Mifumo ya malipo nchini inamuhakikishia usalama mlipaji na mlipwaji-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, matumizi ya mifumo ya malipo nchini ni njia nzuri ambayo inamuhakikishia mlipaji na mlipwaji usalama wa maisha yake huku ikiwa rahisi,miamala ya kasi,rahisi kufuatilia na usalama ulioimarishwa.
Hayo yamesemwa leo Februari 16,2024 jijini Zanzibar na Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Fabian Kasole wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya Kurugenzi hiyo.

Ni katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi nchini ambayo imeratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika ofisi za makao makuu ndogo Zanzibar.

"Kwanza tutambue kwamba,kuchapisha fedha ni gharama, na wakati mwingine unaweza kukuta ni gharama sana kuchapisha sarafu kuliko ile sarafu yenyewe.

"Hivyo, tunapotumia mifumo ya malipo (kidigitali) gharama zote za usafirishaji, usambazaji, uchapaji fedha zikiwa chakavu zinapungua na usalama wa watu wetu unakuwa mkubwa."

Amesema, Benki Kuu inaendelea kutoa elimu kwa umma ili waweze kufahamu umuhimu wa matumizi ya mifumo ya malipo kwa ajili ya shughuli za kila siku nchini.

"Suala zima la kulinda mifumo ya malipo lipo kwa Benki Kuu kama mtunga sera, na lipo kwa mtoa huduma. Kwa hiyo, ili ujilinde unapaswa usiwe na hofu kuhusu hii mifumo."

Pia, amesema mifumo hiyo inaongeza usalama kwa mlipaji na mlipwaji. "Mifumo inaongeza usalama mkubwa kwa mlipaji na mlipwaji,mfano unabeba hela nyingi unatembea kumbe jamaa wameshakuona unakuwa hatarini,kwa hiyo usalama wako na unayemlipa ni muhimu."

Vile vile amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika mifumo ya malipo, ambayo imekuwa ikitengenezwa na vijana wa Kitanzania wenyewe nchini.

"Kwa mfano Mpesa (2007) imezaliwa Tanzania, ikakua Kenya, halafu ikarudi tena ikakuwa Tanzania ilianza na kampuni ya vijana wa kitanzania E-fulusi (E-Fulusi Africa (T) Limited).

"Mambo kwa sasa yamerahisishwa sana katika huduma za fedha, tuna makundi mawili ya malipo, mfumo wa malipo makubwa (kutuma zaidi ya milioni 50). Ni malipo ambayo ni makubwa na ya kila siku ambayo yana uharaka, na taasisi nyingi zinatumia huu mfumo.

"Kuna mfumo wa malipo madogomadogo, thamani yake ni ndogo,lakini ni malipo mengi katika mzunguko wa kila siku."

Amesema, kurugenzi hiyo inasimamia maeneo makubwa mawili ambayo yanajumuisha kusimamia mifumo ya malipo ya nchi inayoendeshwa na taasisi za fedha na zisizo za fedha.

"Taasi hizo ni kama vile kampuni za simu na zile za teknolojia katika sekta ya fedha (fintech). Jukumu lingine ni kuendesha mifumo ya malipo kwa ajii ya kuleta ufanisi na usalama wa malipo nchini,"amesema Bw.Kasole.

Aidha, amesema badala ya wewe kwenda kuchukua fedha taslimu, mifumo yote inaweza kukuruhusu kununua bidhaa au kulipa huduma popote ulipo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news