DAR ES SALAAM-Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo nchini.
Hayo yamebainishwa leo Februari 22, 2024 jijini Dar es Salaam na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TM) kupitia taarifa ya utabiri wa Masika 2024.
"Magonjwa kama vile ukungu (fungus) yanatajariwa kuongezeka na kuathiri mazao kama nyanya, ufuta, maharage na mazao jamii ya mizizi.
"Hata hivyo, shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika maeneo mengi."
Kwa mujibu wa TMA,wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati.
Pia, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba, na kuchagua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu huu wa masika.
Aidha, wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya kilimo hususani maeneo ya mabondeni pamoja na kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Vile vile, wauzaji na wasambazaji wa pembejeo za kilimo wanashauriwa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati.
Kwa mujibu wa TMA,kwa ujumla mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Aidha,ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Machi, 2024 katika maeneo hayo.
"Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, na Mara) pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo).
"Mvua za masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma."
Vile vile,mvua za nje ya msimu zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuungana na mvua za Masika 2024.
TMA imebainisha kuwa,mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2024.
Wakati huo huo, kwa upande wa Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, TMA imebainisha kuwa,mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini.
"Mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Februari, 2024 na kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2024."
Kwa upande waNyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani na zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Februari, 2024.
"Mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Mei, 2024,"imeeleza taarifa hiyo ya TMA.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Mazao Shambani
TMA
TMA Tanzania
Wakulima Tanzania