Tutamuenzi daima Lowassa-Dkt.Mpango

DAR ES SALAAM-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaongoza viongozi na wananchi katika kutoa heshima za mwisho kwa Waziri Mkuu mstaafu, Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais ametoa pole kwa familia, ndugu, marafiki pamoja na watanzania wote kwa ujumla kufuatia msiba huo mkubwa kwa Taifa.

Makamu wa Rais amesema, serikali inathamini uzalendo na mchango mkubwa aliyoutoa Hayati Edward Lowassa katika maendeleo ya nchi kwa kuwa alijitolea kwa dhati kulitumikia Taifa pamoja na kutumia vema karama alizojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia Watanzania katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika. 

Amesema, ni muhimu kila mmoja mtanzania kujikumbusha wajibu aliyonao kwa taifa na kuyaishi kwa vitendo mambo yote mazuri yanayotokana na maisha ya hayati Lowassa.

Amesema ni vema Watanzania kumuenzi hayati Lowassa kwa kuendelea kuchapa kazi ili kuboresha maisha na hivyo kuchangia katika ujenzi wa Taifa kwa kuwa alikuwa mchapa kazi hodari katika utumishi wa umma na katika shughuli zake binafsi ikiwemo ufugaji.

Aidha,Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania wote na hususan vijana kumuenzi hayati Lowassa kwa kutumia fursa mbalimbali kujipatia elimu kwa manufaa ya Taifa kwa kuwa alikua kinara katika elimu na kusimamia kwa uhodari utekelezaji wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ya elimu hususan ujenzi wa shule za Sekondari kila Kata.

Makamu wa Rais amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa mwanamazingira hodari ambapo katika wadhifa wake wa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Makamu wa Rais na alipokuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihimiza sana uhifadhi na Utunzaji wa mazingira. Aliongoza kampeni nyingi za upandaji miti na usafi wa mazingira.

Amesema mchango wake huo uwakumbushe watanzania wote wajibu wa msingi wa kulinda na kutunza mazingira na hususan vyanzo vya maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaendelea kuleta madhara mengi katika Taifa na dunia kwa ujumla.

Vilevile Makamu wa Rais amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa na bidii katika kumwabudu Mwenyezi Mungu akiwa msharika mzuri, akisali mara nyingi katika kanisa la KKKT Azania Front.

Amesema mfano huo ikumbushe kuwa kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa na msingi wa mafanikio katika familia na katika utumishi wa umma.

Makamu wa Rais amewasihi watanzania kutumia msiba huo kudumisha na kuimarisha upendo, amani na mshikamano wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news