Rais wa Poland awasili Tanzania kwa ziara ya Kitaifa

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Poland, Mheshimiwa Andrzej Duda amewasili nchini kwa ziara ya Kitaifa ya siku mbili.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Duda na mkewe Agata Kornhauser-Duda wamepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Mudrick Soraga na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.

Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais kutoka Poland kutembelea Tanzania tangu kuanza kwa ushirikiano wa uwili kati ya nchi hizi ikilenga kuimarisha ushirikiano katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta za kilimo, kodi, viwanda na biashara, utalii, elimu, usafiri, afya, tiba za mifugo, na maji.
Kwa kupitia ziara hii maeneo mapya ya ushirikiano yataibuliwa kati ya Tanzania na Poland kupitia sekta za ulinzi na usalama, nishati, madini, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea rasmi Rais Duda Ikulu, Dar es salaam Februari 9, 2024 kwa mazungumzo na baadaye watazungumza na waandishi wa habari.
Akiwa nchini, Rais Duda anatarajiwa kutembelea mradi wa matibabu ya dharura katika Hospitali ya Aghakhan, Dar es Salaam kujionea utekelezaji wa mradi huo ambao Serikali ya Poland imetoa msaada wa Dola za Kimarekani milioni 1.136 kufadhili mradi huo wenye lengo la kutoa msaada kwa sekta ya matibabu na kusaidia elimu ya wahudumu wa afya katika mkoa wa Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news