Mkomi awapa darasa maafisa rasilimaliwatu nchini

NA LUSUNGU HELELA

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amewataka Maafisa Rasilimaliwatu wote serikalini kuhakikisha wanaweka kumbukumbu sahihi za watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu kabla ya miezi sita ili kuwaondolea usumbufu wa kufuatilia mafao yao pindi wanapostaafu.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kikao kazi na watumishi wa Ofisi yake, ikiwa ni mwendelezo wa kuhimiza utendaji na uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini.

Katibu Mkuu Mkomi amesema haikubaliki mtumishi anapewa barua ya kustaafu huku baadhi ya taarifa za michango ya mafao yake haiko sawa.
‘’Mtumishi anapewa barua ya kumtaarifu kustaafu kabla ya miezi sita halafu baadaye anaanza kusumbuliwa eti michango ya mafao haionekani, sasa hiyo barua aliyopewa kabla ya miezi sita ilikuwa na maana gani," amehoji Bw. Mkomi.

Amesisitiza kuwa, suala hili lazima lifanyiwe kazi kwa kuwa watumishi hao wanaostaafu wamelitumikia taifa kwa moyo hivyo kuhangaishwa sio haki.

Katika hatua nyingine, Bw. Mkomi ametoa onyo kwa watumishi wanaovujisha siri za serikali ambapo ameahidi wale wote watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Amesema, kitendo hicho ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma ambapo ametumia fursa hiyo kuwaasa watumishi hao kujiepusha na tabia hiyo.

Pia, Katibu Mkuu Mkomi amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utendaji wanapotoa huduma kwa wananchi kwani maadili ndio msingi wa utumishi wa umma.

Kwa kusisitiza hilo amewataka watumishi wa Ofisi yake kuwa mfano wa uzingatiaji wa maadili kwa vile Ofisi hiyo ni kioo cha Utumishi wa umma nchini.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa Magufuli amemshukuru Katibu Mkuu Mkomi kwa kutenga muda kuzungumza na watumishi wa Ofisi yake licha ya majukumu mazito yanayomkabili huku akiahidi maagizo yote aliyoyatoa yatatekelezwa.
Awali katika kikao kazi hicho, mada mbalimbali zilitolewa kwa watumishi hao ikiwemo Maadili kwa Watumishi wa Umma, Kukabiliana na Msongo wa Mawazo, PSSSF Kiganjani na faida ya kujiunga na SACCOS ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news