Prof.Bisanda:OUT ni chuo kikuu nyumbufu

IRINGA-Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda amesema kwamba, OUT ni Chuo Kikuu nyumbufu kutokana na mifumo yake imara na madhubiti katika kutoa elimu ya juu nchini.
Prof. Bisanda ameeleza hayo Januari 31,2024 wakati akizungumza na walimu wa shule za sekondari wa masomo ya Sayansi na Hisabati wapatao 80 wa Halmashauri ya Wilaya Iringa kwenye kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Mkoa wa Iringa.

Hii ilikuwa ni katika uzunduzi wa mradi wa CL4STEM kwa walimu awamu ya pili ambapo alifafanua unyumbufu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kama ifutavyo:
Mosi: Aliwaeleza walimu hao kwamba OUT ni Chuo Kikuu cha serikali ambacho kimeanzishwa kwa sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka 1992 na kuanza kutoa mafunzo mwaka 1994 na hivyo mwaka huu kimetimiza miaka 30 ya kutoa elimu ya juu kwa njia za Masafa, Huria na Mtandao.

OUT ina vituo nchi nzima katika kila mkoa na vituo vya uratibu Unguja, Pemba, Kahama na Tunduru. Huu ni moja kati ya unyumbufu wa OUT ambapo wanafunzi wanafuatwa na chuo kule walipo wakifanya kazi zao na siyo wao wanafunzi kukifuata chuo.

Pili: Prof. Bisanda amewaeleza walimu hao kwamba OUT ina utaratibu wa kutoa mihadhara kwa njia ya ZOOM ambapo wanafunzi huhudhuria mubashara mihadhara wakiwa popote pale walipo. Huu ni unyumbufu wa OUT ambao huwezi kuupata popote.
Vilevile, ameeleza kwamba matini za kujisomea za mada zote za masomo zimepakiwa kwenye Mfumo wa Ufundishaji na Ujifunzaji Kielektroniki (MOODLE) na mwanafunzi anaweza kuingia na kusoma akiwa mahali popote.

Mfumo huu unapatikana Online na offline kutegemea na mahitaji ya mwanafunzi. Matini za kila mada zimepangiliwa vizuri kulingana na muongozo wa kozi husika.

Mwanafunzi haitaji kuacha shughuli zake na kwenda darasani bali pale anapopata muda anaingia darasani kwa wakati wake. Huu ni unyumbufu wa hali ya juu kabisa unapatikana OUT.
Tatu: Prof. Bisanda amewaeleza walimu kwamba OUT ina mfumo wa Mitihani unaitwa On Demand Examination ambapo mwanafunzi huomba mtihani pale anapokuwa tayari kufanya mtihani.

Ikiwa mwanafunzi amebanwa na majukumu na hawezi kufanya mitihani wakati wa ratiba kuu ya mitihani ipo fursa ya yeye kuomba mtihani wakati wowote.

Mwanafunzi baada ya kukidhi vigezo atafanya mtihani wake. Huu ni unyumbufu wa OUT katika kuwapelekea wananchi huduma kwa ukaribu.
Nne: Prof. Bisanda amewaeleza walimu hao kwamba OUT ina Mahafali yanayoitwa On Demand Graduation ambapo mwanafunzi anayemaliza masomo yake wakati wowote na kupitishwa na Seneti hupatiwa cheti chake wakati huo huo bila kusubiri Mahafali ya kusanyiko la mwisho wa mwaka.

Mwanafunzi huyu anapokuja kwenye Mahafali ya kusanyiko la mwaka anakuja kusherehekea akiwa tayari alishapata cheti chake. Huu ni unyumbufu wa OUT ambao huwezi kuupata popote.

Tano: Prof. Bisanda amewaeleza walimu hao kwamba OUT inadahili wanafunzi katika mihula ya Novemba na Aprili kwa mwaka kwa wanafunzi wa Astashahada, Stashahada na Shahada za kwanza.
Kwa upande wa Stashahada za Uzamili, Umahiri na Uzamivu kuna mihula ya Novemba, Machi na Juni kwa mwaka.

Huu ni unyumbufu wa OUT kwa lengo la kutoa fursa kwa watu wote muda wowote popote pale walipo wajiunge na masomo kupitia OUT.

