Usiyoyafahamu kuhusu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)

NA GODFREY NNKO

"Ukitaka kujua hali halisi ya Ngorongoro usitake kusikiliza katika mitandao ya kijamii, nendeni wenyewe mkajionee."
Hii ni moja wapo ya nukuu yenye tafakari nzito kutoka kwa Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi Eneo la Ngorongoro (NCAA), Richard Rwanyakaato Kiiza kuhusu Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area) ambayo ina hadhi na heshima ya kipekee duniani.

Lakini kutokana na ongezeko kubwa la watu na mifugo, hifadhi hiyo, bila juhudi na jitihada za Serikali katika kuiokoa na kuendelea kuipa hadhi yake.

Pengine kuna siku isiyofahamika ambayo badala ya kukutana na wanyamapori ambao ni kivutio cha utalii hususani nyati, simba, fisi, chui, viboko, nyumbu, pundamilia, vifaru na wengineno. Kuna siku ambayo ungefika katika hifadhi hiyo ukakutana na ng'ombe, kondoo na mbuzi.

Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi Eneo la Ngorongoro (NCAA), Richard Rwanyakaato Kiiza ameyabainisha hayo Februari 26, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Ni wakati akitoa taarifa za utekelezaji za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ambaye aliingia madarakani Machi 19, 2021.

Vile vile Kiiza alichukua nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt.Samia kwa imani aliyonesha kwake na kumteua ili kwenda kuisimamia mamlaka hiyo.

“Nipende kumhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba nitatumia nguvu zangu zote katika kuhakikisha Ngorongoro inaendelea kuimarika katika kulinda maliasili na malikale zilizopo na kuwa kivutio kikubwa cha utalii duniani, hivyo kuliingizia Taifa letu fedha nyingi za kigeni."

Amesema, Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ilianzishwa kwa Sheria Na.413 ya mwaka 1959 kwa kuigawa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Hifadhi hii ina ukubwa wa kilomita za mraba 8,292 na ilianzishwa kwa ajili ya matumizi mseto ya ardhi, ambapo mambo matatu yanafanyika kwa pamoja ndani ya hifadhi.
“Suala la kwanza ni kuendeleza uhifadhi wa maliasili na malikale,kusimamia maendeleo ya jamii za watu wanaoishi ndani ya mamlaka kwa maana ya Wahadzabe, Wamasai na Wakatoga.”

Pia, amesema hifadhi hiyo ina hadhi tatu ambazo zinatambuliwa na Shirika la Elimu na Sayansi la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ikijumuisha Man and the Biosphere Reserve ya mwaka 1981, Mixed
World Heritage Site na Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark.

“Pamoja na hadhi hizi tatu, mwaka 2023 Hifadhi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilichaguliwa na Mtandao wa World Travels Award kama kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka huo."

Kiiza anabainisha kuwa, wakati Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro inaanzishwa mwaka 1959 ilikuwa na wananchi wasiozidi 8,000 kwa maana ya wananchi 4,000 waliokuwa ndani ya mamlaka upande wa Ngorongoro na wananchi 4,000 waliohamishwa kutoka Hifadhi ya Serengeti.

“Pia, inakadiriwa idadi ya mifugo wakati huo ilikuwa ni mifugo isiyozidi 261,000. Hali hiyo ni tofauti na miaka ya hivi karibuni ambapo kwa mujibu wa takwimu kutoka Taasisi ya Takwimu (NBS) wananchi katika Tarafa ya Ngorongoro wameongezeka kutoka 8,000 mwaka 1959 hadi kufikia zaidi ya watu laki moja, mifugo imeongezeka kutoka mifugo 261,000 hadi zaidi ya mifugo laki nane na hamsini."

Kiiza anafafanua kuwa, ongezeko hili la watu na mifugo limekuwa changamoto kwa zaidi ya miaka 60 toka kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na mwingiliano wa shughuli za uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii ya watu wanaoishi ndani ya hifadhi.

