WINDHOEK-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Februari 23,2024 amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hosea Kutako, Windhoek nchini Namibia kwa ajili ya kuhudhuria maziko ya aliyekuwa Rais wa Namibia Marehemu Dkt. Hage Geingob.
Shughuli za mazishi za Rais huyo Hayati Dkt. Hage Geingob zitafanyika katika Jiji la Windhoek tarehe 24 hadi 25 Februari, 2024 ambapo atazikwa huko Heroes' Acre.
Jumla ya wakuu wa nchi 18 watahudhuria maziko hayo akiwemo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Finland Sauli Niinistö.
Wengine ni, viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Kusini mwa Afrika akiwemo Cyril Ramaposa wa Afrika Kusini na Thabo Mbheki, João Lourenço wa Angola, Mokgweetsi Masisi wa Botswana, Rais wa Kenya William Ruto, na Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, miongoni mwa wengine.
Aidha, nchi 27 zimetuma wajumbe akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Marekani, Deb Haaland na Balozi Randy Berry, Mjumbe Maalum wa China na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China, Jiang Zuojun.
Vile vile Algeria watawakilishwa na Spika wa Bunge la Wananchi wa Algeria, Brahim Boughali.