ZANZIBAR-Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar,Mheshimiwa Rahma Kassim Ali amesema wizara itaupatia ufumbuzi mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kwa wananchi wa Ndunduke ili kuondosha sintofahamu na hatimaye kuwaruhusu wananchi kuendelea na harakati zao.
Mhe. Waziri Rahma Kassim Ali ameeleza hayo wakati alipofika katika eneo hilo la mgogoro liliopo Dole Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mhe. Waziri amezitaka pande zote zilizomo katika mgogoro huo kutotumia nguvu kwani Serikali italipatia ufumbuzi suala hilo ndani ya kipindi cha muda mfupi na kila mmoja atapata haki yake.
Aidha,Mhe. Waziri Rahma ameiagiza Kamisheni ya Ardhi mara baada ya mgogoro huo kupatiwa ufumbuzi kulipima eneo hilo sambamba na kufanya utambuzi mara moja.
Katika kipindi hichi ambacho Wizara inakwenda kuupatia ufumbuzi mgogoro huo amewasisitiza wananchi hao kuendelea kutii agizo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya la kutoendelea na ujenzi wowote katika eneo hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A”,Mhe. Suzan Peter Kunambi ameushukuru uongozi wa Wizara ya Ardhi na Makaazi kwa hatua ilioanza kuzichukua mara baada ya mgogoro huo kufikishwa katika Ofisi ya Mhe. Waziri.
Kwa upande Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndugu Mzee Haji Ali amesema, wizara itaenda kuunda timu ya watu kumi itakayoshirikisha pande zote na kuanza kukaa vikao vyake ili kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.