DODOMA-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum amezindua rasmi Kamati ya Kitaifa ya ushauri kuhusu ulinzi na usalama wa mtoto mtandaoni sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Ulinzi na Usalama wa mtoto mtandaoni.
Akizungumza na washiriki waliohudhuria hafla hiyo jijini Dodoma, Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza masuala muhimu kwa Wazazi au Walezi kuzingatia hasa kutimiza wajibu wao wa kulea watoto na kufuatilia kwa usahihi matumizi ya vifaa vya kielektroniki hasa wakati wa likizo ili mtoto kuwa salama mtandaoni.
"Wazazi au Walezi wekeni kiwango cha muda wa matumizi ya vifaa vya kieletroniki hasa luninga ili kukwepa janga la urahibu na kutoa muda kwa mtoto kufanya kazi za nyumbani na kujisomea. Hakikisha mtoto anatumia vifaa vya kielektroniki chini ya uangalizi wa karibu ili kutojiingiza katika mitandao ambayo ni hatari kwa usalama wa Mtoto. "
Aidha, amewaasa wazazi au walezi, kuwaruhusu watoto kushiriki majukwaa yao yaani Mabaraza ya Watoto shuleni na Madawati ya ulinzi wa Watoto ili kujengeana uwezo wa masuala mbalimbali yanayowahusu.
Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kuhusu utafiti uliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la UNICEF mwaka 2022 kwa watoto wa Tanzania wa umri wa miaka 12 hadi 17 ulioonesha asilimia 67 ya watoto wanatumia mitandao na asilimia 4 ya watoto hao walifanyiwa aina tofauti za ukatili kwenye mitandao ikiwa pamoja na kukutana na wahalifu waliowasiliana nao kupitia mitandao.
Aidha, amesema katika kukabiliana na changamoto ya matumizi mabaya ya mtandao kwa watoto, Wizara kwa kushirikiana na Wadau Kamati hiyo ya Taifa ya Ushauri inayojumuisha Wakurugenzi au Wakurugenzi wasaidizi kutoka Serikalini, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Sekta Binafsi pamoja na kikundi kazi cha wataalamu wa uratibu wa utekelezaji wa mpango kazi wa kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa mtandaoni.
Ameongeza pia, kampeni hiyo iliyozinduliwa inahusu kuelimisha watoto wenyewe, wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuhusu kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili ikijumuisha usalama wa mitandaoni ambapo Kaulimbiu itakayoongoza kampeni hii ni Jukumu Letu; Chukua Hatua.
Vilevile Dkt. Gwajima amesema ni muhimu wazazi kuwalea watoto kwa kuwaandaa kukabiliana na mazingira ya kidigitali kwani bila kufanya hivyo inakua rahisi kwa watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili kupitia vifaa hivyo.
“Kazi ya Serikali ni kujenga ufahamu kwa wazazi ili waweze kuelewa kuwa katika ulimwengu wakidigitali inabidi tuingie kwa lengo la maendeleo na si kwa ajili ya kukatiliwa."
Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Kundo Methew amesema uwepo wa teknolojia ya akili bandia ni muhimu kwa maendeleo ya mawasiliano katika Taifa lakini unakuja na changamoto zake ambazo zinahitaji umakini wa hali ya juu katika kuzitatua.
“Wizara ya habari na Mawasiliano itaipa kampeni hiii uzito unaostahili ili kutoa matunda sahihi ikiwemo utungaji wa sera kwa kuwashirikisha wadau wote sambamba na kukidhi mahitaji ya kidigitali kwa wakati tulionao,"amesema Kundo.
Mtaalam wa Usalama Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Kidigitali, Yusuph Kileo amehimiza kila mtumiaji mtandao kufahamu athari zinazo patikana kwenye mitandao sanjari na namna bora ya kujilinda ili kila mtoto atumiapo mitandao aweze kubaki salama
Akifafanua namna kampeni hii itakua suluhu ya changamoto ya udhibiti wa ukatili mtandao dhidi ya watoto ameeleza, Tanzania inapanga pamoja na elimu ya uelewa na kupitiwa kwa sera na sheria, kutakua na udhibiti mahsus kupitia teknolojia ambapo maudhui yasiyo faa kwa mtoto yanazuiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Tanzania, Raphael Charles amewaasa watoto kuhakikisha wanatumia mitandao ya kijamii kwa kufuata miongozo ya wazazi na walezi ili kuepukana na ukatili unaoendelea katika mitandao ya Jamii.
Kampeni iliyo zinduliwa inapangwa kuendeshwa kwa mwaka mmoja kabla ya kufanyiwa tathmini na itaendeshwa kupitia vyombo vya Habari, mitandao ya kijamii pamoja na mashuleni.