Sera ya Fedha ni msingi wa uchumi wetu-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, mafanikio ya ukuaji wa uchumi hutegemea usimamizi bora unaokwenda sambamba na utekelezaji wa sera mbalimbali nchini.
Sera hizo zinajumuisha, Sera ya Fedha,Sera ya Kibajeti zikiwemo zile za kisekta kama kilimo, biashara, viwanda na nyinginezo.

Hayo yamesemwa leo Februari 14,2024 jijini Zanzibar na Meneja Msaidizi Uchambuzi wa Sera ya Fedha BoT,John Mero wakati akiwasilisha mada ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania,mfumo wa kutumia riba badala ya ujazi wa fedha.

Ni kupitia semina ya siku tatu ambayo imeandaliwa na BoT kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

"Sera hizi za kusimamia uchumi hubadilika kulingana na maendeleo na mahitaji ya uchumi husika.

"Sera ya Fedha hujumuisha maamuzi na hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu ili kupunguza au kuongeza ujazi wa fedha kufikia malengo ya kiuchumi."

Mero amefafanua kuwa,utekelezaji wa Sera ya Fedha unalenga utulivu wa bei za bidhaa na huduma ili kuwezesha shughuli za uchumi kustawi nchini.

"Kwa hiyo, malengo ya Sera ya Fedha ni pamoja na kuhakikisha kiwango cha fedha kilichopo kwenye uchumi kinakidhi mahitaji ya shughuli za uchumi."

Amesema, kiwango kikubwa cha fedha katika mzunguko zaidi ya mahitaji ya shughuli za uchumi hupelekea kuongezeka kwa bei za huduma na bidhaa kwa maana ya mfumuko wa bei.

"Na kiwango kidogo kisichokidhi mahitaji ya shughuli za kiuchumi hupelekea kuzorotesha shughuli za uchumi, na kudumaza ukuaji wa wa uchumi.

"Hivyo, utekelezaji wa Sera ya Fedha unalenga utulivu wa bei za bidhaa na huduma na kuwezesha shughuli za uchumi."

Vile vile amesema kuwa, tafiti zinaonesha chanzo kikubwa cha mfumuko wa bei ni ongezeko la ujazi wa fedha lisiloendana na hali ya shughuli za kiuchumi

“Mfumuko mkubwa wa bei unaathiri uchumi, unapunguza uwezo wa wananchi kununua bidhaa na huduma, hivyo kuathiri hali zao za maisha.

"Na hupunguza uwezo wa akiba waliyo katika kununua bidhaa na huduma, hivyo kupunguza motisha ya kuweka akiba. Hali ambayo huwa inapunguza uwekezaji na kufifisha ukuaji wa uchumi."

Katika hatua nyingine, Mero amebainisha kuwa, kuna mifumo mitatu ya kutekeleza Sera ya Fedha.

Ametaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na unaotumia ujazi wa fedha ambapo Benki Kuu inaweka lengo la ukuaji wa ujazi wa fedha ili kufikia uthabiti wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Pia amesema, ufanisi wa kutekeleza Sera ya Fedha kwa kutumia ujazi wa fedha umekuwa ukipungua kutokana na mabadiliko ya uchumi.

“Imekuwa vigumu kupanga maoteo ya ujazi wa fedha, kasi ya mzunguko wa fedha ukuaji wa fedha unaoendana na mahitaji ya uchumi, kasi isiyotabirika ya mzunguko wa fedha inaonekana pia katika nchi nyingi za Kiafrika,” amesema

Mwingine ni mfumo wa kutumia kiwango cha kubadilisha fedha ya kigeni.

Katika mfumo huu amesema,Benki Kuu huweka malengo ya kiwango cha kubadilisha fedha ya nchi husika dhidi ya fedha ya kigeni ili kufikia malengo ya mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa Uchumi.

Aidha, Mero amebainisha kuwa,katika kufikia malengo hayo, Benki Kuu uuza au kununua fedha za kigeni katika soko.

Akizungumza kuhusu mfumo wa kutumia riba ambao BoT imeanza kuutumia hivi karibuni,Mero amesema Benki Kuu hutoa mwelekeo wa riba itakayotumika katika soko la fedha baina ya mabenki.

"Riba hiyo inajulikana kama Riba ya Benki Kuu. Mabadiliko katika riba hiyo huashiria mwelekeo wa sera ya fedha katika kuhakikisha kuwa ukwasi katika uchumi unaendana na malengo ya kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa uchumi.

"Riba hiyo pia itatumika kama kiashiria kimojawapo katika upangaji wa riba zinazotozwa na mabenki na taasisi nyingine za fedha nchini. Mfumo huu pia hujulikana kama inflation targeting,"amesisitiza Mero.

Mchumi huyo amesema, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kubadili mfumo wa Sera ya Fedha na kuhamia kwenye mfumo unaotumia riba.

Amesema, mfumo utasaidia kuondokana na changamoto zilizopo na kuboresha ufanisi wa Sera ya Fedha katika nchi hizo.

“Benki Kuu nyingi zimeanza kutumia viwango vya riba na kufanikiwa kupata utulivu wa bei kwa muda mrefu, kama ilivyo kwa bei nyingine, viwango vya riba huakisi mabadiliko yasiyotarajiwa katika mahitaji na upatikanaji wa fedha kwa benki za kibiashara.”

Mero amesema,ongezeko la mahitaji ya fedha kwenye benki za biashara kutokana na mavuno makubwa yasiyotarajiwa litasababisha ongezeko la viwango vya riba na hatua za haraka za kuongeza ukwasi zinaweza kuchukuliwa, tofauti na mfumo wa ujazi wa fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news