RUVUMA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito viongozi kuhakikisha wanawapatia wenyeviti wa Mashina wa Chama Cha Mapinduzi taarifa muhimu za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili waweze kuzielezea vyema kwa wananchi.
Waziri Mhagama ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea Wenyeviti wa Mashina katika Kata ya Magagula, Mbingamwalule, Kizuka, Liganga na Litisha zilizopo Jimbo la Peramiho lililopo katika Halmashauri ya Songea Vijijini tarehe 27 Februari, 2024 mkoani Ruvuma.
Ameongeza kwamba, siasa za sasa zinalenga katika kujenga hoja hivyo ni muhimu wenyeviti wa Mashina kuwa na maelezo muhimu yatakayosaidia kukielezea chama vyema kwa wananchi.
"Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM inategemea Mafiga Matatu kwa maana ya Rais, Mbunge na Diwani jambo ambalo linarahisisha katika utekelezaji wa shughuli za serikali na heshima hiyo mnatupatia nyie wenyeviti wa Mashina," alisema.
Aliongezea kuwa, wenyeviti waendelee kuwa na uelewa mzuri wa miradi inayotekelezwa na Serikali kwani itasaidia kusemea chama, na Rais ikiwa ni sambamba na kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo pamoja.
Mwenyekiti wa CCM Songea Vijijini, Thomas Masolwa akizungumza jambo ofisini kwake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini,Menace Komba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Vijijini,Thomas Masolwa amesema ziara ya Mhe. Jenista Mhagama kutembelea Wenyeviti wa Mashina inasaidia kujenga na kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.
Ameongeza kuwa,kuelekea uchaguzi ujao ni vyema Wenyeviti wa Mashina wakajua kwamba Uchaguzi ni hesabu za namba, ukiwa na namba nyingi lazima utakuwa umemshinda mpinzani wako.
"Ni vyema tuhamasishe wananchi waende kukipiga Kura Chama Cha Mapinduzi, tutengeneze wapiga Kura kwa kuhakikisha wanasajiliwa ili watambulike na Chama," alisema.