DAR ES SALAAM-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza maziko ya Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Lowassa yanayotarajiwa kufanyika wilayani Monduli Mkoani Arusha Jumamosi Februari 17, 2024.
Awali Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kuanzia tarehe 10 Februari, 2024.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumapilii, Februari 11, 2024 wakati akitoa taarifa ya ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay, Dar es Salaam.
Amesema,katika kipindi cha siku tano za maombolezo, Taifa litaendelea na shughuli za umma na kijamii sambamba na kushirikiana na wanafamilia katika ratiba ya msiba kama ilivyoandaliwa na kamati ya mazishi ya Kitaifa na wanafamilia.
Amesema,kabla ya mazishi hayo mwili wa Hayati Lowassa unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Amesema,Jumanne Februari 13, 2024 mwili wa Hayati Lowasa unatarajiwa kuangwa na viongozi na wananchi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Jumatano Februari 14 mwili wa Hayari Lowasa utapelekwa katika Kanisa la KKKT Azania Front kwa ajili ya ibada takatifu na kuaga.
Amesema,Alhamisi Februari 15 mwili wa Hayati Lowassa utasafirishwa hadi jijini Arusha ambapo viongozi na wananchi watapa fursa ya kuaga katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.