Ujumbe wa Tanzania wakutana na Chemba ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Thailand

BANGKOK-Ujumbe wa Tanzania hivi karibuni ulikutana na Jumuiya ya Chemba ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Thailand wanaoishi nchini humo ambao wanajihusisha na biashara za aina mbalimbali.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo pia ni Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini humo Mhe. Florian Rwehumbiza.

Katika kikao cha pamoja, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo aliwakaribisha wafanyabiashara hao kujifunza kuhusu Sekta ya Madini Tanzania pamoja na kuangalia fursa za kibishara zilizopo katika Sekta ya Madini nchini.

Pia, Mbibo alitumia kikao hicho kuwaeleza kuhusu mikakati ya Serikali kuendeleza Sekta ya Madini pamoja na malengo ya ujumbe wa Tanzania nchini humo.
‘’Tulipofika katika Wizara ya Viwanda na Madini ya Thailand tuliona kwamba nchi hii inaagiza kwa wingi makaa ya mawe kutoka nje. Sisi tuna akiba ya kutosha ya makaa ya mawe.

"Niombe muwajulishe wanachama wenu kuhusu suala hilo. Lakini si tu katika makaa ya mawe tunayo madini mkakati ya aina nyingi ukiacha madini ya vito,’’ alisema Mbibo.
Kwa upande mwingine, jumuiya hiyo iliomba kukutana na ujumbe wa Tanzania ili kuona namna ambavyo inaweza kushirikiana kibiashara na Sekta ya Madini nchini ambapo kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Madini.

Aidha, ujumbe huo uliomba kupata mialiko katika masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya madini na kueleza kuwa pindi Wizara inapofanya ziara au shughuli mbalimbali za kisekta nchini humo wameomba kujulishwa waweze kusaidia uratibu wa masuala mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Mbibo alipata wasaa wa kutembelea mabanda ya wafanyabiashara na wachimbaji kutoka Tanzania wanaoshiriki katika Maonesho ya 69 ya Kimataifa ya Vito na Usonara yanayoendelea nchini humo.
Aliwapongeza wafanyabiashara hao kwa kuleta madini yao katika soko hilo la kimataifa, kutumia fursa ya kutangaza bidhaa zao na kupeperusha bendera ya Tanzania.

Mbali na mabanda ya Watanzania, pia, alitembelea mabanda mbalimbali pamoja na banda la Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mji wa Chanthaburi maarufu kwa shughuli za uongezaji thamani madini ya vito na biashara ya vito.
Vilevile, alitembelea banda la PRANDA, Kampuni kubwa inayomiliki kiwanda kikubwa cha uongezaji thamani Madini nchini humo ambacho pia, kinatengeneza bidhaa za mapambo ya vito vya thamani kubwa.
Kiwanda hicho kimetoa nafasi kwa vijana wawili wawili wa kitanzania kufundishwa shughuli za uongezaji thamani madini ya vito kiwandani hapo kila mwaka wa mafunzo wa kiwanda hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news