VATICAN-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Februari 12,2024 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francis mjini Vatican.
Katika mazungumzo ya dakika kumi na tano, viongozi hao wawili waligusia kuhusu majadiliano ya kidini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, Afya, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Ni katika muktadha wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican.
Baadaye, Rais Samia pia amekukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu Mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania.
Pia, mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususani katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii.
Wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii nchini Tanzania,masuala ya kikanda na Kimataifa na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa katika kujikita katika kudumisha amani ulimwenguni.
Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara hii ya kitaifa, alikuwa ameambatana na Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa nchini Tanzania.
Wengine ni Prof. Deogratias Rutatora, Mwenyekiti Halmashauri ya Walei Taifa, Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA, Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar pamoja na Theresia Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa Aprili 19,1968 na Askofu Mkuu Pierluigi Sartorelli akateuliwa kuwa ni Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania, utume alioutekeleza hadi Desemba 22, 1970. (VaticanSwahili)