DAR ES SALAAM-Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeandaa kikao cha mashauriano na wadau kuhusu Sheria ya Kimataifa ya Shirika la Miliki Ubunifu (World Intellectual Property (WIPO) itakayolinda Miliki Ubunifu katika Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi kilichofanyika mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema kuwa mashauriano hayo yanalenga kujadili na kuona namna bora nchi itakavyoweza kunufaika na sheria hiyo ya Kimataifa ambayo ikikamilika italeta manufaa kwa nchi na jamii za kijadi kupitia miliki ubunifu zitakazotokana na rasilimali hizo.
Amesema kuwa, katika Ulimwenguni huu wa Sayansi na Teknolojia ni vyema bunifu zinazotokana na Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi zikawaletea manufaa wamiliki hasa jamii ambazo rasilimali na ujuzi huo unapatikana.
Hivyo Sheria ya Kimataifa kuhusu Ulinzi wa Rasiliamli hizo imekuja kwa muda muafaka ili kuzuia matumizi yasiyo halali ya Rasilimali hizo kwa kuweka uwazi na kuwaletea faida wahusika.

"Tunatambua kuwa Taifa letu limejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za kijenetiki zitokanazo na Mimea, wanyama na ujuzi wa jadi ambavyo vina thamani ambayo wengi hawafahamu na mara nyingine rasilimali hizo kutumiwa na watu wengine pasipo kuwaletea manufaa wahusika.
"Kwa sasa tumejipanga kusaidia wabunifu waweze kulinda bunifu zao na baada ya ulinzi wafaidike na bunifu hizo, na matumizi ya rasilimali hizi yawe na faida kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla," amedokeza Bw. Nyaisa.



Kwa kuhitimisha amesema kuwa, majadiliano ya Sheria hiyo yatazaa Itifaki ambayo itakamishwa Mwezi Mei 2024 katika mkutano wa kidplomasia utakaofanyika makao makuu ya WIPO Jijini Geneva, Uswisi.