MOROGORO-Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha leo Februari 10,2024 ameongoza jumuiya wa Wanamzumbe katika zoezi la upandaji miti katika eneo la Maekani.
Akizungumza kabla ya zoezi hilo, Prof. Mwegoha amesema Chuo Kikuu Mzumbe kinaunga mkono maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha zoezi la upandaji miti linakuwa endelevu.
"Hili ni zoezi endelevu, tunaunga mkono maelekezo ya Mhe. Rais na leo hii tunapanda miti 3000 katika eneo hili. Tunaendelea kutunza mazingira, sisi kazi yetu kuhakiksha tunalinda bioanuai," amesisitiza Prof. Mwegoha.
Katika kuhakikisha miti iliyopandwa inakuwa na kustawi, Prof. Mwegoha amesema kupitia Kamati ya Mazingira wamejipanga kuwa na usimamizi endelevu na kuhakikisha miti inakuwa.
Awali, Prof. Allen Mushi ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala ametoa rai kwa jamii kuhakikisha wanapanda miti na kuitunza na kuepuka uchomaji holela wa misitu.
"Kupanda miti ni kuhimu sana, Tupande miti na kuitunza, tusichome moto ovyo," amesisitiza Prof. Mushi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wadau walioshiriki katika zoezi hilo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Utafiti na Ushauri Prof. Eliza Mwakasangula amesema azma ya Chuo Kikuu Mzumbe ni kupanda miti takribani elfu ishirini ambayo itapandwa kwa awamu katika eneo la Maekani.