lakini suala la kuongeza matiti na makalio au upasuaji wa kimapambo haukutajwa mahala popote kwenye sera.
(b) Serikali imeanzisha huduma za kuongeza makalio na matiti bila idhini ya Bunge lakini pia hakuna Sheria, Kanuni wala mwongozo wa kusimamia suala hili (Legal Framework) hivyo haijaainishwa namna huduma hiyo itakavyotolewa. Haki za mteja na daktari hazijawekwa bayana mfano madhara yakitokea fidia itatolewaje kwa mteja, Daktari anayetoa huduma hiyo analindwa vipi dhidi ya madhara yatakayotokea pia gharama zilizotangazwa hazipo kisheria.
(c) Serikali imetangaza na kuanza kutoa huduma ya kuongeza makalio na matiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila bila kuweka wazi madhara ya upasuaji huo kwa wananchi.
Baadhi ya nchi zinazotoa huduma za kuongeza makalio imekuwa ikiripotiwa kuwepo kwa madhara kwa watu waliopatiwa huduma hizo kama kupata magonjwa ya saratani, kuathiri afya ya uzazi na kusababisha ugumba, kuhudhuria kliniki mara kwa mara, kuathiri viungo vingine kwenye mwili na kusababisha magonjwa ya moyo, muonekano au shepu kuwa sio wa kudumu, makalio kubomoka wakati wowote na ngozi ya mwili kubadilika rangi. Hivyo kama taifa ni muhimu kujiridhisha na athari hizi kabla ya kuanza kutoa huduma hii.
(d) Tangazo la kuongeza makalio limewaalika watu wote kwenda Mloganzila kupatiwa huduma hiyo, Hii ina maana kuwa huduma hii itatolewa kwa watu wa rika zote wakiwemo watoto na wanafunzi. Badala ya kuwekeza kikamilifu kuwaandaa vijana kukabiliana na maisha na ujenzi wa taifa lao kwa kuwapatia elimu, ujuzi na maarifa, tunawabebesha mzigo wa makalio na matiti.
(e) Kwa kuwa gharama za kuongeza makalio zilizotangazwa na Serikali Milioni 12 hadi Milioni 18 ni kubwa na hivyo ni watu wachache watakaokuwa na uwezo wa kudumu gharama hizo na hivyo kuchochea matabaka baina ya walionacho na wasio nacho ndani ya nchi.
(f) Kukosekana kwa takwimu za uhitaji wa huduma ya kuongeza makalio nchini, Serikali ituambie kuna watu wangapi waliokwenda nje ya nchi kuongezwa makalio?
Na je tangu tuanze kutoa huduma hiyo hapa nchini ni watu wangapi wamepewa huduma hiyo na fedha kiasi gani imekusanywa na Serikali.
(g) Serikali kutokuweka wazi uwekezaji uliofanyika kuwezesha huduma hii ya kuongeza makalio kutolewa, Serikali iweke wazi kiasi gani cha fedha kimetumika kufanikisha utoaji wa huduma ya kuongeza makalio, katika majengo, vifaa, mitambo na wataalamu. Je kwanini huduma hiyo ilikuwa haitolewi siku za nyuma na kwanini hospitali za binafsi nchini kama Kairuki, Aga Khan nk. hazitoi huduma hii?
Leo tunaambiwa huduma hizi za kuongeza makalio na matiti ni kati ya Tsh. Milioni 12 mpaka Tsh. Milioni 18 ambapo watu wengi wanaweza kushindwa kumudu gharama hizo, Je akitokea mfadhili wa kugharamia huduma hii na kuanza kutolewa bure kwa wananchi wote nchini kwa watu wa rika zote, tutakuwa tunatengeneza taifa la aina gani?
Kama suala la uongezaji wa makalio na matiti halijaruhusiwa katika Sera ya Afya na hakuna sheria, kanuni wala miongozo inayosimamia suala hili, Huduma hii ya kuongeza makalio na matiti hapa nchini inafanyika kwa idhini ya nani?
