NA DR.MOHAMED OMARY MAGUO
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kinajivunia sana kuimarisha huduma kwa wanachuo wake ambao karibu asilimia 95 ni watu wenye majukumu ya kazi na shughuli za biashara, kilimo na ufugaji, uvuvi, machinga, mama lishe na baba lishe.
Tangu OUT ilipoanzishwa mwaka 1992 na kuanza kutoa mafunzo mwaka 1994 kumekuwa na kuimarika kwa hali ya juu katika kutoa huduma kwa wanafunzi wa ngazi mbalimbali za masomo.
Hayo yamesemwa na Prof. Deus Ngaruko ambaye ni naibu Makamu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayesimamia Taaluma, Utafiti, na Huduma za Ushauri wa Kitaalamu wakati akifunga warsha ya mafunzo ya uandishi wa matini za kufundishia na kujifunzia (Study materials).
Ni kwa wahadhiri wa OUT iliyofanyika jijini Dodoma kwenye kituo cha OUT kuanzia Februari 6 hadi 9, 2024.
"OUT imepiga hatua kubwa sana katika kuimarisha huduma kwa wanachuo na kazi ya mafunzo mliyokuwa nayo kwa siku nne hapa Dodoma ni sehemu ya kuhakikisha huduma kwa wanafunzi zinazidi kuimarika.
"Chuo kilipoanzishwa mwaka 1992 na kuanza kufundisha mwaka 1994 kimeweza kuwa na matini za kujifunzia na kufundishia za aina mbalimbali.
"Tulianza kwa kutumia matini kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, Chuo Kikuu Huria cha Nigeria, Chuo Kikuu cha Afrika ya Kusini na sehemu nyingine.
"Mwanzoni mwa miaka ya 2000 tuliandika matini zetu wenyewe kwa kutumia wataalamu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
"Matini hizo zipo na zinawasaidia sana wanafunzi kujisomea wakiwa mahali popote pale wakiendelea na shughuli zao bila kuziacha," alisema Prof. Ngaruko.
Prof. Ngaruko ameongeza kwamba, OUT ilipiga hatua nyingine kubwa kwa kuingiza matini za kufundishia na kujifunzia kwenye CD ambapo matini za masomo husika ziliwekwa kwenye CD moja na kusambazwa kwa wanafunzi kupitia vituo vyote vya mikoa na uratibu vya OUT nchi nzima.
Hii ilikuwa ni katika kipindi ambapo kompyuta zilianza kuingia nchini.
Baadae katika miaka ya 2007 ukaja mfumo wa Ufundishaji na Ujifunzaji Kielektroniki (MOODLE) ambapo matini za kufundishia na kujifunzia zilianza kupakiwa kwenye mfumo huo na wanafunzi kuweza kujisomea wakiwa wanaendelea na kazi na shughuli zao huko huko walipo.
"Mfumo wa MOODLE umekuja kuendelea kuwasogezea wanachuo huduma karibu zaidi kwa gharama na muda nafuu ambapo wanapata matini za kujisomea zikiwa na sauti,picha, maandishi, video, PowerPoint, vitabu vya marejeleo na maswali ya mjadala.
"Wanafunzi pia wanapata fursa ya kuulizana maswali wao kwa wao na mwalimu akitoa muongozo na usimamizi.
"Wanafunzi wanakutana wao kwa wao na wanafunzi wanakutana na walimu wao hapo hapo kwenye mfumo.
"Hii ni hatua kubwa sana ambayo OUT imefikia katika kuimarisha huduma kwa wanachuo wake na mimi nikiwa hapa OUT tangu mwaka 1998 nilipoajiriwa rasmi nimeyaona maendeleo haya hatua kwa hatua na kwa hakika tunajivunia sana," amesema Prof. Ngaruko.
Kufuatia maendeleo yote haya, Prof. Ngaruko ameipongeza kurugenzi ya Machapisho, Utafiti na Uvumbuzi kwa kazi nzuri ya kuandaa mafunzo haya kwa wahadhiri na kutaka yawe ni mafunzo endelevu kwa wahadhiri wote wa OUT.
Matini zitakazozalishwa kutokana na mafunzo haya zitachapishwa katika nakala ngumu na nakala laini zitapakiwa kwenye mifumo kama ilivyo hivi sasa.
Hii itachagiza ukuzaji wa maarifa na ujuzi kwa wanafunzi wa OUT ambapo pamoja na yote haya kuna mihadhara mubashara kwa njia ya ZOOM.
