NA LWAGA MWAMBANDE
LEO Februari 29,2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan amelihutubia Taifa kupitia vyombo vya habari kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema kifo hicho kimetokea Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Aidha, Rais Samia ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia kesho Ijumaa Machi 1, 2024.
Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili aliingia madarakani rasmi tarehe 5 Novemba, 1985. Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema,daima tutamkumbuka Mzee Mwinyi.Endelea;
1:Wengine ni baba yetu, wengine ni babu yetu,
Huyu kiongozi wetu, tuliyejaliwa kwetu,
Sasa kaondoka kwetu, yabaki huzuni kwetu,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
2:Myaka kumi Tanzania, urais alishika,
Alifanya yenye nia, nchi yetu kufunguka,
Mengi twamkumbukia, hadi hapa tumefika,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
3:Ile vita na Amini, kwa kweli tulipigika,
Na siasa za zamani, nchi iliharibika,
Mwinyi kushika mpini, kukaanza kufunguka,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
4:Vita kukaza mkanda, karibu ungekatika,
Ilikuwa njia panda, uchumi weze inuka,
Kitini alipopanda, nchi kaanza funguka,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
5:Mageuzi ya uchumi, ujamaa kugeuka,
Uwe ni huru uchumi, watu wakichakarika,
Kwamba mambo hamsomi, ni Mwinyi alihusika,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
6:Changamoto za dunia, na Urusi kumeguka,
Siasa zikaingia, vyama viweze undika,
Mwinyi alisaidia, demokrasi ikafika,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
7:Huyo ni Mzee Ruksa, ndivyo alifahamika,
Alivyotoa fursa, mambo mengi kufanyika,
Ilikuwa ni hamasa, hadi hapa tumefika,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
8:Ndiye alihakikisha, vyama vingi vinafika,
Muda lipokamilisha, akaenda pumzika,
Hekima alizidisha, hadi muda aondoka,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
9:Urithi katuachia, siasa zinafanyika,
Uhuru twafurahia, biashara zafanyika,
Japokuwa tunalia, amempenda Rabuka,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
10:Pole kwa Watanzania msiba umetufika,
Pole na kwa familia, sote tunasikitika,
Pole Rais Samia, baba ndiyo kaondoka,
Rais Mzee Mwinyi, kaondoka twampenda.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602