Rais wa Namibia, Hage Geingob afariki

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Namibia, Hage Geingob amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, ofisi yake imesema, chini ya wiki tatu baada ya kutangazwa kuwa angepata matibabu ya saratani.
Geingob amefariki leo Jumapili katika Hospitali ya Lady Pohamba katika mji mkuu Windhoek akiwa na mkewe na watoto wake pembeni yake, Kaimu Rais Nangolo Mbumba amesema katika taarifa iliyotumwa kwenye ukurasa rasmi wa Facebook wa Geingob.

"Taifa la Namibia limepoteza mtumishi mashuhuri wa watu, mtu wa mapambano ya ukombozi, mbunifu mkuu wa katiba yetu na nguzo ya Namibia.

"Kwa wakati huu wa masikitiko makubwa, natoa rai kwa taifa kuwa watulivu huku Serikali ikiendelea kushughulikia mipango yote muhimu ya serikali, maandalizi na itifaki nyinginezo. Matangazo zaidi kuhusu hili yatatolewa.”

Ofisi ya Geingob ilitangaza mwezi uliopita kwamba alikuwa ameanza matibabu kufuatia ugunduzi wa saratani.

Tangazo hilo halikutoa maelezo ya kina kuhusu ugonjwa au afya ya kiongozi huyo wa Namibia, lakini lilisema ataendelea kutekeleza majukumu yake ya urais.

Ofisi ya Geingob baadaye ilitangaza kwamba angesafiri hadi Marekani kwa ajili ya matibabu na atarejea Namibia Februari 2,2024.

Geingob, ambaye pia alihudumu kwa muda wa miaka 12 kama waziri mkuu, alikuwa na historia ya matatizo ya kiafya, alichaguliwa kuwa rais wa tatu wa Namibia mwaka 2014.

Mnamo 2013, mwanaharakati huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi alifanyiwa upasuaji wa ubongo, na mwaka uliofuata alifichua kwamba alikuwa amepona saratani ya kibofu.

Vile vile, mwaka jana, Geingob alitangaza kuwa amefanyiwa upasuaji wa mshipa katika nchi jirani ya Afrika Kusini.

Namibia, koloni la zamani la Ujerumani ambalo lilipata uhuru kutoka Afrika Kusini mwaka 1990, inatarajiwa kufanya uchaguzi wa rais na bunge mwezi Novemba.

Geingob hakustahili kugombea tena kwa vile katiba ya Namibia inaweka ukomo wa rais kwa mihula miwili zaidi madarakani.

Mgombea urais wa chama tawala cha SWAPO, Nandi-Ndaitwah, atakuwa mkuu wa kwanza mwanamke wa nchi iwapo atachaguliwa. 

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Kaimu Rais wa Namibia,Dkt. Nangolo Mbumba, mke wa Rais, Monica Kalondo, na wananchi wake kufuatia kifo cha Rais wa taifa hilo, Hage Geingob.

“Kwa niaba ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natuma salamu za rambirambi kwa wananchi wa Jamhuri ya Namibia, Kaimu Rais, Mheshimiwa Dk Nangolo Mbumba, Mke wa Rais, Mheshimiwa Monica Kalondo, familia, marafiki na wandugu. katika SWAPO.

“Nimesikitika sana kupata taarifa ya kifo cha Rais wa Namibia, Mheshimiwa Hage Geingo ,ndugu mpendwa, mheshimiwa, Pan Africanist na rafiki mkubwa wa Tanzania,"ameandika Rais Samia.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news