Nashauri huduma ya kuongeza makalio na matiti ipigwe marufuku nchini hadi hapo tutakapokuwa na muafaka wa kitaifa na pale tutakapokuwa tumejiridhisha kuhusu madhara yanayoweza kutokea kwa watu wanaopewa huduma hiyo na athari ambazo jamii inaweza kupata.
Pia ninaomba kuongeza azimio kwenye Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwamba Bunge liazimie kwamba huduma za kuongeza makalio na matiti zipigwe marufuku nchini na ufanyike uchunguzi wa kina kubaini kilicho nyuma ya pazia na kujua tumefikaje hapo na kwamba wote waliohusika kuruhusu Hospitali za umma kutoa huduma ya kuongeza makalio na matiti wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa Sheria za nchi.
3. SEKTA YA KILIMO
3.1 Changamoto za ugawaji na usambazaji wa mbolea ya ruzuku
Taarifa ya Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyowasilishwa haijaeleza mbolea ya ruzuku iliyotolewa kwa Wakulima na fedha zilizotumika hadi sasa katika msimu wa kilimo wa 2023/2024 na pia hakuna tathmini iliyofanywa ya ugawaji na usambazaji wa mbolea ya ruzuku msimu wa kilimo 2022/2023 ili kuliwezesha Bunge kupata taarifa sahihi juu ya mafanikio na changamoto katika eneo la utoaji wa mbolea ya ruzuku nchini.
Tulipoanza mfumo wa mbolea ya ruzuku msimu wa kilimo 2022/2023 tulikumbana na changamoto nyingi ikiwemo wakulima kuuziwa mbolea feki, mbolea iliyokwisha muda wa matumizi, mbolea iliyochanganywa na mchanga, mfuko mmoja wa mbolea kuuzwa mara mbili, mbolea ya ruzuku kutoroshwa nje ya nchi, mbolea kuuzwa kwa bei isiyo na uhalisia, wakulima zaidi ya milioni 2.2 kukosa mbolea, kuwa mfumo wa ugawaji na usambazaji wa mbolea ya ruzuku ambao una changamoto lukuki ikiwemo kukosa usalama (security) na mfumo huo kuanzishwa bila kibali cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kinyume cha Kifungu cha 24 (2) (a) cha Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019.
Hapa Bungeni ilielezwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe kuwa alipata kibali cha Mamlaka ya Serikali Mtandao katika kuanzisha mfumo wa mbolea ya ruzuku, nilikataa na leo nasisitiza kuwa mfumo wa mtandao wa Mbolea ulianzishwa bila kibali cha eGA na ndiyo maana umekuwa na changamoto lukuki na kuwatia hasara kubwa Wakulima na Serikali.
Kutokana na ubishani huo kwa Mamlaka niliyopewa katika kifungu cha 29
(1) na (2) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya Mwaka 2008 na Marekebisho yake ya Mwaka 2020 nilimuandikia barua CAG ya Tarehe 29 Mei 2023 yenye Kumb.Na.MB/KSS2023/27 nikimuomba kufanya ukaguzi maalum katika matumizi ya fedha za maendeleo na utoaji na usambazaji wa mbolea ya ruzuku katika msimu wa kilimo 2022/2023 ili kujua nini kilichojificha nyuma ya pazia. Naamini taarifa hii itakuwa ni sehemu ya Ripoti ya CAG ya Machi 2024.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Bashe tarehe 7 Februari 2024 hapa Bungeni alikiri kuwepo kwa changamoto nyingi katika usambazaji na ugawaji wa mbolea ya ruzuku msimu 2022/2023 ambao umesababisha hasara kubwa kwa Wakulima na Serikali.
Hata hivyo Waziri huyo wakati wa kuanzisha mfumo wa mbolea ya ruzuku alipewa tahadhari hapa Bungeni juu ya changamoto zitakazotokea lakini akaapa kuwa Wizara imejipanga na wabunge wasiwe na wasiwasi. Leo imekuwaje hadi Waziri akiri kuwepo kwa changamoto lukuki katika msimu wa kilimo 2022/2023? Lakini mbaya zaidi Wizara ya Kilimo ikaendelea na mfumo wa ruzuku ya mbolea katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024 bila ya kufanya tathmini ya kina ya msimu uliopita na kuarifu umma.
