Serikali yakaribisha uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini mkakati

TANGA-Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amewakaribisha wawekezaji wa viwanda vya uzalishaji wa betri za magari ya umeme na vifaa vya kieletroniki kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa Tanzania imebarikiwa na madini mkakati ya kutosha ambayo ni malighafi kuu ya uzalishaji wa bidhaa hizo.
Mhe Mavunde ameyasema hayo leo Kwamsisi, Wilayani Handeni mkoa wa Tanga wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji madini mkakati ya kinywe (Graphite) kinachomilikiwa na Kampuni ya GODMWANGA GEMS LTD.

“Uwekezaji huu unatokana na mazingira mazuri na wezeshi yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Waziri Mavunde.
“Ninampongeza sana Mwekezaji Mtanzania Ndugu God Mwanga kwa kuwa mmoja kati ya wawekezaji wakubwa wa madini kinywe nchini Tanzania na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na upatikanaji wa nafasi za ajira kwa watanzania,” ameongeza Waziri Mavunde.

Ameongeza kwamba mkakati wa Serikali ni kuhakikisha madini hayo yanaongezwa thamani nchini Tanzania ili kutunza ajira za watanzania, kuwajengea uwezo na kukuza uchumi wa taifa kupitia kodi na mapato mbalimbali na hivyo kutumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuongeza thamani madini mkakati kuitumia fursa hiyo kwa kuwa Tanzania imebarikiwa madini mengi na ya kila aina.
Ametumia nafasi hiyo kutoa rai rai kwa uongozi wa mikoa na wilaya kubainisha maeneo maalum ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini kama sehemu ya kuchochea uwekezaji katika eneo hilo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Alberto Msando amesema mkakati mkubwa wa Wilaya hiyo hivi sasa ni kuhakikisha kunakuwepo na nishati ya umeme ya kutosha ili kuongeza uzalishaji katika mgodi huo ambao ni mradi wa thamani ya shilingi bilioni 60 wa ujenzi wa kituo kidogo cha kupoozea umeme ambao utaelekezwa katika maeneo ya uzalishaji ikiwemo viwanda vya uchenjuaji wa madini sambamba na ukarabati wa miundombinu ya barabara.
Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya GODMWANGA GEMS LTD ndugu Godlisten Mwanga amesema ujenzi wa kiwanda hicho ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 800 za madini kinywe kwa siku na utakuwa unaiingizia Serikali zaidi ya Tsh bilioni 1.8 kwa mwezi kama mapato yatokanayo na ada, tozo na mrahaba na hivyo kuwasilisha rasmi maombi Serikalini kuhusu ya upatikanaji wa umeme wa kutosha ili kufikia malengo makuu ya uzalishaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news