Wahujumu uchumi Zanzibar matumbo joto, Rais Dkt.Mwinyi aagiza

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameagiza taasisi zinazohusika na sheria kukamilisha mchakato wa utungaji wa sheria ili kuanza kazi kwa Mahakama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa mwaka huu.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo Februari 7,2024 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar katika viwanja vya Mahakama Kuu Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha mhimili wa Mahakama na taasisi zote za sheria ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Rais amesema, hatua hizo ni ujenzi wa majengo saba ya Mahakama katika mikoa na wilaya Zanzibar, kuongeza idadi ya Majaji, Mahakimu na Makadhi pamoja na kuboresha maslahi kwa Majaji, Mahakimu, Makadhi na watumishi wengine wa taasisi za sheria ili kuongeza ufanisi.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema, ustawi bora wa wananchi utategemea kuwepo kwa misingi imara ya kuheshimu haki za binadamu, utawala bora, uhuru wa Mahkama pamoja na sheria madhubuti zinazoilinda jamii dhidi ya aina zote za unyanyasaji.

Vilevile Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza Mahkama ya Zanzibar kwa kuanza mchakato wa kuboresha mfumo wa kieletroniki wa usikilizaji wa mashauri kwa msaada wa kitalaamu kutoka Mahakama ya Tanzania.

Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amezindua mpango mkakati wa miaka mitano wa Mahakama (2024-2029) na kukabidhiwa ripoti ya utendaji kazi wa Mahkama ya mwaka 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news