Mradi mkubwa wa uchimbaji madini Tembo-Tanzania kuzalisha malighafi za injini za ndege,nyuklia na vifaa vya hospitali

TANGA-Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuwezesha upatikanaji wa Leseni Kubwa ya uchimbaji madini (Special Mining License - SML) kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sands inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Strandline ambayo itapelekea kuanza kwa mradi mkubwa wa uchimbaji Madini Tembo katika Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.
Hayo yameelezwa leo Februari 20, 2024 na Waziri wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde alipofanya ziara ya kutembelea sehemu ya eneo la mradi huo iliyopo katika kijiji cha Stahabu, Kata ya Mikinguni Wilayani Pangani-Tanga.

"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wizara ya Madini kuhakikisha tunawezesha uanzishwaji wa miradi hii mikubwa na ya kimkakati ambayo itapelekea si tu ustawi wa uchumi wa Nchi yetu, bali kuwa kichocheo cha maendeleo na ustawi wa Wilaya ya Pangani na wananchi wanaozunguka mradi huu."

Amesema ni dhamira ya Serikali kuona wawekezaji wakubwa wenye nia njema na nchi ya Tanzania wanapewa ushirikiano ili kuwezesha shughuli zao kwa manufaa ya Taifa.
Mradi huo unatarajiwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 125 ambao uhai wake unakadiriwa kuishi kwa miaka 20 hadi 25 utatekelezwa katika Vijiji 8 vilivyopo katika Kata za Mikinguni, Mwera, Tungamaa na Bweni-Wilaya ya Handeni,Mkoani Tanga.

"Nimefurahishwa na utayari wa wananchi wanaoguswa na mradi kupisha kuanza kwa mradi, na kwa kuwa ni hatua muhimu sana kwani itarahisisha kuanza mradi kwa wakati na kuondoa changamoto ya migogoro kati ya wananchi na mwekezaji," amesema Mavunde.
Akizungumza kwa niaba ya Mwekezaji, Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Ltd ambaye anawakilisha Hisa za Serikali, Mhandisi Heri Gombera amesa kwamba mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka 2026 na unatarajiwa kuzalisha tani milioni 8 za madini mbalimbali kwa mwaka yakiwemo titanium, ilmenite, rutile, zircon na monazite ambayo pamoja na matumizi mengine hutumika pia kuzalisha malighafi za injini za ndege, nyuklia,vifaa vya hospitali na viwanda vya marumaru na rangi.
Aidha, Mhandisi Gombera amebainisha kwamba Kampuni ya Nyati Minerals Sand ipo tayari kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo na kuongeza kuwa pindi watakapopata Leseni yao kwa kushirikiana na Wadau wote wataanza zoezi la tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi ili kupisha kuanza kwa mradi huo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mhe. Zainab Abdallah amemahukuru Mhe Rais Samia kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini ambayo yamepelekea mradi huo kuanzishwa Wilayani Pangani na kwamba pindi mradi huo utakapoanza utaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Pangani kuongeza kipato chao na kujikimu kutokana na ujira watakaokuwa wanaupata kutoka kwenye mradi sambamba na kuchochea uchumi wa wilaya hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news