NHC, PBZ kuwezesha Watanzania kumiliki nyumba mapema

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) na Benki ya PBZ wameingia makubaliano yanayowezesha wateja wao kupata mikopo kwa ajili ya kununua nyumba zenye ubora wa hali ya juu na gharama nafuu.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Februari 7,2024 jijini Dar es Salaam ambapo kwa upande wa NHC wameongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Hamad Abdallah huku PBZ wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Muhsin Salim Masoud.

PBZ inakamilisha jumla ya benki 22 ambazo zinashirikiana na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kutoa mikopo kwa wateja wao ili waweze kununua nyumba za shirika.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah akizungumza katika hafla hiyo amesema, ni hatua muhimu ambayo itawawezesha wateja wa benki hiyo kupata makazi bora hapa nchini.

Amebainisha kuwa, NHC ilianzishwa kwa umuhimu wake nchini hususani kuhakikisha linawezesha upatikanaji wa makazi ambayo ni hitaji muhimu kwa kila binadamu.

"Kila mmoja lazima apate sehemu ya kujibanza na ndiyo sehemu ya kuhifadhi utu wake tofauti na wanyama ambao leo atalala hapa kesho atalala pengine.

"Kwa hiyo kwa sababu hiyo kubwa, Baba wa Taifa katika mashirika ya kwanza kabisa kuyaanzisha Tanzania lilikuwa ni Shirika la Nyumba la Taifa.
"Kwa umuhimu huo, jukumu kubwa ni kuwezesha Watanzania kupata hayo makazi aidha kwa kupanga au kwa kununua.

"Na kwa miaka mingi sana toka Uhuru kuna programu mbalimbali ambazo zimeanzishwa ambazo zilikuwa zikiwawezesha Watanzania kupata makazi.

"Bahati mbaya sana uchumi wa Tanzania miaka ya 1979 wakati tunaingia kwenye vita ya Uganda uchumi wetu ukadorora, uwezo wa nchi kuweza kujenga nyumba kuweza kuwapatia wananchi kwa njia ya mkopo aidha kwa kununua ama kwa kupanga nao vile vile ukapungua sana.

"Tulikuwa tunapata ruzuku toka serikalini nazo zikaondoka ikapelekea shirika kuanza kufanya vibaya."

Amesema, kutokana na changamoto hiyo, mwaka 2010 Serikali iliamua kufanya maboresho makubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC amesema, wakati huo kupitia uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete jukumu kubwa ambalo shirika lilikuwa nalo lilikuwa ni kujenga nyumba na kuziuza.

"Na wakati ule nilikuwa mmoja wa wakurugenzi wa kawaida wa shirika, ambapo tuliingia tukaanza kufanya maboresho ili shirika liweze kufanya vizuri.

"Moja ya jukumu ambalo alisisitiza kwa miaka mingi, shirika lilikuwa linazo zile nyumba ambazo tulikuwa tunajenga na kupangisha.

"Kwa hiyo akatupa maelekezo tuangalie jinsi gani ya kujielekeza katika kujenga nyumba za kuuza, kwa hiyo kuanzia mwaka 2011 tukaanza kujenga nyumba katika maeneo mbalimbali.

"Tukaanza kujenga nyumba takribani 201 katika maeneo mbalimbali nchini."
Amesema, baada ya kujenga nyumba hizo zilivunja rekodi ya kuuzwa kwa saa chache, hatua ambayo iliwapa morali ya kujenga zaidi.

"Na tuliweza kufanya miradi mingi sana na kikubwa ambacho tulikuwa tunakizingatia ni kujenga miradi ambayo ni mizuri, tujitofautishe na waendelezaji wengine ambao wanaangalia faida tu."

Amesema, wao kama shirika wanaangalia ubora wa makazi kwa ajili ya Watanzania na yanayozingatia gharama nafuu.

Amesema, kupitia ushirikiano huo na Benki ya PBZ utawawezesha Watanzania wengi kupata makazi na kuondokana na hadha ya kupanga.

"Ukisema Mtanzania aanze kujenga nyumba yake itamchukua miaka takribani 20, kwa hiyo akianza kufanya kazi mpaka anaelekea kustaafu ndiyo anakuwa anakamilisha nyumba yake.
"Hiyo inakuwa haijamsaidia sana, najua wengi wanapostaafu inawachukua miaka mitatu kuendelea kuwepo duniani.

"Kwa hiyo anafurahia ile nyumba yake kwa miaka michache sana,sasa tunamwezeshaje Mtanzania kuweza kumiliki nyumba aondokane na dhana ya kupanga.

"Kwa sababu ile gharama ya kupanga unaweza kabisa ukamiliki nyumba na baadae kupitia ile mikopo ambayo ulikuwa unaitumia wewe kulipia nyumba ya kupanga ndiyo unaipelea benki ili uweze kununua au kulipia nyumba yako huku ukiwa tayari unaishi humo.

"Kwa hiyo ndani ya miaka 10,15 wewe tayari unaishi nyumba yako, lakini unalipia kidogo kidogo huku ukiwa ndani ya nyumba ambalo ni jambo nzuri sana,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa NHC.

Amesema kuwa,ushirikiano huo na PBZ utawawezesha Watanzania kumiliki nyumba mapema zaidi. "Ni kupitia mikopo ambayo itatolewa na Benki ya PBZ,"amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya PBZ, Dkt. Muhsin Salim Masoud amesema,benki hiyo itawawezesha wateja wake kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kununua nyumba za NHC.

Vile vile amesema, ushirikiano huo ni wa kipekee ikizingatiwa kuwa benki ina matawi Bara na Visiwani hivyo, watakuwa na fursa ya kupata makazi bora na ya kisasa kutoka shirika hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news