Kwa kuwa Waziri alishajiapiza mbele ya watanzania kupitia Bunge hili kuwa yuko tayari kubeba gharama yoyote.
Waziri Bashe alisema Bungeni I’m ready to bare any cost na akaapa kuwa hatokuwa tayari kuwatia umasikini wakulima wa nchi hii na baada ya hapo kilichotokea tukaanza kuona Wakulima wanafia kwenye foleni za kusubiri mbolea za ruzuku, wengine kuuziwa mbolea feki zilizoua ardhi na kudumaza mazao wakiwemo Wakulima wetu wa Nzega (malalamiko yaliyotolewa taarifa ya habari ITV).
Pia kuwepo malipo ya Tsh. Bilioni 68 zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, kuwepo madai hewa na mbolea hewa iliyosababishwa na mfumo kukosa usalama na kuruhusu Multiple Scanning na Wakulima zaidi ya milioni 2.2 waliojiandisha kukosa mbolea.
Kwa kuwa bado kuna dalili nyingi za wananchi kuendelea kuuziwa mbolea feki zinazoua ardhi na kudumaza mazao mfano huko Tabora hivi majuzi Tarehe 31 Januari 2024 Kampuni ya YARA Tanzania Limited kukamatwa na shehena ya mifuko 13,811 sawa na tani ya 69 za mbolea iliyokwisha muda wa matumizi tangu Agosti 2023 ikibadilishwa kwenye mifuko mingine mipya inayoonyesha mwisho wa matumizi ni mwaka 2026.
Pia huko Mbeya Kampuni ya YARA Tanzania Limited ilikamatwa na Tani 7 za Mbolea zilizokwisha muda wa matumizi. Pia huko Njombe Kampuni ya
Minjingu Mines and Fertilizer Limited (MMFL) ilikamatwa na Mifuko 776 ya mchanga kwenye ghala la kuhifadhia mbolea.
Maswali ya kujiuliza kwanini mbolea iliyokwisha muda wa matumizi tangu Agosti 2023 iendelee kuwa kwenye maghala hadi sasa, Huu ni uthibitisho kuwa Makampuni haya yamekuwa yakifanya hii biashara haramu kwa muda mrefu na kupelekea Wakulima kuuziwa mbolea feki na iliyokwisha muda wa matumizi.
Hali hii imekuwa ikisababisha kudumaza mazao, kuharibu afya ya udongo na kuwatia hasara kubwa wakulima na taifa kwa ujumla. Pia matukio mengine bado yanaripotiwa kuendelea ya utoroshaji wa mbolea ya ruzuku nk.
Hivyo basi naomba kuongeza azimio kwenye taarifa ya Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuwa Bunge liazimie kwamba iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza uhalali wa mfumo na zoezi la ugawaji na usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima msimu wa kilimo 2022/2023 na kupendekeza hatua sahihi za kuchukua kwa mujibu wa sheria za nchi.
3.2 Makato makubwa ya Wakulima wa Pamba
Katika msimu wa kilimo wa 2021/2022 bei ya Pamba ilipokuwa Tsh. 1,560 Wakulima wa Pamba walikatwa kiasi cha Tsh. 400 sawa na 26% na mwaka 2022/2023 bei ya pamba ilipokuwa 1,360 walikatwa Tsh. 300 sawa na 22% kwa kila kilo ya pamba waliyouza.
Imekuwa ikielezwa kuwa makato haya ni kwa ajili ya kugharamia mbegu na viuatilifu, Makato haya ni makubwa na yanasababisha bei ya pamba kushuka kwa kiwango kikubwa na kuwatia hasara kubwa Wakulima wa Pamba nchini.
Lakini imekuwa haielezwi thamani ya mbegu na viuatilifu vinavyonunuliwa na Bodi ya Pamba na kusambazwa kwa Wakulima na kama makato yanaendana na thamani ya pembejeo zilizotolewa.