"Ili kuinusuru Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Serikali baada ya kupitia tafiti mbalimbali zilizofanywa na watafiti mbalimbali zote zikihusu matumizi mseto ya ardhi ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na athari zake kwa ustawi wa mamlaka.
"Pamoja na jamii ya wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi, Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua uamuzi wa busara wa kuwaelimisha wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kuhama wao wenyewe kwa hiari kwenda maeneo mengine yaliyotengwa na Serikali.

"Pamoja na sehemu nyingine wanazochagua wao wenyewe kwa ajili ya kupisha uhifadhi pamoja na kuboresha maisha yao, maeneo mahususi yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya wananchi kuhamia ni pamoja na Kijiji cha Msomera kilichopo katika Wilaya ya Handeni, Saunyi Wilaya ya Kilindi na Kitwai B Wilaya ya Simanjiro.

"Zoezi la kuhamisha kwa hiari wananchi wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro awamu ya kwanza lilianza rasmi mwezi Juni, 2021 kwa kujenga nyumba 503 pamoja na huduma zingine za kijamii kama vile shule, miundombinu ya maji, zahanati,

"Barabara, mawasiliano, umeme, majosho, mabwawa, maeneo ya malisho na huduma ya Posta. Hadi kufikia mwezi Januari, 2023 wakati zoezi awamu ya kwanza linakamilika kaya zipatazo 551 zenye watu 3,010 na mifugo 15,521 walihamia katika Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni.

"Awamu ya pili ya zoezi hili ilianza mwezi Julai, 2023 kwa mpango wa kujenga nyumba 5,000 katika vijiji vya Msomera Wilaya ya Handeni nyumba 2,500, Saunyi Wilaya ya Kilindi nyumba 1000 na Kitwai B Wilaya ya Simanjiro nyumba1500.

"Hadi kufikia Februari 25,2024 jumla ya kaya ambazo zimeshahama kwa hiari kutoka ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni kaya 1,042 zenye watu watu 6,461 na mifugo ipatayo 29,919 idadi hii ya watu na mifugo ni kwa awamu zote mbili ya kwanza na ya pili,"amefafanua kwa kina Kamishina wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro,

Mafaniko ya NCAA

Kamishna Kiiza anabainisha kuwa,Novemba, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia alifanya ziara ya kikazi nchini China.

Anabainisha kuwa, katika ziara hiyo Tanzania ilifanikiwa kupata kiasi cha shilingi bilioni 25 kwa ajili ya kuendeleza Ngorongoro Lengai UNESCO Geopark.

Sambamba na miundombinu mingine ya utalii ikiwemo nyumba ya makumbusho itakayojegwa katika lango kuu la kuingilia Ngorongoro.

Pia, Kiiza amesema, mamlaka imeweza kudhibiti matukio ya ujangili wa wanyamapori katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Kamishna huyo anafafanua kuwa,katika kipindi husika mamlaka imeweza kudhibiti matukio ya ujangili wa tembo kutoka matukio 25 mwaka 2020/2021 hadi tukio moja mwaka 2022/2023.

“Hii imewezekana kutokana na Serikali kuiwezesha mamlaka kununua magari ya doria na vitendea kazi vingine.

"Aidha, katika kipindi husika mamlaka kwa kushirikiana na vikosi vya kupambana na ujangili ilifanikiwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola watuhumiwa 175 wanaojihusisha na vitendo vya ujangili."

Hadhi

Kamishna huyo amefafanua kuwa, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeendelea kusimamia na kudumisha hadhi yake ya Kimataifa kwa kutambuliwa kama eneo lenye urithi mchanganyiko wa maliasili na malikale.

Sambamba na uwepo wa miamba na sura za nchi zinazoelezea jinsi Dunia ilivyojiumba na kuwa moja ya maajabu saba ya Dunia.

NCAA na jamii

"Katika kuhakikisha kuwa jamii zilizo ndani ya Mamlaka ya Ngorongoro na zile za jirani zinaongeza kipato, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikitekeleza mradi wa nyuki kwa kusudio la kuboresha uhifadhi na kuongeza kipato hivyo kufanya pande zote (NCAA na jamii jirani) kunufaika.

