ZANZIBAR-Makongamano ya wadau yanayoendelea nchini kuhusu marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 yanalenga kukusanya maoni yatakayosaidia kutengeneza Sera ya Mambo ya Nje Bora itakayoongoza ushirikiano wenye tija baina ya Tanzania na nchi nyingine, mashirika ya kikanda na kimataifa.
Hayo yamesemwa leo Februari 10, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu - Zamzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir wakati akisoma hotuba ya ufunguzi ya Kongamano la nne la wadau lililofanyika kisiwani Pemba.
Makongamano hayo yanayoratibiwa kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ofisi ya Rais-Zanzibar na Taasisi ya Uongozi yametajwa kuwa ni kielelezo cha utawala bora ambao unahimiza ushirikishwaji wa wananchi katika utengenezaji wa Sera za Taifa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) amesisitiza umuhimu wa wananchi walioshiriki kongamano hilo kutoa maoni yao kwa uhuru bila woga. Alisema maoni yao yatasaidia kutengeneza Sera ya Mambo ya Nje madhubuti itakayoifanya Tanzania kutetea maslahi yake katika majukwaa ya Kimataifa na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika dunia ya sasa.
Alisema mijadala yao ya kurekebisha Sera ya Mambo ya Nje itatoa mwelekeo wa kuboresha maeneo mapya yanayopendekezwa ambayo ni pamoja na masuala ya uchumi wa Buluu, diaspora, mabadiliko ya tabianchi, kubidhaisha Lugha ya Kiswahili na kulinda mila na desturi za Tanzania.