Aidha matumizi ya fedha zinazokatwa hayako wazi na hayana uthibitisho hali inayopelekea malalamiko makubwa kwa wakulima. Wakulima kupata hasara kila mwaka na kukata tamaa ya kuendelea na kilimo cha Pamba hali inayopelekea kushuka kwa uwezo wa kununua (purchasing power) na Serikali kukosa mapato na fedha za kigeni.
Bodi ya Pamba imewageuza Wakulima wa pamba kuwa manamba wao, ilikuwaje Waziri wa Kilimo aruhusu Bodi ya Pamba kufanya uharamia mkubwa kwa kiwango hiki kwa Wakulima wa Pamba?
Naomba kuongezea Azimio kwenye Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuwa Bunge liazimie kwamba makato ya bei ya pamba yanayofanywa na Bodi ya Pamba yasitishwe mara moja na CAG afanye ukaguzi wa dharura katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021, 2022 na 2023 ili kujiridhisha na uhalali wa makato na matumizi ya fedha hizo.
3.3 Fidia kwa wananchi walioathirika na uvamizi wa wanyama wakali (Tembo)
Uvamizi wa Tembo na Wanyama wakali wengine katika makazi na mashamba ya wakulima umeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo nchini ambapo mazao yanashambuliwa yakiwa shambani na majumbani, nyumba kubolewa, mifugo imeuawa na watu kujeruhiwa, kupata ulemavu wa kudumu na kuuawa. Uvamizi wa wanyama wakali umerudisha nyuma jitihada za wananchi kujiletea maendeleo hasa waishio kando kando ya hifadhi na kutishia usalama wao.
Licha ya uvamizi huu kufanyika mara kwa mara na taarifa kutolewa serikalini lakini Serikali haijatoa takwimu ni hekta ngapi na tani ngapi za mazao ya wananchi zimeharibiwa, fidia kiasi gani ambayo wananchi wanadai hadi sasa na kiasi ambacho kimekwisha fidiwa kama kifuta machozi na kifuta jasho. Pamoja na kwamba fidia zinazotolewa ni ndogo ikilinganishwa na madhara yaliyotokea lakini zimekuwa hazitolewi kwa wakati na kupelekea mateso makubwa kwa wananchi waliokutana na dhoruba hizo.
Mfano wilayani kwangu Meatu kwa mwaka 2022/2023 kiasi kinachodaiwa na wananchi cha kifuta jasho ni Tsh. 122,094,000 kwa kaya 651 na kifuta machozi ni Tsh. 6,100,000.
Kama Serikali imeweza kulipa Tsh Bilioni 44 kwa ajili ya watumishi wa umma waliofukuzwa kazi kwa vyeti feki, haya madai ya wananchi wanyonge na masikini yanashindikanaje kulipwa na Serikali? fikiria familia ambayo baba mwenye familia ameuawa na tembo, nyumba imebomolewa, chakula chote kimeliwa na ameacha mjane na watoto.
Naomba kuongeza Azimio kwenye Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuwa Bunge liitake Serikali kuwasilishwa madai ya kifuta machozi na kifuta jasho ya nchi nzima ili Bunge lichukue nafasi yake na kuhakikisha kuwa madai hayo yamelipwa haraka kwa wahusika.
4. SEKTA YA MIFUGO
Wafugaji walioshinda kesi Mahakamani lakini Serikali haijarejesha mifugo yao ambapo kwa kipindi cha Mwaka 2017 hadi Mei 2023 ni jumla ya ng’ombe 11,438, punda 13 na kondoo 9 katika maeneo ya Hifadhi za WMA, TAWA, TFS na TANAPA. Mambo haya yanachochea chuki baina ya wananchi na Serikali yao na hii ni kwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ambapo Mahakama ndio chombo cha mwisho cha utoaji haki.
Wafugaji kutoka Mkoa wa Simiyu katika Wilaya za Meatu na Itilima wanadai Jumla ya ng’ombe 1,700, punda 9 na milioni 8, madai haya yana miaka 7 sasa wafugaji wanafuatilia haki zao bila mafanikio yoyote. Nani aliyekataa huko serikalini kulipa madai haya halali kwa mujibu wa sheria?
