NA BEATUS MAGANJA
MKUU wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Mhe. Christopher Emil Ngubiagal amesema,Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ni taasisi iliyoleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Utalii na kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali
Sambamba na wazawa wa wilaya hiyo kutokana na maboresho ya miundombinu ya utalii katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara yanayopelekea watalii wengi kutembelea Hifadhi hiyo.



Mhe. Christopher amesema, awali kabla ya ujio wa TAWA wakazi wa wilaya yake pamoja na watalii walikuwa wakipata adha ya kufika Kilwa kisiwani kutokana na uduni wa miundombinu lakini baada ya kuingia TAWA walipeleka boti za Kisasa ambazo zinawafanya watalii na wazawa hao kufika hifadhini kwa raha mstarehe.
Aidha,amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza soko la utalii aliposhiriki filamu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeleta mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea.
Naye Said Amri Said mkazi wa Kilwa kisiwani amekiri kuwa ujio wa TAWA katika Hifadhi hiyo umechangia kuongeza idadi ya watalii ambapo kupitia wageni hao wakazi wa eneo hilo wananufaika kiuchumi kwa kufanya biashara ndogo ndogo ambazo zinawaingizia kipato.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja ametoa wito kwa wakazi wa wilaya ya hiyo kutumia fursa ya ujio wa Meli za watalii kujiongezea kipato kwa kuuza bidhaa pendwa kwa wageni kama vile vitu mbalimbali vya asili na kiutamaduni.