NCAA yarekodi mafanikio ya namna yake miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Hifadhi Eneo la Ngorongoro (NCAA) imerekodi mafanikio makubwa ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa leo Februari 26, 2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi Eneo la Ngorongoro (NCAA),Richard Rwanyakaato Kiiza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema, Rais Dkt.Samia ameleta mageuzi makubwa ya utangazaji wa utalii na hifadhi kupitia filamu ya The Royal Tour ambayo imeiwezesha mamlaka hiyo kurejesha kwa kasi idadi kubwa ya watalii licha ya changamoto ya UVIKO-19 ambayo iliathiri Sekta ya Utalii duniani.

"Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amekuwa chachu ya mafanikio ya Hifadhi ya Ngorongoro. Juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt.Samia hazikuishia kwenye Royal Tour tu bali kuwezesha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma ndani ya hifadhi."

Amesema, kutokana na juhudi hizo mamlaka hiyo imeendelea kupata idadi kubwa ya watalii na ongezo la mapato yatokanayo na shughuli za utalii hifadhini.

Kiiza amesema, hadi kufikia nusu mwaka wa fedha wa 2023/2024 mamlaka hiyo imeweza kutembelewa na watalii 534,065.

Vile vile, matarajio ya mamlaka ni hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2023/2024 idadi ya wageni watakaotembelea hifadhi hiyo ifikie milioni moja ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita ambapo wageni kwa mwaka nzima walikuwa 752,232.

Pia, wamefanikiwa kuboresha miundombinu ya barabara na huduma nyingine zinazotolewa kwa wageni wakiwa hifadhini humo.

Kiiza amesema, ongezeko hilo la wageni linakwenda sambamba na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ambapo mpaka kufikia nusu ya mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shilingi bilioni 123 tayari zimeshakusanywa.

Aidha, Kiiza amesema, zoezi la kuhama kutoka ndani ya hifadhi hiyo kwa hiyari kuelekea katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga na maeneo mengine linaendelea vizuri.
Ni kutokana na wananchi wengi kuwa na hamasa ya kutaka kuhama hasa ikizingatiwa kuwa mamlaka imeendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuboresha maisha yao nje ya hifadhi hiyo.

"Ukitaka kujua hali halisi ya Ngorongoro usitake kusikiliza katika mitandao ya kijamii, nendeni wenyewe mkajionee."

Pia, amesema katika wale ambao wanahama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera katika wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, kaya inahesabiwa kwa nyumba moja, lakini kwa wale wenye wake wengi hilo Serikali haiwajibiki.

"Tanzania ni nchi yetu sisi sote, popote pale ambapo unapoona taasisi inajaribu kupotosha kuhusu zoezi linaloendelea Ngorongoro ni wajibu wetu kulitolea ufafanuzi."

Msajili wa Hazina

Awali,Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Msajili wa Hazina Thobias Makoba amefafanua kuwa,Ofisi ya Msajili wa Hazina ilianzisha utaratibu wa kukutanisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini na taasisi yakiwemo mashirika ambayo inayasimamia tangu mwaka 2023.
Amesema,lengo la vikao kazi hivyo ni kuzipa nafasi taasisi hizo kuelezea kuhusu utekelezaji wa mambo mbalimbali ambayo wanayatekeleza kwa niaba ya wananchi na mafanikio ambayo wameyapata ili umma ambao ndiyo wamiliki wake waweze kupata mwelekeo wa taasisi zao.

"Kama mashirika hayajulikani na haijulikani yanafanya nini, ni vigumu umma kuweza kupata uelewa juu ya mashirika haya. Hivyo, vikao hivi ni muhimu sana kwa umma kuweza kupata taarifa sahihi na mafanikio ya taasisi hizo.”

Amesema, NCAA ni miongoni mwa mamlaka ambazo zinasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika Sekta ya Utalii nchini, kwani licha ya kuchangia pato la Taifa pia imekuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa Watanzania hususani vijana.

Makoba ameipongeza,NCAA kutokana na kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo hivyo kurahisisha mchakato wa kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi.

Amesema,ofisi hiyo imejipanga vizuri katika kuhakikisha kila Mamlaka iliyo chini yake inafanya vikao vya mara kwa mara na waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya Umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya Sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Ofisi inayojitegemea kimuundo.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) Ofisi ilikabidhiwa majukumu ya Shirika hilo.

Umuhimu wa Ngorongoro

Ngorongoro ina umuhimu mkubwa kutokana na kuwa eneo lenye viumbe hai walio hatarini kupotea, lakini pia ni miongoni mwa mahali penye eneo kubwa la kreta duniani na mabaki ya zamadamu katika eneo la Olduvai Gorge.

Jambo kubwa zaidi mwaka 1979 Ngorongoro iliwekwa kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa Dunia.

Lakini pia ni miongoni mwa maeneo ya kustaajabisha duniani kwa vivutio vyake, kuanzia kuhama kwa makundi ya nyumbu na binadamu kuweza kuishi na wanyama.

Kipindi cha ukoloni, eneo hili lilikuwa la shughuli za uwindaji kwa wakoloni. Mwaka 1928 uwindaji huo ukapigwa marafuku eneo la kreta.

Aidha,Ngorongoro ilikuwa sehemu ya Serengeti hadi mwaka 1959, ambapo palitenganishwa na kupewa hadhi tofauti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news