Wanafunzi wanaingia darasani kila mmoja akiwa huko huko alipo na wanapata fursa ya kumsimiliza mwalimu na kumuuliza maswali.
Awali akitoa mrejesho wa namna mafunzo yalivyofanyika kwa muda wa siku 4, mhadhiri mwandamizi wa OUT, Dkt. Proches Ngatuni ameeleza kwamba, mafunzo yaliyotolewa kwa wahadhiri ni nyenzo muhimu kwa walimu na itawasaidia katika kuandaa matini za kufundishia na kujifunzia zenye ubora wa viwango vya juu.
"Kitendo cha Menejimenti ya OUT kuwezesha mafunzo haya kufanyika ni uwekezaji umefanyika kwetu wahadhiri kwa lengo la kuendelea kuimarisha huduma kwa wanachuo wetu.
"Sisi tuliopata mafunzo haya ni muhimu tukawajibika ipasavyo ili matini zetu ziweze kuchapishwa mapema iwezekanavyo na pia tukatoe mafunzo haya kwa wenzetu kwenye idara zetu ambao hawakupata fursa ya kuja Dodoma kwenye mafunzo tuliyopata sisi.
"Kazi ya kuandaa matini za kufundishia na kujifunzia ni ngumu sana kwani inahitaji muda wa kutosha na rasilimali fedha ili kukamilika kwa ubora madhubiti wa viwango vya juu.
"Tunaishukuru sana Menejimenti ya OUT kwa fursa hii na kamwe hatutawaangusha bali tutatekeleza kazi hii kwa ukamilifu uliolengwa," amesema Dkt. Ngatuni.
Kwa upande wake Prof. Modest Varisanga ambaye ni rais wa Jumuiya ya Wanazuoni wa OUT na Profesa mshiriki katika kitivo cha Sayansi, Teknolojia na Taaluma za Mazingira ameipongeza Menejimenti ya OUT kwa hatua hii kubwa ya kutoa mafunzo ya uandishi wa matini za kufundishia na kujifunzia kwamba yamekuja wakati muafaka kabisa.
"Kwa kweli kuwa na matini za nakala ngumu ni muhimu sana hasa kwa wanafunzi wetu ambao wapo katika maeneo ambayo bado hakuna mtandao wa uhakika na pia hakuna umeme.
"Wanapopata matini zilizochapwa katika muundo wa kitabu na matini hizo zinaelezea mada mbalimbali kama vile mwalimu anavyozungumza na wanafunzi wake ana kwa ana anajisikia faraja lakini kubwa anapata maarifa na ujuzi uliolengwa.
"Hivyo,naipongeza Menejimenti na hapo hapo natoa ombi kwamba kila mwaka kwenye bajeti yake ione namna ya kuweka fedha za kutosha kwa ajili ya kazi hii ya uandishi wa matini za kufundishia na kujifunzia," alihitimisha Prof. Varisanga.
Akizungumza baada ya mafunzo kufungwa, Prof. Raphael Gwahula ambaye ni mratibu wa machapisho katika kurugenzi ya Machapisho, Utafiti na Uvumbuzi amedokeza kwamba, OUT ina sera nzuri sana ya uandishi wa matini za kufundishia na kujifunzia ambayo inaeleza hatua mbalimbali za uandishi pamoja na wajibu na motisha kwa walimu watakaoandika matini hizo.
Prof. Gwahula, amewataka walimu wote wa OUT kuisoma sera hiyo vizuri na kuilewa ili waone fursa zilizopo na kuzitumia. Kuwepo kwa sera hii ni katika azma ile ile ya OUT kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachuo wake.
Hatimaye Dkt. Harrieth Mtae ambaye ni Mkurugenzi wa Machapisho, Utafiti na Uvumbuzi ametoa neno la shukurani kwa naibu Makamu wa Chuo, Prof. Deus Ngaruko kwa kuja kufunga mafunzo haya na kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa.
Pia, amewashukuru washiriki wote wa warsha hiyo wapatao 27 kutoka idara mbalimbali za kitaaluma za OUT kwa kuwa wazingativu na watulivu katika siku zote za mafunzo.
Mwisho, ameishukuru Menejimenti ya OUT kwa ujumla kwa uwezeshaji na pia uongozi wa kituo cha OUT Dodoma wenyeji wa warsha hii kwa mapokezi mazuri katika siku zote za mafunzo.