ZANZIBAR-Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab amewataka wanamichezo wa Kikosi cha Valantia Zanzibar kushirikiana katika sekta ya michezo ili kuimarisha na kukuza maendeleo ya vipaji vilivyopo nchini.
Ameyasema hayo mara baada ya kukabidhiwa makombe kwa mabingwa wa ligi za Mapinduzi Netball, Basketball pamoja na Ligi ya Muungano kwenye sherehe fupi iliyofanyika Ukumbi wa KVZ Mtoni.
Amesema, michezo inatoa fursa mbalimbali hivyo wanamichezo kuendelea kumpa nguvu Mkuu wa Kikosi ili kupata maendeleo zaidi na kufikia malengo yanayotakiwa na Serikali katika kukuza sekta ya michezo hapa nchini.
Katibu Fatma ameongeza kuwa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekua mstari wa mbele katika kuimarisha sekta ya michezo ambayo inaonekana kukuwa siku hadi siku.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Valantia Zanzibar, Said Ali Juma Shamhuna alisema ataendelea na juhudi za kuinua michezo ili kupata vipaji bora.
Alisema, ni vyema baadhi ya timu kufanya jitihada katika mashindano wanayoshiriki ili kukitangaza kikosi ambacho kina wanamichezo imara ambao wataitangaza Zanzibar kwenye ulimwengu wa michezo.
Akitoa shukrani Mkuu wa Utawala, Kanali Juma Hussein alishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano sambamba na kuahidi kuendeleza maendeleo ya michezo kwa kupatikana kwa vijana hao.
Katika sherehe iyo kulikabidhiwa kombe la bingwa wa Zanzibar Netball, mshindi wa pili Ligi ya Muungano Netball, bingwa wa Zanzibar Mapinduzi Cup Netball na bingwa wa Zanzibar Mapinduzi basketball.