Katika maeneo mengine Serikali imekuwa ikilipa fidia na madai mbalimbali kama fidia ya ardhi, madeni ya wakandarasi, wazabuni na watumishi, na kutekeleza hukumu mbalimbali za Mahakama kwanini hili la wafugaji limeshindikana?
Wafugaji hawa wanafuatilia haki yao Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Fedha kwa zaidi ya miaka 7 bila mafanikio yoyote. Wamekuwa wakipigwa danadana tu na kila wizara kutupiana Mpira.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa alishatoa maagizo wafugaji hawa warejeshewe mifugo yao tangu mwaka 2022, lakini aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumaro aliahidi Bungeni kuwa wafugaji wote waliopewa tuzo na Mahakama wapewe haki yao kama Mahakama ilivyoamuru na Waziri wa Maliasili na Utalii wa sasa, Mhe. Angela Kairuki alipokutana na wabunge wa Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Mara 10 Februari 2024 aliahidi kulifanyia kazi mapema suala hili.
Hapa Bungeni mimi na waheshimiwa wabunge wengine kwa zaidi ya miaka
3 tumekuwa tukiikumbusha Serikali kuhusu kutekeleza hukumu ya Mahakama ya kurejesha mifugo kwa wafugaji au kuwalipa fidia lakini jambo la kusikitisha hadi sasa ninavyozungumza hakuna utekelezaji wowote.
Kwa kuwa kinachofanywa na wizara hizo nne ni uvunjifu wa Sheria na Katiba ya nchi, lakini pia ni dhuluma kubwa kwa wananchi wetu ambayo haitegemewi kufanywa na Serikali.
Na kwa kuwa, familia za wafugaji hawa zilionewa na Serikali kwa kubambikizwa kesi na kunyang’anywa mifugo yao kinyume cha sheria na kwamba hivi sasa familia za wafugaji hawa zimekumbwa na ufukara na umasikini mkubwa.
Hivyo basi naomba kuongeza Azimio kwa Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuwa Bunge liazimie kwamba Serikali iwalipe fidia wafugaji hao ndani ya mwezi 1 na taarifa itolewe bungeni.
5. SEKTA YA UVUVI
Uvuvi haramu
Katika kipindi cha miaka ya 2017 uvuvi haramu wa kutumia nyavu haramu na mabomu ulikuwa umekithiri katika maeneo yote ambapo shughuli za uvuvi zilikuwa zinafanyika na kusababisha raslimali za uvuvi kupungua kwa kiasi kikubwa na pia kuhatarisha maisha ya binadamu na viumbe wengine wa majini, mfano katika Ziwa Victoria samaki aina ya Sangara wazazi walibaki 0.4%, samaki wachanga walifikia 96.6%, samaki wanaoruhusiwa kuvuliwa kisheria walibaki 3.3% tu (kati ya sentimita 50 hadi sentimita 85) na wastani wa urefu wa sangara ulipungua na kubaki sentimita 16 tu.
Huku upande wa ukanda wa bahari kutoka Moa Tanga hadi Msimbati Mtwara milipuko ya mabomu ilikuwa karibia kila saa.
Serikali ilianzisha kampeni kubwa ikiwemo kuanzisha operesheni ya kuzisaka na kuziteketeza nyavu haramu zilizokuwa zinatumika katika maeneo ya uvuvi yakiwemo Makokoro, Timba, mabomu na matumizi ya sumu na kuzuia uingizaji holela na utoroshaji wa raslimali za uvuvi nje ya nchi. Pia kutokana na kushamiri kwa uvuvi haramu wananchi walipiga kelele na kutoa ushirikiano kwa Serikali.
Kupitia operesheni hizo mafanikio makubwa yalipatikana ikiwemo kukamata na kuteketezwa kwa moto jumla ya vipande 1,280,906 vya nyavu haramu, mabomu 4,583 yalikamatwa na kuharibiwa kwa mujibu wa sheria na watuhumiwa 14,384 walikamatwa na kutozwa faini na wengine kufikishwa mahakamani.
