ZANZIBAR-Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Maalim Moh`d Nassor Salim amesema mchango wa skuli binafsi katika maendeleo ya elimu kisiwani Pemba ni mkubwa na unahitaji kuungwa mkono kwa hali na mali.
Ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Wamiliki wa Skuli Binafsi na taasisi za kukusanya kodi Pemba, wenye lengo la kujadili changamoto za kodi kwa skuli hizo, mkutano ambao umefanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema,wizara hiyo inathamini mchango wa sekta binafsi na kuandaa mikakati ya kutafuta njia bora ya kuondosha vikwazo vinavyozikabili skuli hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Skuli Binafsi Zanzibar Kondo Malik Kondo amesema wizara hiyo imeamua kuwakutanisha wamiliki wa Skuli binafsi na Taasisi za kodi ili waweze kufikisha kilio chao.
Nao maofisa kutoka taasisi zinazokusanya mapato wakiwemo TRA, ZRA wametoa ufafanuzi juu ya kodi mbali mbali ambazo Skuli binafsi zinatakiwa kulipa.