Tanzania,China kushirikiana kutangaza utalii

NA HAPPINESS SHAYO

SHIRIKA la Kiserikali la China linalosimamia utangazaji wa utalii na uwekezaji (China Tourism Group-CTG) limeonesha nia ya kutaka kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini Tanzania pamoja na kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya Sekta ya Utalii nchini kwa lengo la kukuza utalii wa Tanzania na kuongeza mapato yatokanayo na sekta hiyo.
Hayo yamesemwa Februari 1,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika kikao kati ya shirika hilo pamoja na Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kilichofanyika jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema Tanzania itanufaika na ushirikiano huo ambapo moja ya kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuvutia watalii wengi kutoka nchi za nje hivyo, Serikali itatumia fursa hiyo kuvutia watalii kutoka soko la China.
Aidha, Mhe. Kairuki ameliomba Shirika hilo kuwekeza katika huduma ya malazi kwa kujenga hoteli, kujenga migahawa ya kichina katika mikoa mbalimbali nchini ili kuchagiza sekta ya utalii nchini.

“Tunatamani shirika la CTG liwe na hoteli hata zaidi ya hamsini nchini Tanzania,” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Pia, Mhe. Kairuki ametumia fursa hiyo kuliomba shirika hilo kushirikiana na Tanzania katika utoaji mafunzo kwa watoa huduma za kitaliii nchini ikiwa ni pamoja na wapishi, kushirikiana na wakala wa safari na kampuni za usafirishaji watalii za China.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa China Tourism Group, Dkt. Luo YANQING amesema lengo la ziara yake nchini Tanzania ni kufanya tafiti ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa hoteli pamoja na kuangalia namna ya kuleta kundi kubwa la watalii wa Kichina nchini.

Lengo ni ili watembelee vivutio na kuitangaza Tanzania kwa kuwa China kila mwaka takribani watalii milioni 170 wanatoka nje ya nchi kutalii ikiwa ni takwimu za mwaka 2019.

Pia ameongeza kuwa, shirika la CTG linaangalia namna ya kukuza utalii wa Tanzania katika soko la China kwa kutumia jukwaa la mtandaoni wa China Tourism Group pamoja na kushirikiana katika kufanya branding ya vivutio vya utalii.

Ameongeza kuwa,CTG inataka kuunganisha wakala wa kampuni za kitalii za China na Tanzania ili zishirikiane katika kuleta watalii na kujua ni aina gani ya huduma watalii wa China wanapenda pindi watakapotembelea nchini.
“Tunaangalia uwezekano wa kusajili kampuni ya utalii kati ya Tanzania na China,” amesisitiza.

Kikao hicho kimehudhuriwa na ugeni kutoka CTG na Watendaji kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) pamoja na wataalamu kuto Idara za Wizara ya Maliasili na Utalii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news