Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi afariki

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliyefariki dunia leo katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.
Mzee Mwinyi amefariki alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.
Rais Samia ametangaza kifo hicho wakati akilihutubia Taifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari  hivi punde.

Aidha, Rais Samia ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia kesho Ijumaa Machi 1, 2024.

"Ndugu wananchi, kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, ambaye amefariki dunia leo Ijumaa tarehe 29 Februari mwaka 2024 saa 11:30 jioni katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Saratani ya Mapafu. 

"Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa letu. 

"Nchi yetu itakuwa katika kipindi cha siku saba za maombolezo, ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia kesho Machi 1, 2024. Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi atazikwa tarehe 2 Machi 2024 huko Unguja, kisiwani Zanzibar. Inna Lillahi wa inna ilayhi raaji'un."

Alhaj  Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili aliingia madarakani rasmi tarehe 5 Novemba 1985. 

Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi alizaliwa Kivule, Mkuranga,  mkoa wa Pwani  tarehe 5 Mei, 1925. 

Kazi

Alikuwa mwalimu wa shule za msingi za Mangapwani na Bumbwini, Zanzibar.Kisiasa, mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi alijiunga na chama cha Afro Shiraz (ASP) mwaka 1964 na kushika nyadhifa mbali mbali za Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa kazi hizo ni Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Zanzibar 1963, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1970 na kati ya mwaka 1982 hadi 1983 alikuwa Waziri wa Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Maliasili na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Misri. 

Mwaka 1984 alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Elimu

Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi pia ana cheti cha umahiri wa lugha ya kiingereza, alichohitimu katika taasisi ya Regent, Uingereza mwaka 1960 na cheti cha umahiri wa lugha ya kiarabu alichohitimu, Cairo, Misri, mwaka 1972-74.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news