TUGHE yaipongeza Serikali kwa kukubali ombi lake kuanza kulipa posho ya madaraka

DODOMA-Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimefurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kuanza kulipa Posho ya Madaraka kwa Waganga Wafawidhi katika Vituo vya kutolea huduma za Afya ngazi ya msingi kama ilivyotangazwa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu (MB) jana tarehe 14 Februari 2024 Jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wafawidhi wa Vituo vya kutolea huduma ya Afya ngazi ya msingi.
Akitoa pongezi hizo, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Cde. Hery Mkunda ameeleza kuwa, kwa muda mrefu Chama cha TUGHE kimekuwa kikiwasilisha Serikalini hoja hii ya Posho ya Madaraka kwa Waganga Wafawidhi katika vituo vya kutolea huduma ya Afya na kurejea kurejea Barua ya tarehe 05/10/2023 iliyoandikwa na Ofisi ya Katibu Mkuu TUGHE kwenda Ofisi ya Rais -TAMISEMI) iliyokuwa na kichwa cha Habari (“Kuwasilisha Hoja na Changamoto za Watumishi wa Sekta ya Afya) ambayo ilieleza pia hoja hii hivyo TUGHE imefurahishwa sana na uamuzi huo na kuipongeza Serikali kwa kukubali kuanza kulipa Posho hii kwa wataalamu hao muhimu kuanzia Julai 2024.
“Bado tunaendelea kuikumbusha Serikali kuendelea kushughulikia changamoto nyingine ambazo bado Watumishi wanakumbana nazo kama vile kama vile ajira za mikataba kwa baadhi ya Watumishi wa Umma, Nyongeza ya posho ya kuitwa kazini “On-call allowances” pamoja na changamoto ya Malipo ya nauli za likizo kwa Watumishi wasio Walimu katika Halmashauri za Wilaya kulipwa toka katika mapato ya ndani ya Halmashauri badala ya kulipwa moja kwa moja toka hazina kama ilivyo kwa waalimu, Changamoto za kutokamilika kwa Muundo wa Watumishi wa Mahakama,” alisema Katibu Mkuu TUGHE.

Aidha, TUGHE imeendelea na majadiliano na wadau katika kuhakikisha Mama wanaojifungua Watoto njiti wanaongezewa siku zaidi za likizo ya uzazi. 

Sambamba na hayo pia Chama kitaendelea kuwasilisha mapendekezo mbalimbali Serikalini yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi ili kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini ili kuongeza tija na uzalishaji katika maeneo ya kazi.

Imetolewa na
IDARA YA HABARI NA UHUSIANO KWA UMMA TUGHE

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news