DAR ES SALAAM-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Japan kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia uliodumu kwa miaka 63 kwa maslahi ya pande zote mbili.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) wakati aliposhiriki katika hafla ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa Mfalme wa 126 wa Japan Mhe. Emperor Naruhito ambaye ametimiza miaka 64 tarehe 22 Februari, 2024 jijini Dar es Salaam.
“Wakati tukiadhimisha kumbukizi ya kuzaliwa kwa Mfalme wa 126 wa Japan, pia tunapata fursa ya kusherekea kukua kwa maendeleo ya ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika sekta mbalimbali,” alisema Balozi Mbarouk.
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa kwa miaka mingi Japan imekuwa ikifadhili maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) ambapo maendeleo ya miradi muhimu yameanzishwa.
“Mwaka jana tumeadhimisha miaka 30 ya ushirikiano tangu kuanzishwa kwa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) mwaka 1993.
Ushirikiano wetu umekuza sekta za kilimo, miundombinu, nishati, usafirishaji, afya, elimu kwa ufadhili wa masomo ya muda mfupi na mrefu, pamoja na ufadhili wa miradi 383 ya maendeleo katika sekta ya elimu, afya na maji kwa baadhi ya mikoa ya Tanzania, tunaishukuru Japan kwa jitihada hizo ambazo zimechangia kuongeza maarifa na ujuzi kwenye jamii yetu,” alisema Balozi Mbarouk.
Kadhalika, Balozi Mbarouk ameongeza kuwa biashara kati ya Tanzania na Japan imeendelea kuongezeka kutoka Dola za Kimaraekani milioni 30.9 mwaka 2021 hadi kufika Dola za Kimarekani milioni 89.1 mwaka 2022 na katika kipindi hicho, Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 469 hadi Dola za Kimarekani 521.6, na Kampuni za Japan zilizowekeza nchini Tanzania hadi kufika mwezi Augusti 2023 zimewekeza mtaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani 7.58 na kutoa mamia ya ajira.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini, Mhe. Yasushi Misawa alisema kuwa ushirikiano wa Japan na Tanzania ni wa kihistoria na umekuwa imara wakati wote na Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Tunapoadhimisha siku hii muhimu ya Mfalme wa 126 Mhe. Emperor Naruhito tunakumbuka pia miaka 63 ya uhusiano kati ya Japan na Tanzania. Aidha, Balozi Misawa aliongeza kuwa Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya pande zote mbili,” alisema Balozi Misawa.
Balozi Misawa aliongeza kuwa hivi karibuni Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) imesaidia kufadhili baadhi ya miradi ya maendelo nchini Tanzania ikiwemo ujenzi wa barabara ya juu ya Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara ya Tanzara, ujezi wa barabara mpya ya Bagamoyo na daraja la Gerezani.
JICA pia imefadhili ujezi wa barabara ya Iringa – Shinyanga pamoja na miradi mingine mingi ikiwemo ya kujenga kituo cha kupoozea umeme cha Kinyerezi II.
Kadhalika, Balozi Misiwa ameongeza kuwa tangu mwaka 1989 Japan imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar ambapo miradi 400 yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 30 imetekelezwa. Mwaka 2023 Ubalozi wa Japan ulikubali kufadhili shule nne za Sekondari na Msingi katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Zanzibar.
Tanzania na Japan zinashirikiana katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya, biashara, viwanda, uwekezaji na utalii ambapo kwa pamoja zimekubaliana kuendeleza ushirikiano huo ili kuleta tija katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi wa pande zote mbili.