NA RESPICE SWETU
WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma waliofanya vizuri kwenye matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na kidato cha sita iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana, wamepewa tuzo ya vyeti na pesa.
Tukio hilo lililofanyika katika ukumbi wa chuo cha ualimu Kasulu, lilitumika pia kutambua mchango wa wahisani na wadau mbalimbali wa elimu wanaofanya shughuli zao kwenye halmashauri ya wilaya ya Kasulu.
Akizungumzia tukio hilo, kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Emmanuel Ladislaus alisema, pamoja na siku hiyo kuandaliwa kwa ajili ya utoaji wa tuzo hizo, itumike pia kuashiria kuanza kwa muhula na mwaka mpya wa masomo kwa halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, afisaelimu msingi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Elestina Chanafi, aliiitaja siku hiyo kuwa ni siku ya elimu kwa halmashauri ya wilaya ya Kasulu iliyoandaliwa kwa ajili ya kujipongeza na kujadiliana kuhusu namna ya kuendelea kufanya vizuri katika mitihani hiyo.
Alisema pamoja na majadiliano hayo, halmashauri ya wilaya ya Kasulu imeongeza wigo wa tuzo zitakazoyafikia makundi mbalimbali ya walimu pamoja na shule zilizofanya vizuri kwenye mitihani hiyo.
Miongoni mwa makundi yaliyonufaika na tuzo hizo, ni walimu waliofaulisha kwa kiwango kikubwa katika masomo yao, waliowezesha kwa asilimia 100 stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la pili na walimu waliowezesha vema umahiri wa somo Kiingereza kwa wanafunzi wa darasa la tatu.
Wanufaika wengine wa tuzo hizo walikuwa ni walimu wa shule zilizoongeza ufaulu kwa kiwango kikubwa, usimamizi bora wa kituo cha elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi na walimu wa kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Awali kabla ya kukabidhi tuzo hizo, afisaelimu wa mkoa wa Kigoma Paulina Ndigeza aliyekuwa mgeni rasmi kwenye tukio hilo, alikagua maonesho ya zana za kufundishia na kujifunzia zilizooneshwa na wadau mbalimbali wa elimu.
Miongoni mwa wadau walioshiriki kwenye maonesho hayo ni pamoja na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulika na uokoaji IRC, shirika la Save the Children na World Vision.
Akiahirisha kikao hicho, afisaelimu wa mkoa wa Kigoma alitoa pongezi kwa wazazi, wadau na walimu wa shule za msingi na sekondari wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Alisema, ufaulu wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu umeuinua mkoa na kuufanya kuwa katika nafasi nzuri.
“Matokeo yenu yameuwezesha mkoa wa Kigoma kutoka katika nafasi za chini kama zamani, sasa hivi nikienda popote natembea kifua mbele na kujitambulisha bila kuona aibu kuwa ninatoka mkoa wa Kigoma, hongereni sana Kasulu” alisema.