"Mradi huu umetekelezwa katika wilaya za Ngorongoro tarafa ya Ngorongoro, Karatu,Monduli na Meatu ambapo hadi kufikia 2024 jumla ya vikundi 123 vilikuwa vimenufaika, 68 wilaya ya Ngorongoro,29 karatu,18 Meatu na 8 Monduli.

"Vikundi hivi vimenufaika na mafunzo na kupatiwa vitendea kazi. Jumla ya mizinga 2,476 imekwishatolewa kwa kipindi cha miaka mitatu (2021-2024)."

Kamishna Kiiza anasema kuwa,kuna jumla ya wanavikundi 725 Karatu,455 Meatu na 125 Monduli walipatiwa mafunzo ya mbinu mahiri za ufugaji nyuki.

Aidha, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeweza kutoa visigina asali 12 kwa vikundi 12 ambapo vitano zimekwenda Meatu, vitano Karatu na viwili Monduli.

"Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikigawa unga,sukari na siagi kwa ajili ya uji kwa shule 27 za msingi zilizomo ndani Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

"Kati ya mwaka 2021 na 2024 jumla ya kilo za unga 32,620, kilo za sukari 11,350 na kilo 3,100 za siagi ziligawiwa kwa shule hizo.

Vile vile, katika kuboresha ustawi wa maisha ya wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro,Kamishna Kiiza anasema, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikinunua na kugawa mahindi kwa bei yenye punguzo kwa wenyeji ambapo mpaka kufikia Januari mwaka 2024 tani 600 zilikuwa zimegawiwa kwa wakazi wainaoshi ndani ya hifadhi.

"Katika kuhakikisha siha njema kwa mifugo ya wenyeji wa eneo la Ngorongoro, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikigawa madini chumvi katika vijiji vitano vya wafugaji mifugo ambavyo ni Kayapus, Olorobi, Mokilal, Misigiyo na Irekepusi."

Kamishna Kiiza anabainisha kuwa, mpaka kufikia Januari, 2024 jumla ya kilo 2,000 ziligawiwa kwa wafugaji katika vijiji vitano.

Rais Dkt.Samia

Wakati huo huo, Kamishna Kiiza anabainisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa chachu ya maendeleo ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hasa kutokana na kushiriki kwake katika filamu ya Tanzania ya The Royal Tour.
Amesema, kupitia filamu hiyo,imesaidia kwa asilimia kubwa kuongeza idadi ya watalii ndani ya hifadhi hiyo iliyopo Kaskazini mwa nchini.

"Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimwa Dkt.Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi cha shilingi bilioni 66 kwa ajili ya kujenga tabaka gumu kipande cha barabara chenye kilomita 29.5.

"Ni kutoka lango kuu la kuingilia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hadi Seneto, nia ya Serikali ni kuweka tabaka gumu kipande chote cha kiliomita 83 za barabara ya kuanzia lango kuu (Lodoare gate) hadi mpaka wa Hifadhi ya Serengeti."

Kamishna Kiiza anasema, pamoja na kuitangaza nchi yetu kupitia filamu maarufu ya The Royal Tour na hivyo kuongeza idadi ya wageni waliotembelea Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Mhe.Rais Dkt.Samia alitoa fedha za Uviko-19 shilingi 6,645,258,276 kwa mamlaka.

Amesema, fedha hizo zilitumika kuimarisha miundombinu ya barabara na kununua mitambo pamoja magari makubwa ya kutengenezea barabara, kuimarisha viwanja vya ndege na miundombinu mingine ya utalii ili wageni waweze kufikia vivutio vya utalii kwa urahisi.
Nyingine ni kwa ajili ya kuimarisha huduma za mawasilisano ya simu na inataneti ikiwemo kuhakikisha kuwa utoaji wa huduma kwa wageni unakuwa wa haraka na wa Kimataifa.

Watalii wengi

Kamisha Kiiza amesema, kutokana na juhudi hizo za Mheshimiwa Rais Dkt.Samia mamlaka hiyo imeendelea kupata idadi kubwa ya watalii na ongezo la mapato yatokanayo na shughuli za utalii hifadhini.

"Ongezeko la idadi ya wageni katika Hifadhi ya Ngorongoro limekuwa na matokeo chanya kwenye ongezeko la mapato yatokanayo na utalii.

"Mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 171 mwaka 2022/2023.

"Hiki ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kukusanywa na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro. Hata hivyo, mapato yanategemewa kuongezeka zaidi na nakufikia takribani shilingi bilioni 200 kwa mwaka.

"Kwani katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2023/2024 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 123 tayari zimekusanywa.

"Mapato haya yameongezeka kwa asilimia 13 ukilinganisha na mapato yaliyokusanywa katika kipindi hicho hicho kwa mwaka 2022/23."

Pia, amesema katika kufufua sekta ya utalii mara baada ya UVIKO 19 kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour, juhudi hizo za Mheshimiwa Rais Dkt.Samia zimechangia ongezeko kubwa la idadi ya wageni wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro hadi kufikia wageni 752,232 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ikilinganishwa na wageni 191,614 waliotembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mwaka 2020/2021.

"Idadi ya wageni wanaotembelea hifadhi inatarajiwa kuendelea kuongezeka zaidi na kufikia takribani wageni 1,000,000 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hususani katika nusu ya kwanza ya mwaka 2023/2024 Hifadhi ya Ngorongoro imepokea wageni 534,065.

"Idadi hii imeongezeka kwa asilimia kumi ikilinganishwa na idadi ya wageni waliotembelea hifadhi hii katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/2023."

Ofisi ya TR

Awali,Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Msajili wa Hazina Thobias Makoba amefafanua kuwa,Ofisi ya Msajili wa Hazina ilianzisha utaratibu wa kukutanisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini na taasisi yakiwemo mashirika ambayo inayasimamia tangu mwaka 2023.
Amesema,lengo la vikao kazi hivyo ni kuzipa nafasi taasisi hizo kuelezea kuhusu utekelezaji wa mambo mbalimbali ambayo wanayatekeleza kwa niaba ya wananchi na mafanikio ambayo wameyapata ili umma ambao ndiyo wamiliki wake waweze kupata mwelekeo wa taasisi zao.

"Kama mashirika hayajulikani na haijulikani yanafanya nini, ni vigumu umma kuweza kupata uelewa juu ya mashirika haya. Hivyo, vikao hivi ni muhimu sana kwa umma kuweza kupata taarifa sahihi na mafanikio ya taasisi hizo.”

Amesema, NCAA ni miongoni mwa mamlaka ambazo zinasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika Sekta ya Utalii nchini, kwani licha ya kuchangia pato la Taifa pia imekuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa Watanzania hususani vijana.

Makoba ameipongeza,NCAA kutokana na kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo hivyo kurahisisha mchakato wa kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi.

Amesema,ofisi hiyo imejipanga vizuri katika kuhakikisha kila Mamlaka iliyo chini yake inafanya vikao vya mara kwa mara na waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya Umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya Sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Ofisi inayojitegemea kimuundo.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) Ofisi ilikabidhiwa majukumu ya Shirika hilo.

TEF

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatious Balile, Mjumbe wa jukwaa hilo, Jane Mihanji amesema vikao kazi hivyo ni jukwaa pana ambalo linawakutanisha wanataaluma ya habari na wataalamu mbalimbali kutoka taasisi za umma ili kuweza kupata uelewa wa kutosha.
"Msajili wa Hazina amekuwa ni mdau mkubwa wa tasnia hii ya habari, kwa maana ya kutambua umuhimu wa vyombo vya habari na huduma ya habari katika jamii,na ndiyo maana ametoa msukumo kwa taasisi za Serikali ambazo ni za umma.

"Zimekuwa zikifanya mambo mengi sana makubwa, lakini hayajulikani,"anasema Mihanji huku akifafanua kuwa, ushirikiano huo unawezesha vyombo vya habari kuujulisha umma kuhusu yale ambayo yanafanyika katika taasisi husika ikiwemo mafanikio yake.

Pia, ameipongeza mamlaka hiyo kwa juhudi kubwa ambazo inaendelea kuzifanya katika kuhakikisha sekta ya utalii kupitia Eneo la Hifadhi la Ngorongoro inazidi kustawi kwa manufaa ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news