Kati ya watuhumiwa hao 323 ni kutoka nje ya nchi waliokamatwa wakivua katika maeneo ya nchi yetu kinyume cha sheria na huku wakitumia zana haramu. Pia jumla ya meli 21 zilibainika kufanya uvuvi haramu katika ukanda wa uchumi wa Bahari Kuu ambapo meli ya BUAH NAGA 1 kutoka nchi ya Malaysia ilikamatwa na watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kutozwa faini ya jumla ya shilingi Bilioni 1 au kifungo cha miaka 20. Mmiliki, wakala na Nahodha wanatumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini hiyo.
Aidha ukamataji, utaifishaji na uteketezaji wa vyavu haramu na mabomu ulifanyika baada ya kupata kibali cha MAHAKAMA na pia samaki waliotaifishwa wanaofaa kwa matumizi ya binadamu waligawiwa katika taasisi za umma baada ya kupata kibali cha Mahakama. Shughuli zote za uteketezaji zilihusisha wananchi wa maeneo husika, vyombo vya usalama, BMU, viongozi na watendaji wa Serikali wa maeneo husika ili kuwa na uwazi na kuepuka nyavu hizo haramu kuuzwa kinyemela kwa wananchi.
Mafanikio na faida zilizopatikana baada ya kuendesha operesheni Sangara, Operesheni NMATT na Operesheni JODARI mambo yalibadilika na takwimu zilibadilika.
Kuongezeka kwa wingi wa samaki (biomass) katika maji yetu hususan katika Ziwa Victoria ambapo samaki aina ya Sangara waliongezeka kutoka tani 417, 936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 95.5 na urefu wa sangara umeongezeka kutoka wastani wa sentimita 16 hadi sentimita 25.2. Aidha dagaa wameongezeka kutoka tani 660,333 mwaka 2017 hadi kufikia tani 936,247 mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 41.8.
Aidha mafanikio mengine ni pamoja na kupungua kwa samaki wachanga aina ya sangara wenye urefu wa chini ya sentimita 50 kutoka asilimia 96.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 62.8 mwaka 2019, kuongezeka kwa samaki aina ya sangara wenye urefu wa kuanzia sentimita 50 hadi 85 (wanaofaa kuvuliwa) kutoka asilimia 3.3 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 32 mwaka 2019 na kuongezeka kwa samaki aina ya sangara wenye urefu wa juu ya sentimita 85 (wazazi) kutoka asilimia 0.4 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019 hali iliyopelekea hadi samaki waliokuwa wamepotea wakaanza kuonekana. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na nchi zote zinazozunguka Ziwa Victoria mwaka 2020.
Mauzo ya samaki nje ya nchi yaliongezeka kutoka bilioni 379.25 mwaka 2015/2016 hadi kufikia Bilioni 692 mwaka 2019/2020 huku uagizaji wa samaki kutoka nje ya nchi ukibaki asilimia 0.
Mafanikio haya yalipelekea Hayati Dk. John Pombe Joseph Magufuli, Rais awamu ya Tano na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa, aliipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kazi nzuri ya usimamizi wa raslimali za uvuvi na kuchangia kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi na kukuza uchumi naomba ninukuu sehemu ya Hotuba yake ya kuhitimisha Bunge la 11 aliyoitoa hapa bungeni Tarehe 16 Juni 2020. Nanukuu.
“Mheshimiwa Spika nakumbuka kuna wakati Waziri wa Uvuvi na Mifugo Mheshimiwa Mpina alikuwa akitembea na rula hadi kwenye migahawa lakini hii ilikuwa ni katika kazi ya kuhakikisha tunapata mafanikio haya ambayo tumeyapata…..kwenye uvuvi, sangara kwenye Ziwa Victoria wameongezeka kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020 na urefu wa sangara umeongezeka kutoka wastani wa sentimita 16 hadi sentimita 25.2 na hivyo samaki wetu kuanza kuhitajika kwa kiasi kikubwa katika Soko la Ulaya na ninyi ni mashahidi waheshimiwa wabunge ndege zimeanza kuja Mwanza na kubeba samaki wetu kwa ajili ya kupeleka nje na kwa kuzingatia hilo mauzo ya samaki nje ya nchi yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 379 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 692 mwaka 2019 haya sio mambo madogo Mheshimiwa Spika kwa lengo la kukuza uchumi” Mwisho wa kunukuu.
