DAR ES SALAAM-Watalaam wa upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na wenzao kutoka nchini Marekani wamekamilisha kambi maalum ya siku tano iliyohusisha upasuaji wa urembo na upasuaji wa matibabu (Cosmetic and Reconstructive Surgery) kwa wagonjwa nane.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo na kwa niaba ya timu nzima iliyoshiriki, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa MNH, Dkt. Ibrahim Mkoma, amesema upasuaji uliofanyika ni wa matibabu kwa wagonjwa waliokuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo waliopata ajali ya kuungua moto na wenye misuli iliyokakamaa kutokana na majeraha n.k.
Amesema, kuna mtoto ambaye kichwa chake kilizaliwa kikiwa na vinundu vidogo vidogo mithili ya visunzua (skin tag) ambavyo viliondolewa na kufanya sehemu kubwa ya kichwa chake kuwa na kipara.
Hivyo,amefanyiwa upasuaji wa kuwekewa puto (tissue expander) kwenye kichwa sehemu yenye nywele karibu na kipara ili ngozi ya eneo hilo iweze kuongezeka na kukuza nywele ambazo baada ya mwezi mmoja zitakuwa zimeota sehemu kubwa na kuruhusu kufanyiwa upasuaji wa kuvuta ngozi hiyo ikiwa na nywele na kufunika sehemu yenye kipara hivyo kumwezesha mtoto huyo kurudi katika hali yake ya kawaida.