Tanzania iko tayari kwa wawekezaji Sekta ya Madini-Dkt.Kiruswa

CAPE TOWN-Sekta ya Madini imezidi kuihakikishia Dunia utayari wa Tanzania kiuwekezaji kutokana na utajiri wa Kijiolojia unaobeba madini ya aina zote ikiwemo Mazingira rafiki kama Sheria, Kanuni na Miundombinu muhimu inayochochea shughuli za madini.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya kimataifa kwenye Mkutano wa Uwekezaji wa Mining Indaba unaoendelea nchini Afrika Kusini katika jiji la Cape Town ambapo kwa mara ya kwanza, Tanzania inashiriki pamoja na Sekta binafsi kupitia Chemba ya Migodi Tanzania.

Ameongeza kuwa, bado Sekta ya madini Tanzania inahitaji wawekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo teknolojia zinazotumika kwenye uchimbaji, shughuli za utafiti wa madini na kusema Tanzania imefanyiwa utafiti wa kina kwa asilimia 16 tu na kwamba bado zipo fursa nyingi kwenye eneo hilo.
Aidha, ameyataja maeneo mengine kuwa ni pamoja na uongezaji thamani madini ambapo amesema eneo hilo pia lina fursa za kutosha kutokana na Sera yaTanzania kusisitiza madini kuongezwa thamani nchini kabla ya kusafirishwa nje kuanzia madini ya vito na mengine ikiwemo madini mkakati.

Aidha, Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, mabadiliko mbalimbali ya kisheria yaliyofanywa kwenye Sekta ya madini yalilenga kuiimarisha Sekta ya Madini na kuhamasisha ushiriki wa watanzania ili pande zote zinufaike.
"Tunawahakikishia wawekezaji usalama, faida, na wakati wote Tanzania iko tayari kuwahudumia na kufanya kazi pamoja. Zipo kampuni kubwa zimewekeza nchini kwenye Sekta ya Madini na pasipo shaka kampuni hizo hazijutii kufanya kazi Tanzania. Mfano mzuri ni mradi wa Kabanga Nikeli ambao unatarajia kuwa mradi mkubwa duniani katika uchimbaji na uchakataji madini mkakati ambayo yanahitajika sana duniani Kwa sasa,’’ amesisitiza Dk.Kiruswa.

Mkutano wa Mining Indaba ni moja ya mikutano mikubwa barani Afrika ambao unawaweka pamoja Serikali kutoka nchi mbalimbali, taasisi binafsi wawekezaji, wafanyabishara, wachimbaji na Wadau wengine yote ikiwa ni kuhakikisha rasilimali madini inazinufaisha nchi hizo. Katika mkutano huo nchi zinapata wasaa wa kushiriki midahalo, kutangaza fursa na kukutana ana kwa ana na wadau wenye nia ya kuwekeza na kupata taarifa za kina kwenye fursa wanazolenga kuwekeza.
Mwaka huu mkutano Indaba umetimiza miaka 30 tangu kuanzisha kwake ambapo umehudhuriwa na washiriki wapatao 8,100, wawekezaji 900, watendaji wakuu wa kampuni za Madini 700, na wakuu wa kampuni ndogo 470.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news