DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewapongeza The Ramadhani Brothers kwa kuibuka washindi katika Mashindano ya America’s Got Talent Fantasy League.
Ramadhani Brothers katika America's Got Talent: Fantasy League Episode 102. (Picha na Trae Patton/NBC).
"Pongezi kwa vijana wetu Fadhili na Ibrahim (The Ramadhani Brothers) kwa kuibuka washindi katika mashindano ya sanaa na burudani ya AGT: Fantasy League.
"Safari yenu inaendelea kudhihirisha kuwa juhudi, nidhamu, kujituma na kujiamini ni nguzo muhimu kufikia mafanikio.
"Mnaitangaza vyema nchi yetu na kuweka mfano bora kwa wengine,"amesisitiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Wasanii hao wa sarakasi kutoka Tanzania Ibrahim na Fadhili Ramadhan wanaounda kundi la The Ramadhan Brothers wameibuka washindi wa mashindano ya kusaka vipaji ya America’s Got Talent Fantasy League.
Ni usiku wa kuamkia leo nchini Marekani na kujinyakulia dola za Marekani 250,000 (shilingi milioni 637.5).
Sambamba na tuzo ya kwanza ya msimu huu wa mashindano hayo.
Mashindano ya America’s Got Talent yalianza rasmi mwaka 2006 ambapo dhamira yao kubwa ilikuwa ni kusaka vipaji kwenye nyanja mbalimbali Marekani kabla ya baadaye kupanua wigo na kuvisaka vipaji vya maeneo mbalimbali Duniani.
Kwa mwaka huu 2024 mashindano hayo yamefanyika kwa utofauti kidogo, kutokana na majaji kupewa nafasi ya kuwarudisha washiriki waliopita katika misimu iliyopita kisha kuwapatia nafasi ya kushindanishwa upya ili kuwania kitita cha dola 250,000 pamoja na tuzo.
Aidha,Ramadhani Brothers walishiriki katika mashindano hayo kwa mara ya kwanza mwaka 2023 kwenye msimu wa 18 wa America’s Got Talent wakishika nafasi ya tano.
Vile vile,haya sio mashindano ya kwanza kwa Ramadhani Brothers kushiriki kwenye safu ya kimataifa kwani walishiriki kwenye mashindano nchini Ujerumani, Slovakia, Ufaransa, Australia pamoja na Marekani.(NA)