Huu uvuvi haramu ulioshamiri hivi sasa umesababishwa na nini? ambapo samaki wamepungua kwa asilimia 50 kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kufungwa kabisa kutokana na samaki kuisha, pia maeneo mengine ya uvuvi, uvuvi haramu umeshamiri Bahari ya Hindi, Bwawa la Nyumba ya Mungu, Bwawa la Mtera, Ziwa Nyasa nk. viwanda vya samaki kufungwa na vingine kupunguza uzalishaji na wafanyakazi kutokana na uhaba wa samaki.
Uvuvi haramu unaoendelea ni ushahidi kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeacha misingi imara ya Usimamizi raslimali za uvuvi nchini (FRP), Sera, Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2009 na Marekebisho yake ya Mwaka 2020 pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 na badala yake Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatumia Hekima na Busara katika Ulinzi wa raslimali za uvuvi.
Kitendo cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuacha kusimamia Sheria za ulinzi wa raslimali za uvuvi na kusababisha kushamiri kwa uvuvi haramu kimemshtua Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambapo Tarehe 30 Januari 2024 akiwa jijini Mwanza, aliitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutokomeza vitendo vya uvuvi haramu na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote wanaojihusisha na uvuvi haramu, vyavu haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi.
Pia Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotoa taarifa yake Februari 2023 hapa bungeni ilieleza kuwa usimamizi wa raslimali za uvuvi umeanza kuwa hafifu na kusababisha samaki kupungua ikitolea mfano katika Ziwa Victoria kwa utafiti uliofanyika hivi karibuni unaonyesha kuwa samaki aina ya Sangara wamepungua kwa asilimia 50 na samaki wazazi wamepungua na kufikia asilimia 0.4 kutoka asilimia 5.3 mwaka 2020. Baadhi ya viwanda vya samaki kufungwa na wananchi kupoteza ajira.
Kwa kuwa, Bunge lilishaitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuchukua hatua dhidi ya uvuvi haramu tangu Februari 2023 na Mheshimiwa Rais ameshatoa maelekezo kudhibiti uvuvi haramu
Na kwa kuwa, hali inazidi kuwa mbaya na kupelekea baadhi ya maeneo ya mavuvi kufungwa, viwanda kufungwa na kupoteza ajira za watanzania waliopo kwenye mnyororo wa biashara ya mazao ya uvuvi,
Hivyo Basi, Bunge liitake Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwasilisha taarifa bungeni ya nini kilichosababisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushindwa kudhibiti uvuvi haramu ili Bunge lichukue nafasi yake.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa wabunge kazi ya uwakilishi wa wananchi hasa wanyonge ni ngumu sana, ina lawama nyingi na ni hatari kwani kila unaposimama kwa nafasi yako kupinga mambo yanayofanywa kinyume na utaratibu utaonekana mbaya kwa baadhi ya watu kwa kuwa umegusa maslahi yao binafsi.
Hata hivyo tusiogope wala tusirudi nyuma kwani ndiyo kazi tulizopewa na watanzania na tukala kiapo cha uaminifu mbele ya umma na mbele za Mwenyezi Mungu.
Katika hizi sekta nne za afya, kilimo, mifugo na uvuvi kwa uchambuzi mdogo nilioufanya mmeona namna ukiukwaji mkubwa wa Sheria unaofanywa, kuwepo kwa sheria na sheria ndogo kandamizi, matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma na kukosekana kwa usawa na haki kwa wananchi.
Ni lazima tuendelee kutimiza jukumu letu kikamilifu la Kikatiba la kuisimamia Serikali na tupambane kwa hali na mali kuhakikisha kuwa tunakomesha kila aina ya dhuluma na hatuna chaguo zaidi ya kuendeleza mapambano (Unstoppable Force) hata kama maadui watazidi kuongezeka Mungu wa mbinguni yupo na kamwe hatotuacha.
Nawasilisha,
……………………………………..
Luhaga Joelson Mpina (Mb) Mbunge wa Jimbo la Kisesa