ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kusainiwa kwa sheria mpya itaondoa changamoto ambazo zilikuwa vikwazo katika kufikia malengo ya kimaendeleo.
Amesema, sheria hizo mpya zinajumuisha ya Mahakama ya Kadhi Zanzibar, Sheria mpya ya Ukaguzi wa Umma, Sheria mpya ya Uwekezaji Zanzibar, ambayo ni sheria bora kwa mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji nchini.
Pia, Sheria ya kuweka masharti ya utoaji leseni udhibiti na usimamizi wa huduma ndogo za fedha kwa ajili ya kudumisha utulivu, usalama na ubora wa huduma hizo.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Februari 1,2024 wakati wa hafla ya utiaji saini wa sheria mpya nne viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema Sheria zilizosainiwa zimepita katika hatua mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa utafiti wa kina na ukusanyaji wa maoni ya wadau Unguja na Pemba kabla ya kuwasiilishwa Baraza la Wawakilishi na kujadiliwa kwa mfumo wa demokrasia shirikishi.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa ni jambo la kihistoria kusainiwa kwa sheria mpya nne hadharani kwa wakati mmoja.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amesema Sheria zote nne zilizosainiwa zinagusa moja kwa moja maslahi ya wananchi na haki zao ikiwemo kuimarisha miongozo ya mifumo jumuishi ya kusimamia shughuli zote za uwekezaji, kupanua wigo wa kazi za ukaguzi ili kufikia ngazi za kitaifa na kimataifa, kubaini na kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma, kukabiliana na vitendo vya rushwa, kuzuia matumizi mabaya ya mifumo inayoathiri utekelezaji wa kazi za ukaguzi.
Rais Dkt.Mwinyi amezitaka taasisi za sheria kufanya mapitio sheria zinazokwaza kasi ya maendeleo katika maeneo ya mafuta na gesi asilia.