Sita: Prof. Bisanda amewaeleza walimu hao kwamba mwanafunzi anasoma kulingana na kasi na uwezo wake.

Mwanafunzi hafungwi kwamba ni lazima wote walioanza pamoja wamalize pamoja.

Ni kama mbio za marathoni ambapo wakimbiaji huanza pamoja lakini kila mmoja humaliza kwa muda wake.

Saba: Prof. Bisanda aliendelea kuwaeleza walimu kwamba, OUT ni nyumbufu katika mfumo wake wa ulipaji wa ada amapo mwanafunzi hulipa kwa Units na siyo kwa mkupuo. Hivyo mwanafunzi anaweza kusoma na kuhitimu kwa kulipa kidogo kidogo kabisa.
Mfumo huu wa ulipaji wa ada utaupata OUT pekee kwa sababu wengi wa wanaosoma tayari wana majukumu ya kifamilia na kijamii na hivyo kulipa ada kwa Unit inakuwa rahisi kuliko kulipa kwa mkupuo.

Unyumbufu hapa ni kwamba mwanafunzi analipia units anazoweza na akikamilisha units husika anasajili tena units nyingine analipia mpaka anamaliza units zake zote na kustahili kutunukiwa tuzo yake.

Nane: Prof. Bisanda amewaeleza walimu hao kwamba Maktaba ya OUT ipo mtandaoni ambapo mwanafunzi anaweza kuingia na kujisomea machapisho ya mada za masomo yake akiwa mahali popote huku anaendelea na shughuli zake.

Hii inatoa fursa kwa wanafunzi ambao hawawezi kufika Maktaba kuu ya OUT na maktaba za vituo vya mikoa na uratibu kuingia maktaba wakiwa nyumbani au kazini na kusoma kadri watakavyo. Huu ni unyumbufu na unyambulifu wa OUT.

Sambamba na matumizi ya machapisho ya Maktaba, wanafunzi wa OUT hufundishwa jinsi ya kutafuta na kupakuwa machapisho ya vitabu, makala, tafiti, majarida na nyaraka mbalimbali katika mtandao mpana zaidi nje na maktaba ya chuo.

Hii inawapatia fursa ya kupata maarifa mengi na ujuzi mujarabu na kuwa na mawanda mapana ya kuelewa masomo yao. Hii pia huwajengea uwezo mkubwa wa kujitegemea katika kutatua changamoto mbalimbali katika maisha yao ya kazini na katika familia.

Tisa: Prof. Bisanda amewaeleza walimu kwamba, ikiwa mwanafunzi amebanwa sana na majukumu na kushindwa kuendelea na masomo kwa wakati huo huo anaruhusiwa kupumzika mpaka pale majukumu yatakapopungua na kisha kuendelea na masomo yake.

Hii ndiyo maana wapo wanafunzi wanahitimu masomo yao ya Shahada kwa mfano kwa miaka 3, wengine miaka 4, wengine miaka 5 na wengine miaka 6 kutokana na namna kila mmoja anavyopata fursa kulingana na majukumu yake ya kikazi au familia.

Fursa hii utaipata OUT pekee kwa sababu ni moja kati ya sifa za vyuo Vikuu Huria vyote duniani.

Hizi ni baadhi ya sifa za uyumbufu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambazo Prof. Bisanda amezieleza kwa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Ni matumaini yetu kwamba unyumbufu wa OUT utawavutia watu wengi zaidi kujiunga na masomo ya Elimu ya juu kwa maendeleo ya taifa letu.
Chuo Kikuu Huria chochote duniani kama kile cha Uingereza, China, India, Israel, Nigeria, Afrika Kusini, Pakistani na vingine vingi vina sifa hizi za unyumbufu na nyingine za Juu kabisa ambazo na OUT inaendelea kujipanga ili kuifanya iwe nyumbufu kindakindaki siku za hapo usoni.

Kwa sasa OUT inapokea maombi ya Muhula wa Aprili 2024 kupitia www.out.ac.tz karibuni mnaopenda kujiendeleza mtume maombi yenu mkiwa popote pale nchini na nje ya nchi.

Kwa mawasiliano zaidi tuandikie kupitia nambari 0719017254 au katika namba vituo vya mikoa zinazopatikana kwenye matangazo yetu.

WENU
Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri Mwandamizi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Iringa
31/01/2024

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news